MABADILIKO yanayotokea duniani yanawawia vigumu vikongwe wa kisiasa kuyaelewa na kuyatafsiri katika mtazamo na macho ya ulimwengu wa sasa. Kama ilivyo kawaida kwa mwanadamu hatua za kwanza wanazochukua ni kupambana ili kuzuia mabadaliko hayo yasijiri makwao.
Haijawahi kutokea katika nchi yoyote ile duniani kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kufanyika kirahisi na bila kuwa na upinzani mkali, mkubwa na wa kutisha toka kwa wattu waoga, mbumbu, wasiojua kinachoendelea, wanaonufaika na mfumo wa hali iliyopo au wale wanaotumiwa na wanaonufaika kuwalinda wao na mali zao.
Ninasema vyama vya siasa Tanzania vimepitwa na wakati kwa sababu kile kilichozoea ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja kinajiendesha kama wito na kazi yake kuu ni kupambana na wale wanaotaka kife; wakati wale wa iwezekanayo kuwa serikali mbadala na katika mfumo ambao si tofauti sana na wa chama kimoja katika mambo mengi, wanajiendesha kama vile kazi yao kubwa ni kuja kuingia madarakani kwa udi na uvumba. Hakuna kati yao ambaye anatoa uzito stahilifu kwa matatizo na changamoto za wananchi. Na kwa maana hii sio tu ninaona vimepitwa na wakati bali ninadhani vyama vyote havistahili hata kuwepo na nchi imekosa tu watu wanaoweza kuthubutu kuvifagia pembeni hata kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Mabadiliko ambayo Tanzania inastahili kuyafanya hivi sasa hayana tofauti kwa namna yoyote ile na mabadiliko mengine kama hayo yanayotokea kwingine duniani na yaliyokwishatokea pengine na katika karne nyingine huko nyuma yetu.
Tofauti tu iliyopo hivi sasa ni kuwa sisi kama watu mmoja mmoja na kitaifa hatujajipanga ipasavyo kuweza kuhakikisha kuwa mabadiliko hayo yanatokea kwa faida na manufaa yetu na sio kwa ujibari, ujivuni, kisirani na hasara kwa upande wetu.
Na katika hili kiongozi mkuu wa kujipanga kuyakabili mabadiliko anatakiwa awe ni chama cha kisiasa cnenye viongozi wanaojua watu wanataka kuelekea wapi, nchi inaelekea wapi, duniani inaelekea wapi, nani wanastahili kuwa rafiki zetu na nani hatustahili kuwaamini, kuwathamini na kuwaingiza katika siri na mambo yetu mengine.
Ni chama kinachostahili kuwa na mipango, mikakati, sera, muundo, mfumo, taratibu na kanuni za utekelezaji zinazokipa chama ukuu na nguvu juu ya mwanachama mmoja mmoja au kundi la wanachama fulani ndani ya chama husika katika mustakabali wa kujenga umoja wa chama lakini ndani ya mfumo wa demokrasia hai na inayofanya kazi. Ugonjwa wa 'ndivyotunavyofikiri' ukiachiwa kutambaa kwenye mwili-siasa wa jamii hivi leo ni dhahiri maradhi makubwa zaidi yatajitokeza na kupona kwa mgonjwa kutahitaji manabii na miujiza.
Ni chama ambacho kina 'visheni' na 'misheni' bayana ambazo wanaokiongoza hata wakikurupushwa usingizini wanavikariri bila kukosea hata neno moja.
Ni chama kinachotakiwa kuwa na mizizi yake vijijini zaidi kwa kukivewezesha vijiji na wanavijiji na sio mjini kwenye watu wachache na walioelimika vya kutosha. Ni chama ambacho ofisi zake vijijini vitakuwa ni vituo muhimu katika kazi zake mbalimbali na ofisi ambazo zina nafasi kwa ofisi za viongozi wa wilaya, mkoa na kitaifa na ukumbi wa mkutano ambao vikao vikubwa kwa vidogo vya chama vinaweza kufanyika huko bila wasiwasi na uwepo wa sehemu kama hiyo kuwa ni hamira au chachu ya maendeleo ya kijiji na wanakijiji husika.
Ni kawaida pia kinachopingwa, kupinga na kupambana na kile kinachokipinga. Lakini kwa jambo lolote ambalo wakati wake umefika ni muhali na kazi bure kulipinga. Ima-fa-ima lazima mabadiliko yanayopaswa kufanyika yatafanyika tu.
Ili kutopotezeana muda ni vyema kufunguana macho na kuhamasisha jamii kufagia yale yote yenye kunukia uzee au ukongwe usio na faida na ambayo yanaweza kusababisha kuvunjika kwa amani na umoja katika nchi hii eti tu kwa kuwa ukongwe huo unakataa mabadiliko yasitokee.
