Monday, May 23, 2011

Benki taasisi iliyopitwa na wakati?

' Ninaitunuku makala hii kwa Leah Bourne rafiki katika mtandao na ambaye insha yake ya mwaka 1998 iliwaonya Wamarekani lakini hakuna aliyemjali wala

kuzingatia aliyoyaandika wakati huo.'


WAAFRIKA tumezoea siku zote kusubiri majibu ya matatizo yetu wenyewe na ya kwingineko duniani kutoka kwa Wazungu. Kwa mara ya kwanza ningependa niwe

tofauti na Waafrika wenzangu kwa kuthubutu kuchangia japo kwa ufinyu wa fikira na uzoefu wangu ninachoamini ndio njia sahihi ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo

ya uchumi duniani leo.

Nitawashangaza wengi kwa kudai kwamba namna ambayo viongozi wa Marekani na Ulaya wanavyoshughulikia tatizo la mtikisiko wa kiuchumi duniani

kulikosababishwa na kuparaganyika kwa masoko ya fedha yumkini sio njia sahihi.

Kwanza, wanalishughulikia tatizo hili kwa kujijali wao wenyewe kwanza na kusahau kwamba tuko katika enzi za utandawazi. Na hata sisi tusio na uwezo ni sehemu

ya ufumbuzi wa tatizo lililopo. Na bila sisi kushirikishwa kwa ukamilifu na kwa uhakika mambo pengine yanaweza yakawa mabaya zaidi.

Kwa sababu za nafasi katika makala haya nitaongelea tu juu ya mfumo wa benki, mathalani, katika nchi yetu na fursa za kipekee zilizoletwa na Teknolojia ya habari

na mawasiliano (Teknohama) bila wengi wetu kujua kuwa benki zinastahili kuwa teknohama na yenyewe inastahili kuwa benki.

Kwa maoni yangu Rais Barak Obama wa Marekani, Waziri Mkuu Gordon Brown wa Uingereza na wenzao wanaelekea kushughulika zaidi na athari badala ya

chanzo cha tatizo.

Ninachokiona mimi ni kuwa Obama, Brown na wenzake wanampa mgonjwa wa malaria kali panadol ya kutuliza maumivu kwa muda. Hatima ya yote mgonjwa

atapaswa kuwekewa dripu ya kwinini.

Baada ya kusoma na kutafakari kwa mapana na marefu, ninadiriki kuyakinisha kwamba pengo la elimu ya teknohama kati ya viongozi wakuu wa makampuni na

wataalamu wa teknohama lilisababisha kufanya watalaamu mengi—wakuu wa makampuni husika hawakuyafahamu na kama walikuwa wakihisi lolote hawakuwa

na namna ya kuyakinisha.

Nimesema kwamba viongozi wa nchi za Magharibi na wengineo wanashughulikia zaidi matokeo ya tatizo la uchumi duniani na sio chanzo cha tatizo hilo.

Tatizo ni nini?

Tatizo ni serikali na udhibiti wa masuala ya kifedha. Wengi tunaofanya kazi katika makampuni mbalimbali tunajua kuwa siku zote idara ya fedha husimamiwa moja

kwa moja na bosi mkuu na wasaidizi wake.

Katika miaka hii ya kupanuka kwa soko huru na ushindani inastaajabisha kuona kuwa viongozi wa nchi mbalimbali wanediriki kuongoza nchi zao bila kuwa na

habari na kile kinachotokea katika hazina yao. Ni viongozi wachache sana wanaojua kwa uhakika kila shilingi inayoingia na kutoka nchini kwao.
Achilia mbali kama imetumika sawa au vibaya. Kazi hii waliwaachia watu wengine. Kilichotokea ni kuwa hao watu wengine waliiona hiyo ni fursa ya kipekee kwao

kukata pande la keki ya taifa na kuishi maisha mazuri na kujilimbikizia fedha za makaratasi na sarafu lukuki bila kujali hatima ya watu na nchi yao.

Ni dhihaka, ni kichekesho kuwa na serikali duniani ambazo viongozi wake wakuu wanawakabidhi wanasiasa laghai, wafanyabiashara wezi, marafiki zao wenye

njaa kali, na watu wasio na taaluma yoyote ya mambo ya fedha, kazi ya kusimamia hazina za taifa.

