Saturday, May 7, 2011

Bajeti: Utaratibu wa kimapokeo uliopitwa na wakati

TOFAUTI na Mjerumani ambaye alichukulia Tanganyika na Afrika Mashariki kama kampuni katika uendeshaji wake, Mwingereza alizichukulia nchi zetu kama mashamba ya vibarua.

Sitaki kuingilia sana juu ya tofauti kati ya utawala wa Kijerumani na Kiingereza, itoshe tu kusema utawala unaoichukulia nchi kama shamba aghalabu maamuzi yake hufanywa na mwenye shamba bila ya kuwashirikisha wale aliowaajiri au washikadau wenzake.
Mwenye shamba daima hufikiria kiasi cha mavuno au mifugo atakayopata lakini kamwe hana habari na kutunza na kuliendeleza shamba na hasa kama ni la kukodi.

Mtindo huu wa uongozi ndio uliorithiwa na Tanganyika na baadaye Tanzania katika kubuni, kuendesha na kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi tuliyomo leo. Tulimkataa mkoloni, lakini yake mengi ya 'uoza' tuliyarithi.

Kwa miaka zaidi ya arobaini na nane hakuna aliyekaa na kujiuliza kama bajeti ya kimapokeo kama ilivyorithiwa toka kwa mwenye shamba Mwingereza ndiyo inayoweza kwa kweli kuleta mabadiliko watu wetu wanayotarajia kuyaona katika maisha yao.

Binafsi, ninaamini mia kwa mia kuwa mfumo wa bajeti tuliourithi hauwezi kamwe kututoa kwenye umasikini hata kwa miaka mingine 48.

Kasoro ninazoziona

ZIPO kasoro nyingi ambazo baadhi yake nitazionesha hapa chini. Hata hivyo, ninaamini kwa wataalamu wa mambo ya utawala, uchumi na menejimenti yake wataweza wakipenda baadaye kuongeza kasoro nyingine nyingi tu.

Sio bajeti ya Kidemokrasia. Hii ni bajeti ambayo hufanywa kwa siri na kuwashirikisha watu wachache tu katika nchi. Inawezekana kabisa kwamba hata wabunge ambao wanatuwakilisha na wao pia hushtukiziwa kwa mara ya kwanza kwa kile kilichomo humo kusomwa na kusikilizwa sawa na wananchi wengine. Usiri huu wa bajeti katika miaka hii ya ufisadi na ubabaishaji una hatari kubwa ya kuruhusu urongo, ubinafsi, upendeleo, uonevu na udanganyaji wa kila aina.

Inajali zaidi namba na sio endelevu na ina upungufu katika kumbukumbu za kitaifa. Bajeti hii ya mapokeo pamoja na mambo mengine hujali zaidi namba au tarakimu kuliko majukumu na wajibu wa serikali kimaendeleo. Nia na mwelekeo wa uwezeshaji wananchi kwa maana kile serikali inachoweza kukifanya kwa kutumia rasilimali asili na watu, fedha ya hazina inayokaa bila kuwa na kazi yoyote na vilevile mabenki na vyombo vingine vya fedha hayako bayana kama inavyopaswa kuwa kwenye nchi yenye nia ya kweli kuwaendeleza watu wake. Bajeti sio tu ni kusoma mapato na matumizi ya serikali bali muhimu zaidi ni chombo kinachoweza kuamua kama nchi inaendelea kuwa masikini au inaukata.
Mwelekeo huu ni nadra sana kuonekana kwenye bajeti za Tanzania na Afrika kwa ujumla. Hii pengine ni kwa sababu serikali bado inaendelea kuamini kwamba ni chama fulani kinachoweza kuleta maendeleo na sio wananchi katika umoja na wingi wao.

Inasukumwa zaidi na siasa kuliko kitu kingine. Kila bajeti inayotangazwa sikuzote nyuma yake zipo hisia na pengine ushahidi unaweza kupatikana kwamba, huwa inasukumwa zaidi na masilahi ya kisiasa kwa walioko madarakani na hazina wito wa dhati wa kutaka kubadili hali ya Mtanzania.

Ni ya kitaifa zaidi kuliko ya kimtaa au kimkoa. Ni dhahiri kuwa ukubwa wa nchi yetu ni jambo ambalo halionekani na wengi kutokana na upofu wa kisiasa unaohofia kuwa kuipa mikoa madaraka ya kiuchumi ni tatizo badala ya kuwa fursa ya kiuchumi na ya kusukuma mikoa mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi. Kujilimbikizia sauti ya maamuzi na majukumu ya utekelezaji, hata hivyo, kunachangia sio haba mawaziri kupuuza wakuu wa mikoa na wilaya na kufanya maamuzi toka Dar es Salaam yanayogusa maisha ya kila siku ya wakazi wa wilaya na mikoa husika bila uoga wala kuona wanaingilia mambo ya mkoa. Mathalani, tukio la hivi majuzi la Wachina kuruhusiwa kuchimba dhahabu Chunya na Wizara husika. Hayo achilia mbali, lakini hivi kweli tukijiuliza kama nchi hii inaweza kubadilika kwa mfumo wa wizara ambazo zote ziko Dar es Saalam na ambazo mara nyingi ni za kimwitikio (reactive) na sio za uzuzi, ubunifu na uazsihaji mapya (pro-active) tutakaa tufike au tuendelee? Na je, maendeleo yetu yanatakiwa kuanzia chini kabisa au yanastahili kuanzia juu ndiyo yashuke chini ?

