Monday, May 23, 2011

Kufikiria na kupanga kirazini Rasilimali Watu katika ngazi ya KItaifa

Katika insha hii nitajaribu kuonesha mikakati na mbinu za kuunda wizara, uwakala na taasisi nyingine za kiserikali kwa namna ambayo kwamba ufanisi na ufanifu wa shughuli zetu mbalimbali utakuwa ukiongezeka siku hadi siku.

Awali ya yote naomba kusema kwamba Baraza letu la Mawaziri kama yalivyo mabaraza mengi ya mawaziri Afrika ni kubwa kiasi cha kukiuka misingi ya menejimenti na uratibu bora na hakika. Na sio hilo tu wizara nyingi katika miaka hii zinafaa zaidi kuwa wakala au mamlaka au taasisi maalum zinazojiendesha zenyewe kwa kiasi fulani kutokana na kuingiza kipato kila mwaka kutokana na baadhi ya shughuli zitakazotakiwa kulipiwa na watumiaji.

Kwa kusuka upya mfumo wa serikali kwa namna hii Rais wa nchi atakuwa na watu wachache wa kufuatilia kwa karibu ambao pia wanasimamia maeneo nyeti na yenye uwezo wa kuchangia uzalishaji mali na hivyo kuboresha pato la taifa mwaka hadi mwaka. Kutokana na hili inakuwa ni rahisi kuwatathmini wale wanaoshika nyadhifa hizo.

Nina hakika hili litaongeza sio tu unafuu wa kazi bali hata kutoa fursa ya baadhi ya wizara na mawakala kuendesha, kusimamia na kuchangia michezo, sanaa, utamaduni na kadhalika.


Nadharia ya elimu ya Rasilimali Watu inasema mwanzo wa mafanikio ya taasisi yoyote ile ni kuwa na watu wanaofaa katika nafasi husika katika wakati muafaka; watu wenye ujuzi na uzoefu unaostahili katika majukumu yaliyopo; idadi ya watu wasiozidi au kuwa pungufu katika taasisi na sehemu zake; na watu wenye uwezo wa kufanikisha malengo ya taasisi husika kwa kutumia watu na rasilimali nyinginezo zilizopo.

Aidha ni lazima kwa kazi na majukumu yote yaliyopo kuweza kutathiminiwa na kupimwa ili kiwango cha mafanikio kujulikana wakati wote.
Huwezi kumpa Waziri au Kamishna au Mkuu wa Taasisi kazi bila kujua anastahili kufanikisha malengo gani kwa robo mwaka, nusu mwaka, mwaka au miaka mitano.

Nitaonesha pia kuwa Tanzania inaweza kuwa na wizara kama 14 tu na mambo yake yakawa mazuri kuliko ilivyo sasa. Wizara nyingine zote zitabadilika kuwa wakala au taasisi maalum ambazo sio tu zitapunguza gharama ya uendeshaji serikali bali zinaweza kuwa pia zinaiingizia serikali pato la haja.

Mahala pa kuanzia katika kupanga wizara

Serikali iliyo bora haipangi wizara zake kutokana na matakwa ya kisiasa. Aghalabu huwa inaunda wizara kwa kuzingatia azma na malengo mablimbali ya kiuchumi, kijamii na kimkakati.

Modeli ninayoichagua mimi katika kuamua ni shughuli zipi zinahitaji wizara na zipi zinahitaji wakala au taasisi maalum huanza kwa kujaribu kuzigawa wizara zote zilizopo katika wizara zenye uwezo wa kuzalisha mali; wizara zinazotumia fedha lakini haziwezi kabisa kuingiza pato lolote na wizara ambazo pamoja na kuwa ni za gharama zina nafasi ya kuliingizia taifa kipato cha aina fulani kama zitapangwa na kusimamiwa upya.

Baadhi ya wizara katika makundi ya hapo juu zina sifa pia ya kuwa wizara nyeti au za kimkakati kwa sababu za kuhami au kuwa na uhakika wa usalama wa taifa na watu wake wakati wote. Wizara au taasisi kama hizo zisipodhibitiwa kwa ukaribu na uongozi wa nchi zinaweza kuiweka nchi mahala pabaya.

