Tuesday, November 8, 2011

Muungano kama hawa

Kitupu changu kibaba, japo ninaitwa baba,
Wanangu wananikaba, njaa yawapa adhaba,
Nimemlilia toba, naisubiri ratiba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?



Muungano ni mahaba, au kula na kushiba,
Kiwapi changu kiroba, nyumbani nikakibeba,
Abu, kazi ya bawaba, na mlango haujashiba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Jua njaa yake tiba, si dawa ila kushiba,
Iwe Dovya au Goba, waitaka hii tiba,
Hawaishi kwa ghiliba, utawaumbua msiba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Hata uvae majuba, njaa haina haiba,
Kwa kila mtu ni mwiba, kuzidi kuuziriba,
Na ukizikosa raba, donda huzidi mraba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Unguja si kama Pemba, Tanganyika si kisiwa,
Kukunana ni habiba, kibaba mpe kibaba,
Hukurubisha nasaba, na kuchipuka mahaba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Kazi wote kuzibeba, kubanana na kukaba,
Kutegea si haiba, husababisha msiba,
Wengine hawali riba,kuwaepusha ni toba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Kuukuza uswahiba, lazima wote kushiba,
Tuzieupuke kadhaba, na nyufa kuja ziziba,
Wafanye kazi ngariba, kutahiri waso hiba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

Namshukuru Hassaba. hesabu mwenye kutamba,
Atwepushe na ghiliba, ukweli ziwe hutuba,
Pasiwe wanaoiba, wakakwaza ukuruba,
Muungano ni mahaba, au kula na kushiba?

No comments:

Post a Comment