Kilichotokea kimetokea. Fundisho ni kuwa haiyumkini mtu kuweza kuongoza nchi bila kujua kwa uhakika kila senti inayoingia na kutoka nchini mwake.
Waulize mameneja wa makampuni yanayodhibiti mambo vilivyo. Fedha bwana ndiyo damu ya taasisi. Anayeichezea hiyo sio rafiki ni adui, mmalize au muondoe

mara moja. Ndivyo ilivyo kwa mawaziri na wizara zao, wakuu wa majimbo au magavana na majimbo yao, wakuu wa mabenki na benki zao na kadhalika.

Nirudie kwa mara nyingine uchumi wa dunia na masoko ya fedha haviwezi kujisimamia wala kujilinda vyenyewe. Viongozi na serikali zao duniani lazima wabadilike

na kukubali kuwa jukumu la kuangalia na kusimamia fedha ni lao pia, angalau kupitia watu wanaosimamia mitandao ambayo hatimaye inaishia katika ikulu zao.

Inawalazimu rais au waziri mkuu wa nchi angalau kwa mwezi kama sio wiki kujua ni nini kinachoendelea. Kama hamna ubabaishaji, wizi na rushwa za kuficha hili

halina sababu ya kuogopwa. Ni ubadhirifu, dhuluma, wizi, rushwa na ubabaishaji wa viongozi na serikali zao duniani ndio unaosababisha tusiwe na uwajibikaji,

uwazi na ufuatiliaji wa mambo ya kifedha duniani. Nani anabisha?


Benki kama zilivyo hazihitajiki

Ninathubutu pia kudai kuwa benki na hususan kwa ukubwa wa majengo na idadi ya wafanyakazi wanaoajiriwa sio mfumo unaoendana na wakati tulio nao. Benki

za namna hii zimepitwa na wakati.

Majengo mengi ya benki hapa nchini na nchi za nje yanaweza kutumika kwa shughuli nyingine za maana zaidi na watumishi wengi wa mabenki wanaweza

wakawa kichocheo cha uzalishaji mali kwingineko badala ya ukarani kwenye mabenki. Kwa maneno mengine, benki kama zilivyo leo ni kitambi kwa nchi, kitambi

kisichohitajika na kinachochangia kumlemaza au kulifanya taifa liende kimdwebedo kiasi cha mtu aliyenacho kujichukia yeye mwenyewe.

Benki zimebakia kuwa mahala pa wamilikaji na wale wanaoajiriwa nazo kujivuna na kujionesha kana kwamba ni akili na uwezo wao ndio uliotumika kuwapa nafasi

za kifedha na kiuchumi walizonazo. Hili si kweli. Mfumo wa benki kama ninavyoujua na kama wewe unavyoujua umekaa kwa namna ambayo jamaa hawa

wanakusanya fedha kutoka kwa wengi na kuzikopesha kwa wachache kwa faida kubwa.

Gharama nyingi na kwa mantiki hiyo rasilimali muhimu za taifa zinaishia kwenye majengo, mishahara na gharama nyingine za uendeshaji ambazo kwa hivi leo

kuporomoka kwa uchumi wa dunia kunadhihirisha hazihitajiki na hazistahili kukubalika.

Maendeleo ya Teknohama

Jambo ambalo kina Obama na Brown bado hawajaangalia kwa umakini wake wote ni KINA, UREFU NA UPANA WA MAPINDUZI YA TEKNOHAMA yanayoendelea

duniani kila kukichwa.

Mapinduzi yoyote makubwa yanapotokea wale waliokuwepo huwa vipofu na wamefungwa fungwa na mazoea na desturi kiasi cha kutojua au kuamini kuwa kile

kinachotokea kweli kinatokea na kitatokea.

Mapinduzi ya TEKNOHAMA yanaandikwa kwenye ukuta kwamba: "Benki kama zilivyo leo zimepitwa na wakati na kuwa ni sawa na ile mijusi mikubwa 'dinosaurs'

na haina tena nafasi katika karne ya 22 hapa duniani." Katika kuonesha haki, kwa hakika, benki zimeikubali na kuitumia TEKNOHAMA kwa kiasi fulani. Lakini kiasi

hiki ni kama asilimia 20 tu ya kile kinachostahili kufanyika.

Baya zaidi ni kuwa kuna baadhi ya benki kuu ambazo bado hazijakubali kuwa Teknohama ni rasilimali muhimu wanayostahili kuwa nayo, kuitumia kikamilifu na

kuienzi na kwamba asilimia kubwa ya watu wao wanastahili kuwa wale wanaojua Teknohama na Taaluma ya Fedha kwa pamoja. Hili lazima libadilike kama

tunataka kuwa na uchumi imara duniani.

