Nchi haitoendelea, bila mkoa huru kuwa,
Maamuzi kujifanyia, bila ya mtu kungojea,
Na awe nayo raia, sauti ya kusikiwa,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Arusha yasingetokea, leo yanayotokea,
Mkoa unatawaliwa, na chama chenye izaya,
Wajanja walipokwapua, kile wasichojivunia,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Mbeya ukiangalia, chama fulani chafaa,
Kuutawala mkoa, zingeliisha ghasia,
Uchumi wadidimia, king'ang'anizi kung'ang'ania,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Na Mwanzo nako pia, kama haya yatokea,
Uhuru wanalilia, wakazi wake mkoa,
Mambo yao kimkoa, wao wenyewe kuamua,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Wamechoka kuwekewa, viongozi wasofaa,
Na tena sio wazawa, uchungu nao hawajawa,
Angelikuwa mwana kaya, uchumi angelipaua,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Ardhi wanachukua, wa mkoa wasokuwa,
Juu walikokalia, wawekezaji wauzia,
Sasa wanagombania, ardhi kujilindia,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Mali asili tambua, ni ya wakazi wa mkoa,
Haijawa, haitakuwa, ya hao wanaopewa,
Tutaambiana ubaya, haya yakija tokea,
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Tuacheni kusinzia, haja za watu kujua,
Muda usijepotea, mabaya kujatokea,
Ama chelewa chelewa, mwana hutomkumbatia!
Mkoa lazima uwe, na waziri mkuu wake.
Tuesday, November 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment