Tuesday, November 8, 2011

Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

NYIE hawatawafunga, mkifunga wapinzani,
Mbona mnayabananga,hamjui mwajizaini,
Dunia geuzi anga,wajinga hawabaini,
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Kutesa kwa zamu ringa, ila ujue yakini,
Wafunge watakufunga, kama haki hukuauni,
Usiombee kimbunga,kikukute mtaani,
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Hujatengwa na mtenga, wajua Raskazoni,
Mpingwa huja kupinga, ikawa abautani,
Mgongwa huja kugonga, ujikute hatarini,
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Sheria ukizipanga, jua na wewe undani,
Na kanuni ukitunga, jione nawe mpinzani,
Ujapoivaa khanga, usilisahau gauni,
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Ukiuchonga mzinga, na nyuki wabaini,
Asali ukenda kinga, kubali na yake faini,
Porini ukenda chunga, simba usiwaamini,
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Hukungwa naye mkunga, uzazi hauna dini,
Na mfungwa huja kufunga, Mandela hili aamini,
Ila sidhani kwa mwanga, iweje kuwangiwani?
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

Hutwanga mtwanga unga, na hili asibaini,
Nchi yataka waganga, haitaki majinuni,
Nchi yataka kuunga, nyie vipi mwabanduani?
Mkiwafunga wapinzani, nao hawatawafunga?

No comments:

Post a Comment