Tuesday, November 8, 2011

Kina kabla ya uhuru

Hawa ninawaambia, kabla walozaliwa,
Uhuru kuingia, Tanganyika na Zanzibar,
Tuwatunuku hidaya, ila kuongoza baa,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!



Mtakuwa ni raia, haki zote mtapewa,
Ila kutusimamia, hilo tunalikataa,
Nchi mmeifumua, kushonwa inatakiwa,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Vijana wanatakiwa, kompyuta kuzivaa,
Ofisini wakikaa, wajua yanayotokea,
Mizubao na sinzia, kuondoka ni huria,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Twataka wanaojua, uchumi kuutibia,
Isiwe tunaugua, malale na kusinzia,
Hoja kuzichanganua, miradi ije tufaa,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

KazI mmeshatufanyia, nchi ni kutuachia,
Ushauri kuutoa, pembeni mmesogea,
Nasi tutawachambulia, Tanzania kuja paa,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Wenyewe kujichagua, bila jina kwangalia,
Ujuzi umejaliwa na kazi unaijua,
Ndani utajaingia, ufanye ya manufaa,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Barabara kujijengea, hatua tutazichukua,
Reli kukarabatia, msaada si ruia,
Na umeme kusambaa, hiyo kazi ya siku moya,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Maji tutawamiminia, maziwani kuyavua,
Mito tutajihamia, yazidi maji kujaa,
Na misitu kuridhia, wananchi kujilindia,
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

Ardhi hatutaigawa, kwa wageni bila ubia,
Hati tutatishikilia, hadi kijapo kiyama,
Nani wa kutununua, na sisi wote wazawa?
Kina kabla ya uhuru, baibai mnapewa!

No comments:

Post a Comment