Inatilia mkazo zaidi matumizi au gharama na sio mapato. Ili nchi iendelee lazima bajeti yake ilenge zaidi katika kuwa chachu ya uzalishaji mali, utoaji huduma, biashara na ujasirimali katika sekta mbalimbali ili mapato ya nchi yaongezeke na hivyo mapato ya serikali nayo kukua kwa haraka na kasi zaidi.

Haitambui kuwa kupunguza gharama ni mbinu mojawapo ya kuongeza pato la taifa. Kwa wasomi wa mambo ya bajeti za umma na fedha, njia mojawapo ya kuongeza pato la nchi ni kupunguza gharama za serikali. Ukinunua magari madogo yasiyozidi bei ya milioni 20 badala ya magari yanayouzwa kwa milioni 50 tayari si tu umeokoa fedha nyingi katika ununuzi huo bali pia katika unywaji dizeli na petroli na gharama nyingine za uendeshaji wake. Ukipunguza safari za nje na idadi za wanaokuwemo katika misafara hiyo pia unakuwa unaliingizia taifa pato la haja. Kadhalika, ukijenga hosteli katika kila nchi ambayo tuna ubalozi ili viongozi wetu wakae humo badala ya hoteli kubwa, unakuwa umeliingizia taifa mabilioni ya fedha fumba na kufumbua.

Haizui mianya ya uvujishaji kodi. Wapo wanaosema kwamba tukikaa na kujipanga ipasavyo kama kampuni badala ya shamba la bibi, tuna uwezo mkubwa wa kufichua mianya mbalimbali inayovujisha pato la taifa ikiwemo ile katika uvunaji na uuzaji mali asili, upotevu wa maji na umeme kutokana na njia chakavu, mikataba mibovu ya ununuzi na uchotaji kiujanja fedha katika taasisi kama vile mifuko ya hifadhi, bima ya afya na mamlaka mbalimbali. Hii pengine ni sababu mojawapo inayowafanya wafanyakazi waamini kuwa ina uwezo wa kuwa na fedha za kuwalipa lakini haijakaa mkao safi wa kufanya hivyo kutokana na utendaji wake wenye mashaka kiuchumi.

Haiwachukulii wananchi kama wenye hisa au wenye kampuni. Bajeti hii haiko katika mkao wa kuwachukulia watu katika vikundi, mitaa, tarafa, majimbo, wilaya na mkoa kama kampuni na wakazi kama wenye hisa.

Inalea Utegemezi. Bado bajeti zetu kwa kila hali zinajenga sio utegemezi bali ile hali ya kutaka kutufanya tuamini kwamba walioko madarakani ndio tu wanaoweza kutuletea maendeleo na sio sisi wenyewe wananchi wa kawaida katika maeneo yetu mbalimbali. Dhana hii isipotoweka bajeti itaendelea kuwa jembe la mkono badala ya kuwa trekta. Upo uwezekano mkubwa wa wananchi kutoa mchango wa hali na mali katika maendeleo yao ili mradi wahamasishwe na kuongozwa ipasavyo. Upo uwezekano wa wafadhili kusaidia mtaa, kata, tarafa, wilaya na mkoa na tofauti ikaonekana ili mradi tukubali kuwa maendeleo kutoka Dar es salaam kwa nchi nzima.

Hakuna utundu na uvumbuzi. Bajeti zetu nyingi ni za ki-oto (automatic) na ubadilishaji wala sio uboreshaji wa kile kilichotangulia. Aidha, hakuna juhudi inayoonekana katika kuandaa wataalamu wa mambo ya fedha na bajeti wenye upeo wa juu na watakaokataa kufanya kazi katika matakwa ya kisiasa ila kwa kufuata utaalamu, hekima na busara zao za kitaarafu.

Hakuna kipaumbele mahsusi. Kuna kipaumbele cha ujumla kwa majina ya wizara na kadhalika, lakini hakuna kipaumbele mahsusi kinachotamka bayana kwamba tutaendeleza labda Mkoa wa Rukwa ili uzalishe mahindi yote yanayohitajika Tanzania; au tutaendeleza tu utalii mkoa wa Arusha, Mara na Kilimanjaro ili mapato yatakayopatikana huko yasaidie maendeleo ya sekta hiyo katika mikoa ya kusini; au tutaendeleza vijana wetu katika soka, Teknohama, Lugha na kadhalika ili 'tuwauze' nchi za nje kwa faida na wawe wanatuingizia mabilioni kila mwaka; au tutachangia maendeleo ya shule na hospitali katika mikoa ya mpakani ili zipokee wanafunzi kutoka nje na hospitali zipokee wagonjwa kutoka nje ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni!

Baada ya bajeti hii, CAG asiangalie tu mapato, matumizi katika taarifa zake, lakini aende hatua moja zaidi na kuishauri serikali kwamba sserikali kubwa ni mzigo usiobebeka kwa wananchi. Tuangalie uwezekano wa kuwa na wizara zisizozidi 20 na kuipa mikoa nchini uhuru wa kujitawala katika masuala yao ya kijamii na kiuchumi mapema iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment