eri wa mali ni mwizi, wa kura ni muuaji,
Haki anaidarizi, kumpa aso na mji,
Ni msanja wa kunazi, haubebi hata maji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Anamzidi jambazi, kura anayezifoji,
Si mthamini kizazi, huyu wa wazi mkabaji,
Anajal imatanuzi, na ukubwa kuuhiji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Hana radhi ya mazi, huyu ni mgeuzaji,
Na kinyesi na ushuzi, kwake yeye upambaji,
Ukilifanya fumanizi, usiache utekaji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Ni gunia la viazi, lisilo na mbebaji,
Kunyanyuka haliwezi, hadi aje mchukuaji,
Ni chombo kisicho kazi, kutupwa ni mataraji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Tabia yake ushenzi, hata ikiwa ya jaji,
Huuzwa kwa manunuzi, haki tusijeitaraji,
Ni mbegu za maangamizi, hazifanzi uokoaji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Havistahi makuzi, ni kama mnenguaji,
Kiuno bila shimizi, ndio chazidi kuchaji,
Na ya jana sio juzi, hautaivaa beji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Kibirizi, kibirizi, mlinzi na mauaji,
Hili ni kama jinamizi, kuponya linahitaji,
Na usalama si wizi, kama hivyo hatuuhitaji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Utu sio sisimizi, watu viumbe hojaji,
Usitumiwe kama ngazi, kesho haitakufariji,
Kama umekosa kazi, kwingine tafuta mtaji,
Kuiba mali ni wizi, kuiba kura mauaji!
Tuesday, November 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment