Tuesday, November 8, 2011

Siasa na umafia

Yabadilika dunia, na ujanja unakua,
Ili kutokudhaniwa, jambazi polisi hua,
Vigumu kutuhumiwa, wadhifa anaopewa,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'



Padri ukishakua, nani atakudhania,
Zinaa ukiingia, na uchafu kukujaa,
Wengine watashukiwa, salama utabakia,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Ustadhi ukishakua, mcha Mungu wakujua,
Uovu ukipania, gizani hawatajua,
Siri utajifichia, hadi zizidi tamaa,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Na siasa nazo pia, upupu zinachukua,
Fikra zazidi via, nani anayefikiria,
Roboti utadhaia, wanayozungumzia,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'
Watu wasio ulua, fani wameivamia,
Kuiba waazimia, ni nani atawajua ?
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Uongozi wakikwaa, ganzi wameshajipatia,
Mbwa mwitu hujavaa, ngozi ya kondoo mliwa,
Kundini wakishaingia, kazi yao kutanua,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Wanono watajilia, tena kimya kimya,
Hakuna atayejua, hadi mtu kufichua,
Ila taifa huvia, na kuzidi kusinyaa,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

Na vyama vyajatokea, udokozi kuulea,
Hazina kujaingia, kila kitu kupakua,
Pasiwe cha kubakia, ilo mifupa masalia,
Watu kinachoibia, si chama hao 'mafia.'

No comments:

Post a Comment