Hali ilivyo sasa ni kwamba wanasiasa waliopo wamezoea kutawala kwa kutumia mabavu na maguvu; udikteta na ukiritimba katika maamuzi na uendeshaji vyama; kusukumiza kwenye makoo ya raia zao katiba na sheria zisizokubalika; kupora mamlaka na madaraka ya wananchi kinyume na katiba; kutumia njia za haramu kupata mapato yao na ya chama; kutumia vyombo vya dola kwa faida na maslahi yake; uzaini na uongo; kununua na kuwatumia watu; kugawa na kutawala; kulea ukabila wa kichama kwa maana ya kuwabeba tu wanachama wa chama tawala kuwa viongozi na kuwaacha wasio wanachama bila kazi wala changamoto za maana katika kuendeleza wilaya au mkoa au taifa;
uroho, choyo, inda na ulafi wa hali ya juu kutaka kutawala hata pale chama husika kisipokuwa na sapoti ya kutosha; kutumia vyombo vya usalama vya taifa kwa matumizi binafsi na sio kwa maslahi ya kitaifa; kutumia vyombo vya habari kukwamisha uwazi na kudanganya badala ya kusema ukweli; Viongozi wasio na mwelekeo wa kuinufaisha nchi hii na watu bali zaidi wao wenyewe na watu wa nje, kutumia makundi ya kijamii kama vile wanawake, vijana, wazee, wazazi, wanavijiji, wanafunzi, walimu, wafanyakazi na kadhalika kwa manufaa yao na sio ya kitaifa au ya umma; kuwatumia waandishi habari kama askari wa kukodiwa kufanikisha malengo yao; kushirikiana na mafisadi na wevi kufanikisha malengo ya kichama; kuingiza udini na ukabila katika uongozi na uanachama; kutumiwa na viongozi wa nje wa serikali na makampuni kwa maslahi yao na sio ya Watanzania; kushindwa kujenga imani na kujiamini kwamba kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe tunaweza kunufaika zaidi kuliko kudanganywa kwa misaada toka nchi za nje ambayo ni sawa na mtu kupewa perememde wewe ukaibiwa kipande cha almasi au vito vingine vyenye thamani.
Mlolongo huo hapo juu ni ushahidi tosha unaonesha ni kwa kiasi gani vyama vya kisiasa nchini Tanzania vimepitwa na wakati na vinahitaji kufa au kupona 'kusasaishwa' ili sio tu viende na wakati bali viweze kutekeleza kwa ukamilifu na usahihi zaidi majukumu yao ya kisiasa, kijamii na kitaifa.
Ili kwenda na wakati vyama vya kisiasa vinastahili pamoja na mambo mengine kuwa na wanasiasa wasioshindwa na wasiotishika katika kutumia nguvu ya hoja, uchanganuzi, uchambuzi na ubunifu katika kuongoza na wanaostawi katika kutofautiana kimawazo, kifikra na kimaono.
Lazima kila chama kihakikisha kuwepo kwa demokrasia na uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa ndani na nje ya chama; kuruhusu kuwepo kwa katiba na sheria zilizoandikwa na wanachama au wananchi wenyewe na sio wao kama viongozi au watawala; na pia kutumia njia za halali na zinazokubalika na zisizowaumiza watu wengine kupata mapato yao na ya chama.
Ni wajibu wa chama chochote ndani au nje ya madaraka kuvhiheshimu, kushirikiana na kuvitumia vyombo vya dola kwa faida na maslahi ya umma na si watu wachache; na kujali usawa, haki na ukweli wakati wote.
Kila chama kinastahili kuthamini utu na ubinadamu wa raia wote; kujenga umoja katika tofauti za kiimani na kiitikadi; kukana na kuharamisha ukabila wa aina zote ukiwemo ule ukabila wa kichama, udugu, ujamaa na urafiki katika kazi na majukumu mengine ya kitaifa.
Chama lazima kidhibiti wakati wote uroho, choyo, inda na ulafi miongoni mwa wanachama na viongozi wake; kuwaachia wengine kutawala pale chama kisipokubalika na wakazi husika; na kutotumia vyombo vya usalama wa taifa kwa maslahi, matakwa na haja binafsi ikiwemo kuwachunguza viongozi wastaafu, wanaharakati na wanachama na viongozi wa upinzani.
KIla chama kinawajibika kutotumia vyombo vya habari kudanganya wale wenye uelewa duni wa mambo; kutowaweka waavijiji katika giza la kuelewa na kukubali kuwa demokrasia na vyama vingi ni jambo lenye manufaa kwetu kama nchi na watu; na pia kutowatumia waandishi habari kama askari wa kukodiwa kufanikisha malengo ya chama na viongozi wake.
Chama kinawajibika kutoshirikiana na matajiri na mafisadi katika kupora madini na maliasili za nchi hii; kutowagawa Watanzania katika makundi ya kijamii yanayoweza kuja kuwa hatari kwa taifa baadaye, k.m, vijana, wazee, wanafunzi, wanawake, wazazi wa chama fulani n.k.
Chama kiwe makini na kutoingiza udini na ukabila katika uongozi na uanachama; kutotumiwa na viongozi wa nje wa serikali na makampuni kwa maslahi yao na sio ya Watanzania; kufanikisha kujenga imani na kujiamini miongoni mwa Watanzania kwamba kwa kutumia watu wetu wenyewe, wazungu wasio na ajira makwao, rasilimali zetu wenyewe tunaweza kunufaika zaidi kuliko kudanganywa kwa misaada toka nchi za nje ambayo ni sawa na mtu kupewa perememde wewe ukaibiwa kipande cha almasi au vito vingine vyenye thamani na wewe ukaridhika na kuona ndiye uliyefaidi kuliko aliyefaidi kikweli.
Chama cha kisiasa sahihi na kinachostahili kuwepo katika karne ya 21 nchini Tanzania ni kile kitakachoweza kufanya mikutano yake mikubwa na midogo, kwa siku kama sio wiki kadhaa, katika kijiji chochote, mkoa wowote Tanzania kwani mikoa na vijiji hivyo vitakuwa na serikali na utawala bora unaoweza kukimu na kuruzuku mambo hayo kutokana na kuwezeshwa na chama husika na wafuasi wake na watu wengine wanaozingatia misaada kufika kule inakotakiwa na sio vinginevyo..
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment