Tuesday, May 24, 2011

Ili kufufua michezo na ushindani.....

Ili kufufua michezo na ushindani.....

INASEMEKANA zaidi ya nusu ya Watanzania ni vijana wenye umri chini ya miaka 15. Huu ni umri wa kusoma na kucheza. Hali ilivyo si hivyo. Wengi wanaopenda riadha, ngumi, mbio za baiskeli, kuogelea na kadhalika hawapati fursa hiyo. Asilimia kubwa ya watoto na vijana wetu wanakuwa bila kushiriki katika michezo yoyote ya maana na inayoweza kuwaendeleza kimaisha, kiakili, kimwili na kiroho.

Tatizo ni nini ? Labda tuulize Wizara husika. Na tuwaulize kwa staili ya aina yake. Hivi wizara husika na waziri wake wamewaendea Watanzania mijini na vijijini na kuwahamasisha kuwepo kwa viwanja vya michezo kwa ajili ya watoto wao mitaani mwao wakakataa? Au je, wizara ina mradi wowote unaohusiana na kuwanusuru watoto wetu kiafya na kimwili kwa kuwapatia viwanja jirani na waishipo,

ili washiriki katika mchezo wanaoupenda? Je, Wizara husika ina habari na misitu inayojengwa karibu na mji na kisha kutumika kama uwanja huru wa mazoezi kwa wananchi

wote kuanzia watoto hadi wazee. (Mfano mzuri upo Baden, Wurtenburg, Ujerumani). Je, wizara husika imekwishawahi kutuma watu wake kuonana na mastaa wa

michezo mbalimbali kama vile kina Serena Williams, Del Porto, Nadal, Tevez, Ronaldino, Tiger Woods na kadhalika na kuwakaribisha kuja kuona ni nini wanachoweza kuwafanyia vijana wa Kitanzania ?

Je, wizara inashirikiana vipi na balozi za nje, makampuni na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kujenga na kuendeleza miundo mbinu ya michezo na vipaji vya kimichezo vya vijana wa Kitanzania?

Je, kuna wakati wowote wizara husika imekaa na wakuu wa mikoa fulani kama vile Kilimanjaro ambako kilichokuwa kiwe kiwanja cha mpira/michezo sasa kimegeuzwa soko ili wajitahidi kujenga viwanja bora za kimataifa kila mkoa na pale pindi tunapopewa changamoto angalau ya kuwa wenyeji wa Kombe la Mabara tuweze kukubali kazi hiyo bila woga ?

Je, wizara husika imekwisha shirikiana na Wizara ya ndani na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili kuona namnna ambayo maaskari vijana wanaweza kushiriki katika michezo na hatimaye kuliletea taifa sifa na heshima ? Je, kuna mpango na mkakati wa miaka mitano katika kuimarisha mitaa, shule za msingi na sekondari kimichezo?

Na je, elimu walimu wa michezo/makocha (kama wapo) wanayoipata inaenda na wakati. Yaani, kwa maneno mengine mwalimu wa michezo aliyefundishwa hapa Tanzania

anaweza kumuendeleza kijana hadi afanikiwe kuingia kwenye medani ya kimataifa ? Kwanini, mathalani, tunashindwa kuwa na mashindao ya rika la umri wa miaka 12,14, 16, 18, 20 katika soka, basketball, netball na kadhalika? Je, kuna mikakati yoyote ya kuanzishwa na kuendelezwa michezo mbalimbali mitaani na vijijini kama njia ya burudani, lakini pia kuendeleza vipaji vya kimichezo vya vijana sehemu hizo ? Katika ngazi ya vijiji je, kuna mashindano gani ya maana ambayo yatakuwa yakiwahamasisha vijana kuendelea kufanya vizuri ili washiriki katika michezo ngazi ya kata na tarafa na wilaya?

Je, kuna wilaya yoyote yenye kufanya mashindano yoyote ya maana ambayo yanaweza kumfanya mchezaji anayenyanyukia wa Kitanzania kuendelezwa na kufikia kushiriki hadi ngazi ya kimataifa? Kwa kuwa michezo sasa ni mali inafaa pia kuuliza kwamba je, serikali huwa inatoa msaada wa aina yoyote kwa watu wanaojikita katika kuwekeza kwenye

kuendeleza vipaji vya kimichezo vya vijana wa Kitanzania.

Huwa inawasaidia wawekezaji hao katika mambo gani? Na je, serikali, mangimeza wake na wanasiasa, hususani wabunge wanaweza kutoa mchango gani katika kuhakikisha kuwa watu binafsi, makundi ya kijamii na taasisi nyingine zinajitolea ili pawepo na taasisi za mafunzo na utaalamu wa kimichezo? Kuna mkakati gani wa kupata toka nje au kutengeneza papa hapa nyumbani, vifaa vya michezo ambavyo vitakuwa vya bei

nafuu na hivyo wazazi wengi kumudu kuwanunulia watoto wao?

Je, ipo mikakati yoyote ya kuimarisha lishe, tiba, mazoezi na ushauri katika vyakula ili vijana wanaoshiriki michezo waweze kujenga siha na nidhamu itakayosaidia kuwafanya wawe wanamichezo bora ?

Je, kuna mipango yoyote ya kuwa na taasisi inayotoa misaada au mikopo ya kifedha na hivyo kuwawezesha wanamichezo kujiendeleza na kujiimarisha katika michezo wanayoshiriki? Je, mikoa ya kusini inahamasishwaje kuwa na mashindano ya kimataifa inayoshirikisha nchi hii na nchi kama vile Msumbiji, Malawi na Zambia ?

