Tuesday, November 8, 2011

Siasa kongwe na nzee

Mbali tuzitupilie, siasa kongwe na nzee,
Kale isituzuzue, tulipo hapo tutue,
Yajayo tutabirie, tupange tufanikiwe,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Hivi sasa tuamue, nani nchi tuwaachie,
Shughuli waifanyie, umaskini waondoe,
Watu watutumie, taifa juu lipae,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Tupumue, tusikae, mchakamchaka uwe,
Usia tukumbukie, baba taifa atoe,
Budi sisi tukimbie, acha wengine watembee,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Batabata tuwatoe, si mwendo watu uwafae,
Hatua tuzichukue, mbiombio tukimbie,
Malengo tuyafikie,dunia itushangae,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Majukumu tuyajue, kisha tushughulikie,
Katu wote tusitue, na wala tusitulie,
Nchi yataka itibiwe, na nafuu ipatiwe,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Matatizo tutatue, Watanzania wapumue,
Mbeleni tusiugue, maradhi yote yatibiwe,
Kivulini tuingie, kama walivyo wengine,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Haki tuizingatie, udikteta uvie,
Ukiritimaba tuue, na uhuru ukomae,
Ubabe tuukatae, na dola isitumiwe,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

Sherehe tusherehekee, sio wajisherehekee,
Wananchi chini wasiwe, ila juu watulie,
Dunia iwasifie, wajifunze na wajue,
Siasa kongwe na nzee, zinaturudisha nyuma.

No comments:

Post a Comment