Kuna wanaoamini kuwa benki zinastahili kufunga fungate na Teknohama na sio tu kuitumia. Au kwa maneno mengine benki lazima iwe Teknohama, na

Teknohama lazima iwe benki. Kuna ukweli kiasi fulani lakini ninaamini kuwa Teknohama ni kubwa kuliko benki zote zikiwekwa pamoja.

Teknohama imeacha benki nyuma
Hatari iliyopo na ambayo bado inastahili kutathminiwa kwa mapana na marefu zaidi ni kwamba haiwezekani kuwa na wakuu wa mabenki ambao wanawategemea

watu wa Teknohama kuelewa kile kinachoendelea katika biashara zao.

Katika hali kama hii chochote kile kinaweza kikatokea bila mkuu wa benki kujua ni nini kinachoendelea. Wenzetu Ulaya wana afadhali kidogo lakini katika nchi zetu

zinazoendelea hili linaweza likasababisha kufilisika kwa benki au hata nchi bila kiongozi kujua kinachoendelea na hasa aina ile ya kiongozi anayedhani kazi yake

ni kuishi makao makuu au Ikulu na sio kusimamia na kuhami fedha na uchumi wa kampuni au nchi.

Sio tu kwamba Teknohama imewaacha nyuma viongozi wetu bali pia kile wanachokijua ni kile wanachoambiwa tu na wataalamu wa Teknohama. Kuna viongozi

wachache sana ambao wanakaa wakawaza na kuwazua ni nini kinachoweza kufanywa na Teknohama leo na kesho katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi,

kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni.

Nitawachokoza katika haya machache. Kwanza, je, kuna kiongozi yeyote duniani ambaye ameshafikiria uwezekano kwa watoa huduma za mtandao na simu

popote/simu za mkononi kuwa ndio benki za karne hii na kadhaa zijazo?

Niulize pia ni fedha za aina gani tunazostahili kuwa nazo leo nchini na duniani? Wanaojua historia ya kuanza kwa matumizi ya kitu kiitwacho fedha wanatambua

kwamba fedha ilianza kama bidhaa za aina tofauti. Katika baadhi ya nchi mifugo ilishawahi kuwa fedha, wengine walifanya kowe au kauri fedha na jamii zingine

zilifanya mawe ya thamani kama dhahabu na vito vya aina nyingine kuwa fedha.

Aidha wengine walifanya nafaka kuwa fedha, mvinyo na sigara zilishawahi kuwa fedha na kadhalika.

Baada ya hapo mwanadamu akagundua kuwa anaweza kutumia karatasi au sarafu kuwakilisha fedha fulani. Huu ndio mwanzo wa kuzuka fedha wakilishi. Hadi

hapa fedha ilikuwa ikilindwa na thamani sawa kwa vitu kama dhahabu na fedha.

Majanga mbalimbali kama ukame, njaa, vita na kadhalika viwakapa viongozi wa serikali akili ya kuanzisha fedha kwa kutumia mabavu ya serikali [fiat money].

Fedha yenyewe haikuwa na thamani iliyolingana mahala popote, bali dola iliamrishwa iwe na thamani fulani na ikakubalika hivyo.

Fedha ya fiati [au fedha isiyo na thamani] na serikali kuchapisha makaratasi na kuamuru yakubalike kama fedha pamoja na serikali kuwakopa watu na nchi

nyingine yamechangia sio haba kwa hali ya uchumi iliyopo leo duniani.

Hivi leo pamoja na kuwepo kwa fedha ya mkopo [credit money] vilevile kuna fedha digiti au elektroniki kupitia kwenye kompyuta na mitandao mbalimbali kati ya

serikali, benki na walaji.

Cha kujiuliza hapa ni je, ndio mwisho wa safari? Na hivi kweli fedha za sarafu na karatasi bado zinahitajika kwa matumizi yote ya kiuchumi na kifedha.
Na kama kuna njia na aina mbadala ya fedha ni zipi hizo?

Je, sio kazi ya benki kuhakikisha kuwa duka la rejareja pale kijijini linaungwa kimtandao na duka la jumla katika kijiji kikubwa au mjini ili biashara ifanyike zaidi

kielektroniki na kwa kuhamisha mizigo bila matumizi ya fedha za karatasi? Na jibu utakalolipata hapa lifananishe na lile la kuunganisha shule-benki-na kampuni za

simu za mkononi ili malipo ya ada yafanyike kielektroniki? Uuzaji wa tiketi za mpira au muziki? Malipo ya nauli za daladala kwa mwezi badala ya kila siku? Vituo

vya mafuta vyenye kutumia kadi ya benki yako? Na mengineyo mengi tu.

Lengo la insha haikuwa kuonesha kuwa nina majibu ya matatizo ya kifedha na kiuchumi yanayoikabili dunia hii leo. La hasha. Lengo langu lilikuwa ni kuchokoza

mawazo kwa kuonesha kuwa bado hatujagusa chanzo cha tatizo lililopo. Na bila kufanya hivyo, yaani, kugundua kiini cha tatizo majawabu yetu kwa tatizo hilo

yatakuwa ni ubabaishaji tuu.

Ingawa bado hatujaanza kuyaonja kwa ukamilifu makali ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia lakini tusisahau kuwa ukiona wakubwa wananyolewa kwa chupa,

wewe mdogo usitaharuki kunyolewa kwa jiwe. Taharuki yetu iwe kwa kuacha uvivu wa mawazo na kuanza kujiuliza yale yasiyoyumkinika.

Na swali moja muhimu ni je, benki, kama zilivyo leo kweli ni taasisi tunazozihitaji? Au kampuni za mitandao ya tovuti na simu za mikononi zikishirikiana na benki kuu

matawi ya mikoa na wilaya na benki kata au benki mtaa ndio jawabu la menejimenti na matumizi ya fedha katika miaka ijayo?

Mfumo mbadala wa taassisi za fedha na aina mpya ya fedha ni vitu vinavyoweza kuwa na faida kadhaa kwa wanadamu.

Baadhi ya faida hizo ni pamoja na kupunguza rushwa; kudhibiti riba za dhuluma na za kiwizi; kudhibiti ulanguzi wa fedha na kupunguza kuhodhiwa kwa fedha kwa

namna ambayo hakuchangii kuondoa umaskini au kuleta maendeleo kwa nchi na watu wake.

Aidha jambo hilo litasaidia kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali; kupiga vita tabia ya watu kuishi kwa mikopo na nje ya uwezo wa mtu na kuupa utu

thamani zaidi kuliko mali au fedha.

Mfumo mpya wa taasisi za fedha kimataifa na kitaifa vilevile unaweza kuchangia kusafisha safu za wanasiasa ili nchi iwe na watu safi, wasio na ubinafsi wala ulafi na

uroho wa kutisha; kuongeza mapato ya serikali kuu na serikali za mitaa na kusimamia vyema zaidi mgawanyo wa rasilimali ili kila kitu kifanyike kwa manufaa

makubwa zaidi kwa idadi kubwa zaidi ya watu wetu.

Ninaamini kuwa mfumo huu pia utasaidia kuhakikisha fedha inatumika kwa manufaa ya binadamu na sio kwa maangamizi yake; kufanya bima na mifuko ya jamii

na pensheni kuwafaa wanachama wake zaidi badala ya kuifaa serikali na wakubwa wake na kuhakikisha kipato cha mtu na haki zake nyingine zinakuwa katika

salama zaidi kuliko ilivyo hivi leo.

Tusije tukashangaa kuwa yule Mjapani aliyeanzisha benki yake na aina yake ya fedha digiti au elektroniki pengine ndiye binadamu mwenye akili timamu kuliko

wote duniani hivi leo. Inaelekea yeye anajua dunia inakotakiwa kuelekea leo na kesho. Sisi wengine hatuoni hilo na hatulikubali japo lipo wazi. Nalo sio lingine:

wakati umefika wa kufunga fungatte kati ya benki na Teknohama ili kuondosha gharama zote zisizo za lazima na kumpa mwandamu katika nchi zote duniani afueni

kutokana na kubeba gharama kubwa za kifedha kutokana na mfumo wa benki na taasisi nyingine za kifedha uliopitwa na wakati.

Kwa bahati mbaya benki zinazokuja kudai kilichokuwa chao awali au kuwekeza upya Tanzania na Afrika kwa ujumla zinakuja zaidi na mawazo ya Kimagharibi na siyo ya Kimashariki. Mawazo ya upande mwingine ni yale ya kumlea, kumtunza na kumsaidia mweka amana kwa njia zote zile ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na miradi midogo kuwa mikubwa na pengine ya kimataifa.

Kwa maneno mengine, Benki zinazostahili kuwepo Tanzania sio zile ambazo ni mteja sikuzote anazifuata bali ni zile ambazo mara kadhaa kwa mwaka maofisa wa benki hiyo wanamuendea mteja kule aliko na kuangalia na kutathmini anayoyafnya na kisha kumshauri na kumuuliza wanaweza wakamsaidia vipi kupiga hatua mpya katika maisha na kazi au ajira yake ?

No comments:

Post a Comment