Nilipopitia muundo wa kabineti ya Tanzania hivi karibuni niliona kuna wizara 26 nazo ni kama ifuatavyo: Utumishi wa umma, Utawala bora, Masuala ya Muungano, Mazingira, Utawala wa mikoa na serikali za mitaa, Masuala ya Bunge na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wizara nyingine ni Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha na Uchumi, Viwanda, biashara na masoko, Kilimo, ushirika na usalama wa chakula,Mali Asili na Utalii na Maji na Umwagiliaji Maji.

Aidha kuna Nishati na Madini, Maandeleo ya Miundo Mbinu, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Afya na Ustawi wa Jamii, Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

Kadhalika kuna wizara ya Ardhi, Nyumba na makazi, Habari, Utamaduni na Michezo, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mambo ya Ndani, Sheria na Katiba, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na mifugo na uvuvi.

Nafasi na uwezo wa kuitoa nchi yetu toka kwenye umasikin kwenda kwenye neema na kuwafanya Watanzania wabadilike na kuwa watu wasiokubali kuacha matatizo kuendelea kuwa matatizo mwaka nenda, mwaka rudi unategemea sana jinsi tunavyoainisha na kubainisha ni shughuli zipi zinahitaji wizara na zipi zinahitaji taasisi au uwakala tu.

Kwa kugawa majukumu ya kiserikali kwa namba tuliyoyagawa viongozi wanakuwa na uwezo wa kujua sio tu nini kifanyike lakini muhimu zaidi vigezo na malengo yaliyopo na jinsi ya kutathmini katika vipindi vilivyopangwa.

Ukiziangalia wizara zilizoorodheshwa hapo juu tunaweza kuzigawa kama ifuatavyo:

I. WIZARA ZENYE UWEZO WA KUZALISHA MALI:
. Fedha na masuala ya Uchumi;
. Viwanda, Biashara na Masoko;
. Kilimo, usalama wa chakula na Ushirika;
. Mali Asili na Utalii;
. Maji na Umwagiliani ;
. Nishati na Madini;
. Afya na Ustawi wa Jamii;
. Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.


II. WIZARA GHARAMA
. Utumishi wa umma;
. Utawala bora;
. Masuala ya Muungano;
. Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
. Maendeleo ya Miundombinu;
. Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia;
. Habari, Utamaduni na Michezo;
. Mambo ya Ndani;
. Sheria na Katiba;
. Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto;


III. WIZARA GHARAMA LAKINI ZENYE UWEZO WA KUINGIZA:
. Serikali za Mikoa na Utawala wa mitaa;
. Mazingira;
. Masuala ya Bunge;
. Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
. Kazi, Ajira na Vijana;
. Ardhi, nyumba na makazi;
. Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Tuchukulie kwamba mchanganuo wa Rasilimali Watu na Kazi uliofanyika ni dhaifu na hivyo shughuli kadhaa zisizoiva au kuendana pamoja zimelundikwa pamoja basi tunasahihisha mambo kwa kuwa na mpangilio safi zaidi kama huu hapa chini:

I. SHUGHULI ZINAZOSTAHILI KUWA NA WIZARA

A. Wizara zinazochangia uzalishaji mali:

. Wizara ya Fedha;
. Wizara ya Viwanda na Mchakato wa Madini;
. Wizara ya Kilimo na Viwanda vya Kilimo ;
. Wizara ya Ardhi ,Matumizi na usalama wa Mali Asili na chakula;
. Wizara ya Utalii na Huduma za Kibiashara;
. Wizara ya Umeme kwa Taifa na Matumizi ya Nishati mbadala;
. Wizara ya Afya na Huduma za Tiba za Kimataifa;
. Wizara ya Elimu na Kujifunza Daima;
. Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia;

B. Wizara Gharama au Nyeti na za Kimkakati::

. Wizara ya Mambo ya Ndani;
. Wizara ya Sheria na Haki za Binadamu;
. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa;
. Wizara ya Menejimenti ya Rasilmali Watu na Ujengaji Uwezo;
. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

II. WAKALA NA BODI MBALIMBALI

Kama tulivyoona kabla baadhi ya wizara au sehemu za Wizara zinaweza kubadilishwa kuwa wakala au bodi au kamisheni ambazo zinaweza kujiendesha kwa kiasi fulani kutokana na uwezo wao wenyewe wa kuingiza kipato fulani.

Wakala wa Utumishi wa Umma. Huu ni wakala unaoweza kujiendesha kwa kutoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa umma na wengineo. Wakala unaweza kujiingiza pia katika utafiti na ushauri.
. Bodi ya Ukaguzi wa Utawala Bora. Bodi hii pamoja na shughuli zake za ukaguzi inaweza kuwa na shughuli kama hizo hapo juu.
. Kamisheni ya Masuala ya Muungano. Kamisheni hii inaweza kufanya utafiti na ushauri kuhusu mbinu za kuongeza ubora wa Muungano na ushiriki wa Tanzania katika maeneo mengine ya kiuchumi.
. Wakala wa Uendeshaji MIkoa Kiuchumi. Hii inaweza kufanya kazi kama vile Vituo vya Uwekezaji katika ngazi ya Mkoa.
. Wakala wa Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini. Taasisi hii inaweza kufanya kazi za mafunzo, utafiti na ushauri kwa sehemu husika ;

Wakala, Kamisheni au Bodi au Mamlaka za wa Hifadhi na Maendeleo ya Mazingira; Bunge na wabunge;Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Maendeleo ya Lugha na utamaduni; Masoko ya Ndani na Biashara ya Nje; Matumizi na Hifadhi ya Maji, Mito , Maziwa na Habari; Mafunzo ya Ufundi, Ujuzi, Stadi na Maarifa Mapya; Mipango ya Uchumi na Ufanikishaji Ujasiriamali; Kilimo cha Umwagiliaji na Uvunaji Maji ya Mvua; Maendeleo ya Makazi ya Watu na Ujenzi wa Nyumba; Kuwajali Wasiojiweza, Watoto, Wazee na Wanawake;Masuala ya Kikatiba; Maendeleo ya Vijana na Vipaji; Maendeleo ya Mifugo na Bidhaa za Mifugo; Maendeleo ya Uvuvi na Rasilimali Bahari; Maendeleo ya Miundombinu; Utafiti na Maendeleo ( ikiwemo Sayansi na Teknolojia); na Maendeleo ya Taasisi ndogo za Kifedha na Ushirika.

Wizara na Taasisi hizi zimepangwa upya hivi kwa ajili ya kuongeza ufanisi na ufanifu wa serikali na hususan katika matumizi ya Rasilimali Watu adimu.

Kundi la wizara zinazoweza kuchangia uzalishaji mali linajumuisha wizara zote ambazo zinaweza kusaidia sekta binafsi au mashirika ya umma au ushirika mbalimbali au ubia wa watu au taasisi hizo ili kuzalisha mali au kutoa huduma fulani inayohitajika katika jamii yetu.

Kundi la Pili linajumuisha taasisi, bodi, mamlaka, kamisheni au wakala ambao, aghalabu, huchukuliwa kama watoa huduma kwa wizara au taasisi nyinginezo katika nchi. Huduma hizo hujumlisha pamoja na kuweka mazingira mazuri yanayosaidia uzalishaji mali au utoaji huduma bora.

Mawakala kwa kawaida watakuwa ni taasisi zenye dhima na heshima sawa na wizara. Wengi kati wa mawakala watakuwa wakitoa huduma kwa watu binafsi, mashirika, wilaya, mikoa na taifa kwa namna ambayo kwayo mawakala watakuwa wanaingiza kipato chenye kuwawezesha kuendesha shughuli zao bila kuitegemea sana serikali baada ya miaka michache ya kuanza shughuli zao.
Hata hivyo sifa yao kuu itakuwa ni kuwa wakala hawatakuwa na urasimu na umangimeza kama ule wa wizara. Hili linatokana na ukweli kuwa kila wakala anakuwa na malengo anayopaswa kuyafikia katika kila kipindi kilichopangwa.

No comments:

Post a Comment