Saturday, May 14, 2011

Maendeleo huja kwa Kuchochea migogoro chanya

MIGOGORO kwa kiasi kikubwa husaidia kila upande kuweka wazi bila unafiki mahitaji na maslahi yake mbele. Wananchi wanapofanya kazi kwa ushirikiano au ushindani migogoro hujidhihirisha kwa baadhi yao kukata tamaa, kejeli, jazba, mazungumzo, majadiliano na mabishano. Hususan, katika ushindani ambamo watu huwa na malengo tofauti au wanakuwa na misheni zilizofanana, ambamo ni mmoja tu kati yao anayeweza kuibuka na ushindi.

Uweledi, uzoefu, ustadi na ujuzi wa kugeuza migogoro kuwa kitu chanya ndipo hapo inapohitajika. Hatima ya yote hapa ni kuwa na lengo moja na kuongeza faida au manufaa kwa pande zote husika.

Migogoro chanya ni njia pekee inayomaliza kiini cha matatizo mengi. Kwa tulio wengi tunakubali matatizo na kuyaacha matatizo kuwa matatizo hadi wale yanayowasumbua wanakufa. Na jumla ya matatizo ya wananchi na hasira yao, ndiyo yanayogeuka migogoro mikubwa baadaye.

Migogoro huwa na faida pale viongozi wanapokuwa wakweli, safi, wachapakazi, bora na waliodhamiria kuleta mabdailiko ya kimsingi katika jamii husika.

Kinyume chake udikteta katika kuwatawala watu na ubwanaukubwa wowote ule uwe wa mtu au wa kikundi fulani huzusha utitiri wa migogoro hasi.

Kuanzisha na kuchochea migogoro chanya kubadili hali ovyo, duni na mbaya waliyonayo wananchi na kutafuta hali ya neema kwa kasi na ari zaidi na bora kuliko waliyonayo.

Fursa za kimaendeleo kwa wananchi zinakuwa ni mambo pacha na matatizo yao ya kila siku na sio tena kitu cha siri bali ni mazungumzo na matukio ya kila siku. Maana usiri ni chanzo kikubwa sana cha migogoro katika jamii husika.

Tulionesha pia kwamba watu au jamii isiyo na migogoro hunyauka na kufa kimaendeleo kama jamii.

Hali hii inaonekana katika baadhi ya vijiji na mikoa nchini ambayo inabaki sana nyuma kimaendeleo ikifananishwa na mingine.

Migogoro kila siku isiyodhibitiwa huwa uwanja wa vita visivyokwisha kama hali ilivyo Somalia leo.

Ni dhahiri basi upo umuhimu wa kuchochea migogoro chanya katika jamii ili kuwazindua wale walioko usingizini na kutumia kuwa macho kwao kuumua mabadiliko na maendeleo endelevu katika jamii husika.

Nitajaribu kutumia mifano kadhaa ili kulithibitisha hili. Kwanza, tuanze na bunge letu tukufu. Bunge hilo lilipokuwa na wabunge wengi kutoka chama tawala halikuwa limechangamka kama lilivyochangamka leo. Baadhi ya wabunge walikuwa wakilala badala ya kutoa michango inayowasilisha dhiki na uhitaji wa wale wanaowawakilisha. Swali ni je, gogoro la kibunge ni chanya au hasi. Uchanya wake utatokana na pande zote mbili kujua tabia na mwenendo stahilifu ambao wabunge wanatakiwa kuufuata ili nchi ipate maendeleo kwa kutanguliza mbele Utanzania badala ya uchama, ukubwa na umimi.

Migogoro itakuwa hasi kama wabunge watalifanya bunge ni mahala pa kukashidiana, kudhihakiana, kudharauliana badala ya kuheshimu michango ya watu na nguvu ya hoja badala ya nguvu za kisiasa na kimamlaka.

Mfano wa pili ni wa vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi. Hii ni migogoro ya muda mrefu ambayo inafikia hata wakati mwingine tunaisahau na kuiona ni sehemu yetu ya maisha.

Mfano mwingine ni wa katiba mpya. Huu ni mgogoro kwa sababu kuna wale walioko madarakani leo ambao katiba ya zamani imewafaa, itawafaa na inaelekea itaendelea kuwabakisha madarakani kwa muda fulani lakini sio milele na wale ambao wanaoona katiba iliyopo inawanyima mengi wanayostahili na wakati umefika wa kuibadili ile ya zamani.

Upande mmoja kuna serikali na chama tawala (sio wote) na kwa upande mwingine kuna wapinzani na Watanzania wasio na chama (sio wote) na kazi iliyoko mbele yake ni kugeuza mgogoro huu wa katiba uwe mgogoro chanya kwa faida ya Watanzania wa leo na wa kesho. Na kazi ya kuandika katiba mpya bila shaka itakuwa rahisi kama wote tutaelewa na kulikubali hili.

Mgogoro yenye manufaa itaifanya serikali na chama tawala kwa upande mmoja na wapinzani na wananchi wengine kwa upande mwingine, waweze wote kwa pamoja kuibuka washindi katika ujenzi wa nchi.

Ipo tofauti kubwa sana kati ya maisha vijijini na maisha ya mjini. Kuna wanaothubutu kusema kwamba maisha vijijini yangelikuwa bora kwa robo tu ya yale ya mjini basi wasingeliishi mijini. Ipo haja basi ya kuchochea maendeleo ya vijijini angalau vijiji vifanane fanane na mijini na hivyo tukawa tunatenda haki kwa wote. Sio kosa kwa mtu yeyote yule kwenda vijijini na kuwaambia hamna maji, umeme, barabara, hospitali safi, shule bora kwa sababu viongozi wameshindwa kazi yao. Mgogoro chanya ndio njia pekee ya kupunguza tofauti kati ya vijiji na miji.

Mgogoro mwingine ni ule wa upatikanaji huduma na mahitaji ya msingi kwa wananchi. Hili kwa mujibu wa Machiavelli ni jukumu la kwanza la uongozi wowote ule. Maana wananchi wengi wakipata chakula cha kutosha, wakalala mahala pazuri na wakawa huru kuzifuata ndoto zao huwa hawana habari na siasa na utawala.

Bila maji, umeme, barabara, madaraja, shule na hospitali nafuu na taratibu za kunusuru masikini kwa huduma twaibu na upatikanaji mahitaji yote ya msingi, migogoro itakuwa hasi zaidi kuliko chanya. Na ukweli huu budi ujulikane na kila mtu.

Katika mikoa kuna maeneo ambayo ina vyuo au vyuo vikuu viwili hadi kumi wakati kuna mikoa haina hata chuo kikuu kimoja. Katika hali kama hii bila shaka kwenye katiba iliyopo, ibara ya 9 kifungu (d) kinachosema: "kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja," hakijazingatiwa. Na hili ni swali la nini huzuka kwanza, yai au kuku ? Ndivyo ilivyo pia kwa viwanda na miradi mingine mikubwa-hakuna usawa kinchi!

Hakuna asiyejua kilichotokea huko Yugolsavia hata tukisema Mungu aepushilie mbali! Maana kinachoonekana sasa ni kuwa ni pale tu mkoa unapokuwa na Waziri mkuu au Waziri wa elimu utakapoweza nao kupata chuo achilia mbali Chuo Kikuu. Kwa maoni yangu, badala ya kujenga vyuo vikuu vikubwa tunavyoshindwa kuvitawala na kuviendesha vyema ni bora kila mkoa kwa sababu za haki na usawa kila mkoa uwe na Chuo Kikuu chake ili kuchochea maendeleo ya elimu ya juu, utafiti na uchumi kwa jamii husika.

Watanzania wote walichangia kwa kodi yao uanzishaji wa makampuni ya umma. Yalipotaifishwa hakuna Mtanzania wa kawaida aliyenufaika kitu moja kwa moja. Hiki ni chanzo kizuri cha mgogoro kama tutauliza kama tuliweza kuanzisha makampuni yaliyomilikiwa na serikali kwanini tunashindwa kuanzisha makampuni yatakayomilikiwa na wananchi au wanajamii wenyewe moja kwa moja ?

Pengine mikoa inazorota kimichezo na kisanaa kutokana na serikali na chama tawala kuhodhi baadhi ya viwanja vya michezo. Je, upo mgogoro chanya utarudisha viwanja hivyo mikononi mwa wananchi na kuchochea bora zaidi kujengwa ?

Katika kila eneo la maisha, imani/dini, kazi, elimu, uwekezaji, kujiajiri, huduma, biashara na kadhalika kuna tofauti na kasoro nyingi tu. Hii ni migogoro. Kazi yetu sio kuifukia chini bali kuiweka wazi na kuishughulikia iwe migogoro chanya kwa faida ya nchi na watu wetu!

Kwanini Barricks wapewe migodi mingi hali hawajali maisha ya Watananzia wanaoteketea huko Mara, Bulyahunlu na kwingineko?
Na kwanini kodi zao ziwe chini kiasi cha kuishtua IMF? Huu si mgogoro? Na kwanini hatukuwapa Wachina au Wakorea au Warussi au Wajapani baadhi ya migodi ili
tunufaike zaidi.

Madrasa za kiislamu, shule, vyuo,vyuo vikuu, hospitali na taasisi zingine kama vinaendeshwa ovyoovyo na kimasikini, je ni vibaya kuuondoa siasa na ukiritimba uliopo katika dini hiyo ili kuleta migogoro chanya na hatimaye taasisi hizo ziendeshwe vyema kwa faida ya wote ?

Migogoro chanya hufanya kazi yake vizuri kama watu wanaheshimiwa, wanaelimishwa, wanafunguliwa macho na wahamasisha kuikataa hali mbaya iliyo na kudai hali nzuri ambayo wanaelezewa au kuiona katika picha au sinema.Wachochezi wakifanya kazi yao vizuri wanaweza kubainisha mabilioni ya kodi yanayokusanywa kila mwezi kuwa yanaweza kabisa kufanya kazi hiyo na nyinginezo nyingi na kurahisisha kuharakisha mapambano yetu ya kutafuta maendeleo.

Uongozi safi na bora hauwezi kupatikana hadi pale wananchi watakapoamka na kutambua kuwa wao ndioi 'matajiri' na mabwana au wamiliki wa katiba, mamlaka na madaraka yote ya nchi hii na viongozi ni vibarua wao. Wana uwezo wa kuwapa kazi na kuwafuta kazi pindi watakapotaka kufanya hivyo. Umma ukishirikiana na wanasiasa wakweli, watendaji waadilifu na vyombo vya habari visivyotumiwa kwa maslahi ya watu binafsi kufuatilia kazi na nyendo zote za watumishi wao ili nchi ipate kitu chenye thamani sawa na kile inachowalipa wale walioko madarkani.

http://www.blogger.com

No comments:

Post a Comment