Na mikoa ya magharibi kama vile Tabora, Rukwa, Kigoma na Kagera inahamasishwaje iwe na mashindano ya kimataifa kati yake na nchi jirani za Kongo, Rwanda na Burundi? Kama ilivyo kwa mikoa ya kando ya bahari kuwa na michezo ya kimataifa inayoshirikisha nchi za Madagascar, Ushelisheli, Mauritius na Komoro? Au mikoa ya Kaskazini Mashariki kuwa na michezo kati yake na nchi za Kenya, Sudan, Somalia na Djibouti ? Kuna wanaouliza pia hivi ni jukumu la nani kuhakikisha kuwa kila mkoa unakuwa na stadiumu ya kimataifa ?

Na je, wananchi wa kila mkoa wakihamasishwa na Wachina wakaombwa kuonesha walichokifanya Dar es salaam na watu

wakahakikishiwa kuwa wamiliki wa viwanja hivyo watakuwa ni wao na hisa watapewa na viwanja havitaporwa na chama cha kisiasa hatutakuwa na 'stadiumu' kama hizo? Je, ni jukumu la nani kutafuta na kuajiri makocha wa kufundisha makocha wa michezo mbalimbali wa Kitanzania? Ni nani pia anayeweza

kushughulikia upatikanaji wa mitumba ya vifaa vya michezo kama tulivyochangamkia kuruhusu upatikanaji wa mitumba ya nguo na ile ya magari?

Na hivyo nchi hii na wahandisi wote tuliosomeshana hakuna anayeweza kweli kuwezeshwa kutengeneza baadhi ya vifaa vya michezo nchini na vikapatikana kwa bei rahisi sawa

na bure ? Je, wizara mbona ina kigugumizi katika kuwa na kaulimbiu inayosema: ''MICHEZO HVI LEO NI AJIRA, MZAZI KAMSOMESHE MWANAO MICHEZO PIA ?" na kisha kuwaelimisha wazazi kutong'ang'ania kuwashindilia watoto wao wasio na uwezo masomo wasiyoyaweza na badala yake kuibua vipaji vyao vingine ili wachanue kiulaini? Maswali haya ingawa yanaulizwa kiaiana aina ni dhahiri kwamba, yakijibiwa inavyostahili yatasaidia kutufungua macho Watanzania, hususani katika suala la kufufua michezo na ushindani Tanzania. Michezo si utani wala sio usanii. Ukiwa mtu wa utani utani na msanii sio rahisi kuwahamasisha vijana

wachangamkie michezo kama njia ya kujikwamua na umasikini. Hili lataka mtu kuonyesha kwa vitendo na sio kwa maneno kwamba kweli unataka kuwaendeleza

wenye vipaji vya michezo.

Maana hakuna mtu anayevunjika moyo haraka kama mwana michezo na njia moja ya kumvunja moyo haraka ni ahadi za uongo au maneno matupu yasiyoishia kutafisirika kivitendo. Kwa miaka mingi tumekuwa tukiwasanifu vijana kwamba ni viongozi wa kesho na nchi itajengwa nao, lakini tumekuwa na mikono mifupi katika kuwa nyenzo na zana za kuonesha kweli tuna nia ya kweli kuhakikisha kuwa wanakuwa kile tunachowaimbia kuwa! Naje,


wizara inajua ni michezo mingapi ambayo leo hushindwania katika Olimpiki na ipi ambayo Tanzania ikikamia inaweza kufanikiwa sio tu kushiriki bali kushinda? Na nini kifanyike ili hilo liwezekane? Katika miaka hii ya kupanuka kwa sekta binafsi na kunyauka kwa sekta ya umma ni jukumu la wizara husika kulichukulia pia suala la michezo kwamba ni ajira na linahitaji mipango na mikakati. Tunapozungumzia ajira kwa hiyo tunapaswa pia kuwa na idadi tosha ya watu tunaosema hawa watajiajiri wenyewe kwa kuwa washiriki katika mchezo huu na ule. Sampuli ya wanamichezo wanaoweza kujiajiri sio hawa wanaoishia darasa la saba na wanaojua

tu Kiswahili.

Ni lazima watoto na vijana hawa wawekewe ngazi toka shule ya msingi hadi vyuoni au vilevile toka mtaani hadi vyuoni. Baadhi ya vyuo vyetu vinatakiwa kubadilika na kuanza kuwafuata watu waliko ili kuendesha masomo kama haya ya michezo, lugha na uzamili katika maeneo maalumu ya kitarafu. Kwa kuwa tumeweza kuwa na shule ya sekondari kwa kila kata ninaamini sio kazi pia kuwa na shule ya michezo, lugha, sanaa na muziki katika kila kata. Kwa kufanya hivi

basi itakuwa ni rahisi kwa wale wanaofulia katika masomo ya kawaida kujinoma katika maeneo ya michezo au sanaa wanayoipenda na wanayoamini kuwa inaweza kuwapa ajira mwisho wa yote. Maana swali hapa ni je tunasoma au watu wanasoma kwa ajili ya nini? Ukikubali kwamba tunasoma ili tupate mkate wetu wa kila siku basi utagundua mara moja kwamba tunawatendea isivyo haki wasio na vipaji vya kuwa wanafunzi wazuri wa masomo ya kimapokeo, kwa kutowapa

fursa ya kusomea kile wanachokitaka na kukipenda. Aidha, ni muhimu kwa Watanzania kujiganga na ubinafsi ambao sasa unatangulizwa karibu katika kila jambo kwa kuwasidia wale wote wenye vipaji vya michezo bila kujali kama wanakuhusu au hawakuhusu!

No comments:

Post a Comment