Tuesday, November 8, 2011

Sasa vuta nikuvute

Lazima nchi itwete, na kujakauka mate,
Watajatembea viwete, zikijageuka kete,
Na watu lazima mtote, kwa jasho pia matete,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!


Hali hii sasa tete, mambo vuta nikuvute,
Watu wataka wapate, si skuzote waote,
Ndoto wazitema mate, na hawataki mfute,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Ahadi kwao uwete, hungoja usiwakute,
Ni puya wazipepete, nafaka wasipukute,
Wengine msinifate, uoga jadi ya wote,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Nakukumbuka Mnete, Ujerumani usinate,
Njoo tuhidi viwete, hata kidogo waokote,
Na neema uilete, misada waipate,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Kila mtu ana kete, ataka naye apate,
Hatoishi kwa mkate, mtu anataka vyote,
Kwa hili msimsute, suteni nafsi zote,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Mtapoenda popote, chunguzeni na mtete,
Ili amani iote, fanaka iwe kwa wote,
Watu lisiwakerekete, la kukosa wao mkate,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Na hata vipi mnyate, gizani vyenu mng'ate,
Bado hudondoka mate, usingizini waote,
Kuteketea si lolote, na umauti ni wa wote,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Naomba yasinikute, nilapo wote niite,
Hata kidogo nipate, tutagawana na wote,
Na Rabana asisite, kichache aje avute,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

Utupe leo mkate, peke yetu tusifute,
Na wenzetu waupate, slensi isiwapite,
Baadaye nisijute, kwa ubinafsi nisutwe,
Sasa vuta nikuvute, mtu ataka apate!

No comments:

Post a Comment