Thursday, November 17, 2011

Muswada wa katiba na hatima ya nchi yetu...

AKIZUNGUMZIA uwezekano wa kuandikwa katiba mpya ya Tanzania kwa mara yake ya kwanza, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti na mwanachama wa Chama kimojawapo cha siasa nchini Tanzania, CCM, Bwana Jakaya Kikwete pamoja na mambo mengine alionesha kutamani sana kwamba katiba itakayoandikwa iweze kutufaa kwa miaka 50 kama sio 100. Hata hivyo, kile kilichowasilishwa na Waziri wake wa katiba hakikufanana kabisa na matamanio mema yake hayo.

Tofauti na msimamo huu wa mheshimiwa Rais, muswada wa serikali yake kwa bunge la Jamhuri ulidhihirisha nia ya serikali ya Chama cha Mapinduzi kuitumia fursa hiyo ili iweze kujikita vyema zaidi nchini kwa halali au haramu kisiasa kwa kuwatumia wabunge wao ambao ilionekana kama walishapewa mafunzo maalum kuhusu kinachotegemewa kutoka kwao.

Pamoja na spika wa bunge hilo kudai kwamba wanaharakati, wapinzani na waandishi wa habari wanapotosha kilicho mezani mwa wabunge, kazi nzuri ya uchambuzi wa kina iliyofanywa na Mheshimiwa Tundu Lissu (CHADEMA) ilionesha kulikuwa na uwezekano mkubwa wa wabunge wa CCM kutokuwa wameusoma muswada huo na Tundu akawa anapigia gitaa mbuzi.

Pengine wabunge wa CCM walishaambiwa kwamba ni lazima upite kama ulivyo na hakuna aliyesumbuka kuusoma kikwelikweli, lakini baadaye ilidhihirika waziwazi kwamba muswada huo ulikuwa na udhaifu mkubwa na kasoro nyingi za kimaudhui, kisheria, kisiasa na kikanuni kikatiba ambao kwa watunga sheria makini lazima wangelihitaji muda wa ziada wa kuufanyia kazi na sio kama wenzetu walivyoanza kuchangia wakiwa na uelewa 'finyu kiuzalendo' kwa kazi iliyokwa mbele yao.

Sio siri kwamba CCM inachokitaka pengine ni kujihakikishia uzima wa milele. Kitu ambacho hakiwezekani. Na haitawezekana kwa sababu hizi si zama za Nyerere, Mkapa na Mwinyi na chochote kinaweza kutokea kwa watu ambao hali ya uchumi inawawia ngumu kila kukichwa, mali asili zao zinatwaliwa bure, watu wanauawa na kubakwa migodini na wakubwa wanapora fedha, wanyama pori, miti, ardhi na rasilimali nyingine kwa jinsi wanavyotaka. Na wasichonacho wananyang'anywa hata kile kidogo walicho nacho, wakati wenye nacho wanazidi kuongezewa kila siku.

Watanzania hawatakaa wasahau kwamba kunako mwezi Novemba, mwaka 2011 baadhi ya wabunge wao kupitia CCM walipoteza fursa ya kipekee katika kuutanguliza Utanzania mbele ya nafsi na uchama wao. Matokeo ya ubinafsi na uchama wao yakawapotezea fursa hii adhimu ambayo ingeliwaweka pazuri sana katika historia ya nchi yao na watu wake.

Kilichotokea ni kwa wabunge hao wa CCM-CUF kuonesha dhahiri kuwa ni mbwa-mwitu (wawakilishi wa chama na serikali) waliovaa ngozi ya kondoo (wawakilishi wa wananchi). Kipaumbele siku hiyo hakikupewa wananchi na vizazi vyao vijavyo bali chama, matashi yake na ubinafsi wa wabunge hata kama Watanzania kwa ujumla wao watapoteza kikubwa zaidi siku zijazo.


UCCM na UCUF kwa kiasi fulani katika hili umewafanya wengi waamini kuwa wabunge wa vyama hivyo wanastahili kupata shahada ya udaktari katika uchama, usisi, umimi na katika mapambano ya maslahi na maendeleo ya wabunge binafsi.

Kwa maneno mengine, wabunge wa CCM na CUF walikuwa wakituambia kwamba vyama vyao na uongozi wa chama chao ni muhimu kuliko Utanzania wetu au utaifa wetu, watu wetu na vizazi vyetu vijavyo.

Kubwa zaidi ni lile la spika, muwakilishaji muswada na wabunge wa CCM waliochangia muswada huo kusingizia eti kuna urongo, uzushi, upotoshaji na tafsiri mbovu ya kile kilichotakiwa kuwakilishwa. Haraka aliyokuwa nayo spika, wabunge wa CCM kuchangia na mwasilisha muswada na wenzake kuliacha maswali mengi kuliko majibu. Mwisho wa siku kilio cha spika, muwasilisha mada na wabunge wa CCM na CUF kilifanana na kile kilio cha mchunga kondoo aliyekuwa akisumbua wanakijiji wenzake kwa kupiga mayowe ya MBWA MWITU, MBWA MWITU kumbe yote ilikuwa ni mzaha kama sio urongo.

Uzaini wa CCM wa kujionesha eti wana CCM na viongozi wao wanaipenda na wana uchungu sana na Tanzania kuliko watu wengine umewafanya jamaa hao kuangukia pua katika siku ambayo wengi wao hawataiashau na wao wenyewe wameamua kujizika kihistoria.


CCM na wakewenza Unguja

Baya zaidi ni lile la muswada huo kudiriki kuifanya Zanzibar kuwa sawasawa na Tanganyika isiyopo katika kuamua hatima ya nchi yetu na watu wake. Hiki ni kitendo cha waendesha utumwa, kikoloni, kibabe, kihuni na cha kidhalimu ambacho hakistahili kukubalika.
Kwani nia ya kuwapa ukubwa huu Wazanzibari wasiostahili kuupata ni kurahisisha siasa ndani ya CCM kati ya Wazanzibari na Wabara. Kwa maneno mengine, CCM imediriki kuwauza Watanganyika kwa Wazanzibari, kama walivyouza migodi ya dhahabu, ili mradi tu mambo yao yawe safi.

Ukewenza Zanzibar na Serikali ya JMT, unatuweka pabaya kitamathali na kiuyakinifu kwa kiasi cha eti watu asilimia 2 Tanzania kuamua hatima ya asilimia 98 iliyobakia.
Kwa maneno mengine, muswada huo unawageuza Wazanzibar wakoloni na Watanganyika watawaliwa katika nchi yao wenyewe. Sijui hata kama muswada huo utapita kama hili litakaa likubalike kesho na keshokutwa.

Hadhi ya Zanzibar kiukweli haina tofauti na ya mkoa wowote bara. Tofauti tu ni kuwa mikoa inabanwa kuwa huru kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa mafaniko yake makubwa na haraka zaidi. Kilichokosekana ni uamsho kwa wakazi mikoani na uadilifu kwa serikali kuipa mikoa serikali huru zinazosimamiwa na waziri mkuu wa mkoa, baraza la mawaziri wa mkoa na wawakilishi wa mkoa na mikoa mingi tu ingeiacha Zanzibar nyuma kimaendeleo, bila ya visiwa hivyo kuona hata indiketa za mikoa hiyo kwenye mbio za ustawi wa jamii na maendeleo ya mkoa.

Itakuwa ni jambo la fedheha kama wabunge na serikali yetu baada ya kushindwa kuafikiana na wapinzani wa kweli ndani ya bunge itakuja kufanza hivyo kwa kupata shinikizo toka Marekani na EU. Jambo hili litaonesha kwamba viongozi wetu hawajaiva wala kukomaa na hakika hawastahili kuiongoza nchi hii kama kweli tunataka kuendelea na umoja na amani tuliyo nayo hivi leo. Kinachoonekana hapa ni kwamba kuna Watanzania wenye akili na uwezo mkubwa tu lakini kwa kukosa uongozi adilifu na mzuri wanashindwa kuwatumia.

Viongozi wa dini

Viongozi wa dini kama ilivyokuwa kwa wenzetu nchini Kenya wana mchango mkubwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na katiba nzuri na safi na itakayowafaa Watanzania kwa muda mrefu kuliko hii ya kupandikizwa ilivyotsukuma sukuma.

Yapo mambo kadhaa ambayo viongozi wa dini wanaowatakia Watanzania na vizazi vyao amani na umoja wanaweza kuhoji na kutoa mwongozo yaende vipi kwa faida ya watu wote. Mathalani, hivi leo kanisa katoliki linafanya vizuri sana katika elimu na sekta ya afya, lakini siasa za uziwi na upofu zinaweza kuhujumu haya yote kama katiba isipohifadhi sheria na haki muhimu za kulinda kanisa, mali zake na viongozi wake. Misikiti na Makanisa yakikaa nyuma, viongozi wa dini wasije anza kulalama baadaye kwamba katiba imewapendelea hawa, au kuwaonea hawa.

Makampuni na taasisi na katiba

Makampuni na taasisi kisheria ni sawa na mtu au raia. Makampuni na taasisi zikikaa nyuma na kutokushiriki kwenye mchakato wa katiba mpya yapo masuala mengi yanayoweza kuja kuzuka baadaye kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni yakaya kuwa ni kwa hasara kubwa kwa upande wao.
Katika suala hili lal katiba mpya sisi sote ni wadau na washiriki na hakuna anayestahili kubakia kuwa mtazamaji tu au juu ya wenzake kwa namna yoyote ile.

Muswada huu kama ilivyokuwa kwa miswaada mingine dhaifu, inayovuja na dhalimu kwa wananchi na vizazi vijavyo, imedhirisha mapungugu mengi mengine katika muundo, mifumo na taratibu zetu za uongozi na uendeshaji nchi. Baadhi ya kasoro hizi ni pamoja na hatari ya kuwa na wabunge wa kuteuliwa badala ya kuchaguliwa kwenye bunge la kiwakilishi; jinsi ambavyo serikali iliyoko madarakani inaweza ikapora mamlaka na madaraka ya wananchi na kufanya mapinduzi ya kikatiba bila kuwajibishwa ipasavyo; muungano unavyozidi kuonekana kukosa maana kwa Watanganyika na kuwa mzigo usiobebeka; na ule ukweli kuwa nchi bado imo kizani na haijajaliwa kuwa na kiongozi na wanasiasa wanaoweza kututoa kwenye shimo refu la giza ambalo tumejikuta tumo leo.

Pepe: sammy.makilla@columnist.com

No comments:

Post a Comment