Tuesday, May 24, 2011

Ardhi, viwanja na mipango mji

WATANZANIA waliowahi kufika nchi za nje bila shaka wanajua fika kwamba, mojawapo ya eneo linaloheshimiwa sana na wenzetu ni viwanja vya michezo, bustani za kupumzikia, misitu midogo ndani na pembezoni mwa miji (inayotumika pia kwa mazoezi na michezo ili kulinda afya za wanamichezo ), maua, miti na utunzaji

wake.

Sio rahisi kwa wanasiasa na wenye fedha kurubuni idara ya ardhi na kupewa maeneo ya umma na serikali ya nchi husika ikaendelea kuwa madarakani. Hali kadhalika, heshima ya serikali na viongozi wake hutokana na hali ya ubora na usafi wa miji katika nchi wanazoziongoza.

Katika miji mbalimbali hapa Tanzania, sio tu kunazuka 'slamu' au makazi yasiyopimwa na yasiyoko katika mipango mji, lakini mamlaka zinazohusika zikishirikiana na wanasiasa, watumishi, viongozi wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa na matajiri sasa wana uwezo wa kugeuza hata maeneo au sehemu zilizopimwa na kupangwa kuwa pia slamu.

Kilichotokea katika wilaya ya Kinondoni nina hakika ni kitu kitakachokuja kugundulika sio muda mrefu kutoka sasa kuwa ni uoza au ugonjwa ulionea katika miji yote Tanzania.

Ninaamini uchunguzi ukifanywa na chombo huru katika miji yote hapa Tanzania, isipokuwa kwa ile miji michanga itagundulika kuwa hayo ya Kinondoni ndiyo hayohayo katika miji mingine Tanzania.

Mpaka makala haya yanapoandikwa tayari kashfa ya ardhi Kinondoni imekwishasambaa katika wilaya nyingine mbili za mkoa wa Dar es salaam, yaani, Temeke na Ilala pia.



Watu watakuwa wanajiuliza hivi inatokeaje bustani, viwanja wazi, misitu midogo na viwanja vya michezo na maeneo ya huduma muhimu kwa jamii vinauzwa halafu baada ya miaka kadhaa ndio jambo hilo linagundulika? Kuna uhusiano gani kati ya uchaguzi mkuu, Wizara ya ardhi, manispaa na mipango miji hapa nchini?

Je, serikali inastahili kushindwa kusimamia masuala ya ardhi katika miaka hii ya sayansi na teknolojia ya ramani kuwa kitu kinachofanyika kwa kutumia kompyuta? Au ni kwa sababu ya serikali, manispaa na wanasiasa kujipendekeza kwa wapiga kura na wapiga debe wao ndio maana sheria ya ardhi inakuwa ni kama mchezo wa kuchekesha?

Nini hasa chanzo cha 'uhalifu' katika masuala ya ardhi na kama sheria zilizopo zinatosha kuwatia adabu na mambo kama hayo yasiwe yanajirudia tena kila mwaka? Hayo ndiyo maswali ya msingi yanayostahili kuulizwa na kujibiwa.

Maswali haya yakiulizwa na kujibiwa bila ushabiki au watu wengine kuona wanaumbuliwa yatasaidia sana kuepuka sehemu zetu za mji zilizopangika awali kugeuzwa salamu na kukuza maeneo ya salamu katika miji yetu mbalimbali. Kubwa zaidi ni kuwa nchi ni mipango. Huu uswahili tunaoulea ili tupate kura hauwezi kutufikisha mbali. Tabia hii ikiendelea katika miaka michache ijayo tutajikuta tunapoteza hata vile tulivyofanikiwa kuvipata hivi leo.

Isitoshe kwa kuwa nchi hii inatamani sana Utalii na Huduma za Ukarimu kuiingizia nchi yetu pato la haja ni lazima tunywe dawa chungu ya kukata uchafuzi mipango wa miji yetu kwa namna ambayo inakuwa ni fundisho kwa wananchi wengine popote pale Tanzania.

Kwa wasiojua, miji misafi, iliyopangika, yenye bustani za kupendeza, viwanja vya michezo kwa wakubwa na watoto, misitu midogo ndani na pembezoni ya miji na vijito na viziwa vya uongo na kweli, ni KIVUTIO kikubwa kwa watalii kuliko hata baadhi ya maeneo mengine tunayoamini kuwa ni kivutio kwa watalii.

Pamoja na maswali hayo inafaa pia kuuliza maswali yafuatayo:

• Hivi Wizara husika, yaani, Wizara ya ardhi, haijabebeshwa mzigo mkubwa na dhamana nzito kuliko uwezo wake? Maana kuna wanaoona

saa zingine kuwa wizara hiyo yenyewe ni kama sheria kama sio katiba ya nchi ? Ni dhahiri kama hakuna haki na utawala wa kisheria katika masuala ya ardhi

katika jamii yoyote basi haki na utawala wa kisheria hauwezi kuwepo mahala pengine. Wizara na idara zake lazima ziwe mfano wa haki na utawala wa kisheria

katika nchi. Je, kuna haja ya wizara hiyo kutofautisha kati ya kazi kiini kwa wizara na zile zinazofaa kufanywa na mamlaka zitakazokuwa chini ya wizara hiyo?

Tunaweza kujifunza nini kwa mfano kutoka Afrika Kusini, Namibia na Botswana?
• Nani anastahili kudhibiti maeneo yaliyopangwa kwa matumizi mbalimbali katika miji yetu na kuhakikisha kuwa hayatumiki vinginevyo, piga ua?

Hali kadhalika, kuhakikisha jamii inapata bustani, viwanja vya kupumzika, michezo na vya huduma mbalimbali bila mikwara, kuchelewesha wala usumbufu wa aina

yoyote?
• Je, siasa za vijiwe na utaratibu wa kuwa wamachinga au wahangaikaji wengine wasiokuwa na kazi maalum wanaweza kujenga kijukwaa cha

saruji na kufanya eneo hilo kuwa lao unaingilianaje na sheria za nchi kuhusu ardhi ? Je, kuna chama chochote cha siasa kinachostahili kuwa juu ya sheria na

vifungu vya katiba vinavyohusu masuala ya ardhi na matumizi yake?
• Katika mada hiyo hiyo je, viwanja vya michezo vilivyochukuliwa na chama fulani cha kisiasa na kinashindwa kuvitunza na vingine vimegeuzwa

masoko na magulio,kwanini visirudishwe kwa wananchi ili wawekeze humo na kuwa na hisa sawasawa na kuwa na hisa katika kampuni za uzalishaji au huduma

au kibiashara?
• Je, ni kwa kiasi gani ukubwa na maguvu ya wanasiasa na utajiri wa matajiri wa Kitanzania unachangia kuharibu badala ya kuboresha

mipango miji yetu? Kwa upande mwingine ni kiasi gani udhaifu wa watumishi wetu katika wizara na idara husika na njaa na tamaa zao zinachangia pia katika hilo?

Nini kifanyike?
• Ni kwa kiasi gani pia kushindwa kwa serikali zetu mbalimbali kuwa na mipango inayorahisisha upatikanaji wa nyumba kwa wakazi wao mijini

na vijijini kunachangia tatizo hili?
• Hivi serikali inastahili kweli kuwa katika majengo ya kizamani katika kata moja tu ya Magogoni/Kivukoni, yanayokula nafasi kubwa na

kuchangia usumbufu mkubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakati serikali hiyo inastahili kuwepo Dodoma na majengo yake yaliyosambaa na

yanayoendana na karne ya sayansi na teknolojia ?
• Je, ni nini kitakachotokea Soko Kuu la Pamoja la Afrika Mashariki linapoanza kazi wakati kuna ‘nyufa; nyingi katika masuala ya ardhi na

matumizi yake hapa nchini? Tuisaidiaje serikali kuziba nyufa hizo?

Nini kifanyike

Ikiwa kweli tunataka miji ya kistaarabu, ambayo wanasiasa, ikulu, wizara au wenye fedha hawawi juu ya sheria ya ardhi mambo yafuatayo yafanyike:

• Paendeshwa ukaguzi maeneo yote ya ardhi utakaofanywa na chombo maalum kinachostahili kuwepo sikuzote ili kudhibiti masuala ya

mipango miji na matumizi sahihi bora ya ardhi nchini;
• Pale uvunjaji sheria utakapothibitishwa uamuzi wa kurudisha viwanja na maeneo yote yaliyogawiwa kinyume cha sheria, lazima ufanyike bila

mizengwe wala kuchelewa, hii ikiwa ni pamoja na viwanja au maeneo husika kurejeshwa kwa matumizi mahsusi na wavunja sheria kulipa gharama zote na

maafisa ardhi husika kutoruhusiwa tena kufanya kazi katika wizara au idara zake, Hii ina maana pia kwamba, wote waliofanya ujanja watalazimika kubeba

gharama za ubomoaji na ubadilishaji viwanja kuwa maeneo yanayostahili kuwa kama ilivyopangwa awali.
• Kuhakikisha kwamba, ramani zote za miji zinakuwa katika kompyuta na wavuti maalum ya taifa inayohifadhi ramani na mipango miji yote.
• Katika miaka hii ni muhimu kwa serikali asubuhi na mapema kuanza kununua maeneo na nyumba zenye utata kwanza na baadaye maeneo

yanayopaswa kuwepo maeneo na huduma za kijamii na kadhalika,ili kupatikane bustani, viwanja vya michezo na vya kupumzikia katika kila kata mbili kama sio

moja.

Ili tuendelee kulinda amani na umoja wetu na imani ya wananchi kwa serikali yao, ni lazima masuala ya uuzaji na ununuzi ardhi yawe wazi na yanayofahamika na

ngazi zote kuanzia mwenyekiti wa mtaa hadi Baraza la Mawaziri na Ikulu wakati wote. Kama patakuwa na mtandao wa kompyuta stahilifu hii sio kazi kubwa.Utawala

wa sheria katika suala la ardhi na matumizi yake ni jambo la kheri kwa wote, walioko madarakani na wapinzani wao kadhalika.

No comments:

Post a Comment