WATU husema kila jambo lina wakati wake. Juma hili limeshuhudia taarifa za tafiti kadhaa ambazo pamoja na mambo mengine zimeonesha kuwa kinachowakera sana Watanzania hivi leo ni rushwa na mengine yanafuatia.Ni kipindi kilichoshuhudia pia ahadi toka kwa kiongozi mkuu wa ndugu zetu wa Usalama wa Raia kwamba wanakuja na mikakati mipya ya kulifanya jeshi hilo liwe safi na linalokubalika, sio tu na Watanzania bali na Afrika nzima kama mfano wa kuigwa.
Kutokana na wao polisi kuonesha angalau nia ya kufanya jambo jema makala haya ninawatunza wao pamoja na yaliyomo ambayo yanaongeza kuwapanua mawazo juu ya kile kinachostahili kufanyika ili azma yao isiwe wimbo utakaosahaulika baada ya muda si mrefu.Kwanza, tukubaliane kwamba, matatizo ya jeshi la polisi sio rushwa tu. Kuna matatizo mengi ambayo kwa umoja wao ndiyo yanayochangia watu kuwa na alama ya ulizo kila saa juu ya utendaji kazi wa jeshi hilo.
Baadhi ya matatizo ya jeshi hilo ni yale ya baadhi yao kukosa wito; tamaa ya kutaka kutajirika haraka haraka kutokana na kujifananisha na wengine; wakubwa wenye ajenda zao nje ya usalama wa raia na mali zao; elimu ndogo ya uraia na uzalendo na uamsho wa chini juu ya wajibu wa polisi katika kukuza na kuimarisha demokrasia changa.Aidha, polisi wana matatizo ya zana na vifaa vichache na duni; kukosa
maendeleo katika matumizi ya teknohama, makazi bora, maslahi ridhishi, nafasi finyu za kujiendeleza ili kukabiliana na mazingira ya nchi na ya dunia yanayobadilika kila leo.Lakini la ajabu kwa upande wangu mimi ni kuwa matatizo haya yote yanaweza kutatuliwa kwa jeshi hilo likisaidiwa na serikali kujipanga upya ili kumaliza ile hali ya mitaa na barabara zetu kuonekama kama vile hazina au hazifuati sheria hata kidogo.
Muulize mtu yeyote anayetoka nchi iliyostaarabika na
atakuambia anachokiogopa sasa hapa nchini zaidi ya rushwa ni kutokuwa na utawala wa kisheria unaofanya kazi.Hili linaashiria kwamba, kuna kazi kubwa sana ya kuleta mabadiliko ya msingi sio tu ndani ya jeshi la polisi, lakini pia katika jamii ya Kitanzania ambayo imeachiwa kwenda upogo na serikali kadhaa zilizotangulia pengine katika ile hali ya wazazi kumdekeza mwana na kumuachia kufanyaatakalo bila kuadabishwa.
Kwa hiyo kama tunataka mapinduzi ya kweli tukubali kuwa
tuanze na kukataa maadili na tabia mbovu tulizozilea hadi wa leo. Hili sio jambo dogo. Linahitaji waliopewa dhamana ya kutuongoza kukutana na wataalamu wa saikolojia na sosholojia ili hatimaye pawe na mkakati wa kupakua toka akilini mwa Watanzania takataka na uchafu mwingine uliomo humo na kisha kusafisha akili na bongo zetu sawasawa halafu kuanza kupandikiza uadilifu, haki, uaminifu, ukweli, utu na ubinadamu ndani yetu.Wakati tunasubiri hayo yatokee; maana kama tunavyowajua wanasiasa duniani hawana haraka na jambo, pengine ipo haja ya kuzungumzia mambo mawili matatu ambayo jeshi la polisi, serikali, kampuni za
simu za mikononi na watu kama 2-Mobile na wale wengine wenye majukwaa ya kupokea na kurushia taarifa wanaweza kuifanya ili jeshi letu la polisi litimize ndoto yake ya kuwa chombo safi na kinachokubalika na jamii.Kabla ya kufanya hivyo, lazima awali ya yote tubainishe ni nini hasa majukumu ya jeshi hilo.
Nitafanya hivyo kwa kuuliza maswali kwamba: Hivi katika karne hii ya sayansi na teknolojia ni kazi ya polisi kukamata magari barabarani ? Hivi usalama wa watembeao kwa miguu
na hasa watoto, wazee na walemavu unamtegemea nani? Hivi ukiwa na madereva ambao hawaheshimu 'zebra-crossing' na taa za barabarani utasema una polisi wa usalama barabarani au wa hatari barabarani?
Hivi unaweza kuwa na askari 10 au 20 ambao eti kazi yao ni kuandika maelezo ya wanaoletwa vituoni ukasema unawatumia jamaa hao vizuri? Hivi kweli tunashindwa kujipanga kwamba, kazi ya ulinzi iwe barabarani, viwandani au nyumbani ni ya watu wanaolipwa mshahara kufanya kazi hiyo?Wakati unafikiria majibu ya maswali hayo mimi ninapendekeza yafuatayo:
Idadi ya polisi wanaobaki vituoni ipunguzwe kwa kiasi kikubwa kwa kutumia kompyuta na nakala-igizwa [templates) kwa kuwa makosa yote yanayoweza kufanyika hapa nchini yanajulikana na yanaweza kuandaliwa nakala-igizwa hizo na kazi ya wanaokaa nyuma ya kompyuta ni kujaza maelezo kidogo kwa kubadili majina, tarehe, namba au idadi za vitu na sehemu mbalimbali, mahali pa tukio na maelezo binafsi machache ili katika dakika 2 au tatu maelezo ya mtu yawe yamedakwa, kuchapwa na kusainiwa. Hili litaongeza idadi ya askari
watakaokuwa majiani na mitaani kunasa uhalifu na kusaidia watoto, wazee na walemavu na watu wengine wenye matatizo binafsi.SMS na Usalama Barabarani.
Hakika aliyegundua ujumbe mfupi anatufungua macho kwenye mengi ambayo hata bado hatujaanza kuyafikiria. Hebu tuangalie hili la usalama barabarani, rushwa na matumizi ya teknohama.Je, makosa yote yanayoweza kufanywa iwe na gari, dereva, konda au abiria na kadhalika barabarani
yanajulikana? Tunaweza kuyapa haya namba maalumu? Na je, kuna polisi, dereva wa daladala au konda asiyekuwa na simu ya mkononi?Ndugu Mwema unaweza kuongea na Vodacom, Zain, Zantel na Tigo na wale wenye majukwaa ya kuhifadhi, kupokea na kutuma ujumbe ili wakueleze kama inawezekana kwa mambo haya kufanyika:
1. Usalama barabarani kutuma ujumbe makao ya Usalama Barabarani kwa kubonyeza kitufe chake kwenye simu na kujaza maelezo muhimu ambayo yote yako kwa namba kuhusu kosa lililofanywa na daladala fulani ?
2. Makao makuu husika kupokea taarifa hiyo na kuhifadhi kumbukumbu na kisha kumtumia papo kwa hapo dereva wa daladala husika kuwa kafanya kosa
fulani, mahala fulani, saa fulani na kwamba alipe faini kiasi fulani ?
3. Makao Makuu ya Usalama kuwa na 'Caution Money' toka kwa wenye daladala itakayotunzwa nao na kukatwa wakati daladala ya mtu hiyo imetozwa faini?
4. Dereva wa daladala kumuarifu tajiri yake alipe faini hiyo kwa kutumia simu yake ya mkononi.
5. Fedha hiyo kuingia kwenye mfumo wa Daladala-Pesa/Barabara-Pesa wa Usalama Barabarani ambao utatumika kuongeza ubora wa maisha ya watumishi wote
wa Jeshi la Polisi pamoja na wanaofanya vizuri sana pia kutunzwa bonasi na bakshishi nyingine?
Na je, bajeti ya serikali nayo hatima ya yote haitatunishwa na
mfuko unaotokana na kuhakikisha kuwasheria za usalama zinafuatwa na kunakuwepo na utawala wa kisheria nchini? Angalizo: Kama wazo hili linakubalika na
kutekelezwa ikumbukwe kwamba, kila mvunja sheria za barabarani anayeripotiwa sio tu atalipa faini bali atalipia ujumbe uliotumwa kumripoti na ujumbe mwingine
utakaofuatia hadi alipe faini ikiwa ni pamoja na ujumbe wa kumkumbusha kwamba hajalipa faini aliyotozwa.
Aidha, raia ndani ya basi au barabarani wataweza
kumripoti dereva yeyote mzembe ili mradi simu zao ziwe zimesajiliwa na majina yao yanajulikana na wanaweza kutoa ushahidi. 'Lotto' ya Usalama barabarani inaweza kuwazawadia pia watu kama hao.Huu ni mfano mmoja tu, lakini ninaamini Tanzania ya leo ina watu wengi tu wenye akili kama mchwa baadhi yao wakiwemo humo humo ndani ya jeshi la polisi basi mjaribu kuona pia njia nyingine zinazofaa zaidi ya mawazo ninayotoa mimi.Ninachokisema mimi ni kuwa upo
uwezekano wa jeshi la polisi kuwa na watu wachache vituoni na wengi wao wakawa mitaani; na huko mitaani kuna uwezekano mkubwa wa kutumia simu za mikononi kunasa na kuripoti makosa ya barabarani bila askari kulazimika kuandika kitu zaidi ya kubonyeza namba na maelezo ndani ya simu yake; na taarifa hizo kupokelewa makao makuu kupitia watoa huduma za simu za mkononi/wenye majukwaa ya kutuma na kupokea ujumbe na juu ya yote simu hizo hizo za mkononi
kutumiwa na wenye daladala kulipa faini za papo kwa hapo.Hili si wazo jipya, ila muktadha wake ni mpya. Sio wazo litakoeleweka au kukubalika kirahisi na wengi
kwani huenda likawa linachangia moja kwa moja kuondoa vitendo vya madereva, abiria na usalama barabarni vinavyochangia kuwepo kwa rushwa kwa kukata
kabisa mzizi wa fitina.
Nimezoea kutoa mawazo bure na sitarajii kunufaika chochote na mawazo haya kama ambavyo sijawahi kunufaika na wazo langu lolote huko nyuma. Hivyo mtu asije kunishuku kwamba, ninatumiwa na wamiliki wa kampuni za simu za mikononi kuwapatia biashara mpya bali nalitoa hili toka dhati ya moyo
wangu ili kuchangia usalama barabarani na kutokomeza kabisa rushwa vitu ambavyo vinamkera yule, wewe na mimi.
Tuesday, May 24, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment