WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Nairobi hivi karibuni walifanikiwa kutengeneza kifaa cha kuchaji simu za mkononi kwa kutumia dainamo ya baiskeli.
Chaja hiyo sasa imeanza kutumika na hasa na watu wa vijijini au wale wanaoishi kwenye mitaa isiyo na umeme.
Utafiti ni shughuli yoyote inayofanyika katika misingi na kanuni zinazokubalika kutafuta matatizo na kisha kupendekeza mikakati ya ufumbuzi na hatimaye kuchangia katika kutatua na kuliondosha tatizo hilo.
Taifa lolote linaweza kugawanywa katika sekta au maeneo makuu manne—jamii, uchumi, siasa, teknolojia na utamaduni. Ni muhali kukuta hakuna matatizo katika sekta zote hizi. Matatizo yapo na yataendelea kuwepo. Tofauti kati ya nchi zinazokwenda mbele na zile zinazosimama hapohapo zilipo kama sio kurudi nyuma ni kwamba zile za kwanza huchangamkia aghalabu utafiti kama njia ya kuendelea kupunguza matatizo yaliyopo katika sekta hizo. Wale wasioendelea siku zote utakuta hawagharamii utafiti wa aina yoyote wa maana na kama upo unaogharamiwa basi ni kwa kiasi kidogo sana.
Kutogharamia utafiti kwa hiyo ni sawa sawa na kutoruhusu kutumika kwa bongo za watu katika ufumbuzi wa matatizo yao na utumiaji fursa zilizopo ili watu wajipatie maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.
Ufumbuzi wa matatizo ya aina yoyote ni kielelezo kikuu cha tofauti kati ya watu wanaokaa mkao wa kimaendeleo na wale wanaokaa mkao wa kihasarahasara. Mtu anayetafuta maendeleo anajua kwamba kutotua tatizo lililopo ni sawa sawa na kubaki hapo hapo alipo kama sio kuporomoka kimaendeleo kwa kiasi fulani.
Kuhamasisha utafiti katika jamii ni njia mojawapo inayofanya kazi kubwa ya kupiga vita tabia ya watu kulea na kuendekeza matatizo.
Wakati mwingine watu hudhani kwamba utafiti lazima uwe ni kitu cha gharama kubwa siku zote. Hii ni dhana potofu. Vijana wale wa Chuo Kikuu cha Nairobi wameweza kufanya walichokifanya kwa kuokota takataka jalalani. Takataka za baiskeli, redio, televisheni, simu za mkononi na vitu kama hivyo. Lakini mwishowe wameishia kutengeneza kitu kilichotokana na takataka kuwa kifaa cha thamani na kinachouzika. Kweli upo utafiti wenye kuhitaji gharama lakini sio tafiti zote zinazohitaji gharama kubwa zaidi ya kwamba kuna majengo mahala, umeme, vifaa vya msingi vya kiutafiti na uwezeshwaji kimshahara kwa wale wanaohusika.
Ninashauri turejeshe tabia na kazi za utafiti kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu kwa njia zozote zile tutakazoweza kufanikisha hili.
Katika ngazi za shule ya msingi tungeanzia na yale wanafunzi wanayoyajua na kisha kuwapa fursa ya kujifunza wasiyoyajua kwa njia mbalimbali ikiwemo kusafiri na kutembelea maeneo nje ya shule, kuona video na sinema za maarifa na kielimu shuleni, kufikishiwa tovuti mashuleni na kutembelewa na wageni wenye ujuzi au ubingwa katika fani mbalimbali watakaozungumza nao.
Kwa namna hii wanafunzi wa shule za msingi Tanzania wasiojua majina ya ndege, miti, wanyama pori, wadudu, samaki na kadhalika watanusurika na ujinga huu tuliondelea kuulea kwa muda mrefu shuleni na mitaani.
Wanafunzi wa shule za sekondari wanaweza kufanya makubwa zaidi kwa kuhakikisha kila sekondari ina maabara za sayansi, ufundi, teknolojia/teknohama na nyinginezo.
Katika vyuo vikuu ni lazima tuoanishe elimu na kile elimu inachotakiwa kukifanya hapo baadaye. Hatuwezi kuendelea na hatuna uwezo huo, katika karne hii wa kuwa na wanafunzi wanaobebwa katika kila jambo. Kwa asilimia kubwa ya watoto wetu (isipokuwa kwa wachache wenye baba vigogo au vizito) elimu na kazi sio jambo linaloweza kuendelea kuepukika tena.
Njia ya kulirahisisha hili ili isiwe mzigo mkubwa kwao ni kwa sisi wenyewe kuoanisha elimu na kazi. Kwa maneno ya baba taifa iwe kwamba : "Elimu ni Kazi, na Kazi ni Elimu!" Kwa maneno mengine lazima elimu yetu iwe na mwelekeo wa uzalishaji mali au utoaji huduma.
Pakuanzia ninaamini ni kwa wizara husika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajumuishwa katika tafiti zitakazochunguza ni aina gani ya elimu inayohitajika ili ije iwe ya manufaa kesho kwa mwanafunzi wa Kitanzania wa shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu.
Pamoja na mashule utafiti unaweza kufanyika pia katika
sekta yenyewe, kama vile watoaji huduma za simu, mabenki, wachimba madini na mafuta, viwanda, biashara na kwingineko. Aidha kila kampuni au taasisi inaweza kuwa na ajenda yake ya utafiti na kuishughulikia kwa kipindi fulani ili kufanikisha malengo yake ya kutatua matatizo iliyokwishabainisha.
Utafiti ni uwekezaji. Ni uwekezaji leo ili kesho tuweze kupata na kutumia zaidi. Kama tusipowekeza katika utafiti basi hili lina maana kwamba huko tunakokwenda tutakuwa na kitu pungufu kuliko hiki tulichonacho sasa.
Kuna tafiti ambazo wakifanya watu wengine itakuwa ni uzushi na stahili yake ni tafiti hizo kufanyika na mwananchi au mkazi au mwenyeji mwenyewe—anayevaa kiatu kinachobana ndiye anayejua ni wapi kiatu kinafinya.
Mifano ya kazi za utafiti zinazohitaji kupewa kipaumbele ukiachilia zile za umaskini, kiuchumi na kisiasa ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa na wenyewe pia kuna umuhimu wa kuwa na tafiti ambazo zitachangia kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na jamii na uchumi bora zaidi katika maeneo yafuatayo:
Katika kilimo na umwagiliaji ipo kazi kubwa sio tu ya kupata maji na ya kuyaleta katika mashamba bali pia kumfanya Mtanzania akubali aina hii ya kilimo na kuamini kwamba anaweza kuneemeka kwa kilimo cha umwagiliaji maji. Na ndivyo ilivyo pia kwa kilimo cha kawaida, yaani, kile cha mvua, ufugaji, uvuvi, ufugaji nyuki na kilimo cha matunda na mazao ya vibandani. Ni lazima tafiti zifanyike hapa ili kumfanya Mtanzania aamini kwamba KILIMO kinaweza kumnusuru.
Ni asilimia ndogo tu ya watu wetu wanapata umeme na kama kweli tunataka Tanzania nzima iwe na umeme hili haliwezi kufanikiwa bila utafiti unaoendelea siku zote ukijaribu kupata njia mbalimbali ambazo kwazo uzalishaji na usambazaji uememe unaweza kufanyika. Ndivyo ilivyo kwa nishati mbadala pia. Na katika eneo hili tayari kuna watu wamekwishajitokeza na kinachokosekana hapa pengine ni utashi wa kisiasa na kuondolewa kwa ukiritimba usiohitajika.
Watanzania wana dhiki kubwa ya nyumba na majengo mijini na vijijini. Ni muhimu kwa hiyo kuwa na tafiti za ujenzi wa nyumba, barabara, reli na miundo mbinu kwa ujumla ili kuhakikisha kwamba sio tu tatizo hilo linakwisha bali wananchi wetu wasio na ajira wanapata ajira za uhakika na kiwango cha maisha cha Watanzania kuwa juu.
Mara kwa mara viwanda au mashine hapa nchini huwa zinasimama kwa kukosa vifaa au spea au vipuli. Je, wakati haujafika wa sisi kuwa na tafiti zinazochangia kuzalisha spea au vipuli vya aina mbalimbali za mashine, mitambo na motokaa kwa asilimia kadhaa ya vile vyote vinavyounda chombo hicho kwa mwaka na hatimaye chombo kizima kiwe kinatengenezwa papa hapa nchini?
Hili linahusu pia vifaa vya sayansi, elimu na Teknohama.
Hivi leo, kuna watoto na vijana wa Kitanzania wanaofanya na wanaoweze kufanya utafiti bila kufundishwa na mtu na wakachangia makubwa kwa nchi hii na kinachokosekana ni wito wa kisiasa tu wa kuwaunga mkono na kuwawezesha kufanikisha yale wanayoyafanya.
Kinachotokea sasa huko China ni kwamba kijana akiangalia redio, televisheni, mashine, diski mama, CD, DVD, Flush au kifaa kingine kutoka nje na akakichambua na kuona kwamba anaweza kuunda chake mwenyewe basi hakatishwi tamaa na kutishiwa na usalama wa taifa bali anapewa fursa na msaada wa hali na mali kufanikisha azma yake.
Ninaamini kwa hapa nchini, tunachotakiwa kufanya ni kwa chombo kama Costech kujishusha chini zaidi na kuwafikia mafundi Tabata, Gerezani, Mwenge, Kimara na kadhalika kwa kuwa na masomo ya kujiendelza kwa Kiswahili ili kukuza uwezo wao wa kutengeneza na kuuza vifaa sio tu hapa nchini bali hata nchi za nje.
Aidha wakati tumefika wa kuangalia wanafunzi wanaokwenda kusoma nje wanaenda huko na watarudi na kitu gani kuchangia manendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi. Kwa hili nina maana tuwe kama wenzetu wa nchi chipukizi kimaendeleo kwa kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaokwenda kusoma nje wanakwenda kusoma na pia kufanya utafiti utakaowawezesha baadaye kurudi nyumbani na akili ya kufanya jambo fulani ambalo pia likifanikiwa litawawezesha kujiajiri wenyewe na kuajiri watu wengine.
Saturday, May 7, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment