Saturday, May 7, 2011

Taifa budi liwe na kumbukumbu

KATI ya masuala yaliyoibuka katika semina, warsha, mikutano na baadaye kutangazwa na vyombo vya habari wiki hii ni pamoja na ya madai ya taifa kukosa tabia na mfumo wa kuweka na kutumia kumbukumbu za masuala tofauti yakiwemo yale ya maazimio, sera, utekelezaji na kukwama katika mipango na mikakati ya miradi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Kihistoria, Tanzania inasifika kwa kufanya maamuzi mbalimbali yaligonga vichwa vya habari katika magazeti kote duniani. Kama ilivyo katika sanaa na sayansi ya maamuzi, baadhi ya maamuzi hayo yalikuwa hayana kasoro kubwa na mengine yalikuwa na kasoro mbalimbali ambazo zilikuwa sababu tosha ya kutofanikiwa kwa nia au mradi huu au ule.

Katika menejimenti tunatambua fika uamuzi unaweza usifanye kazi wakati Fulani, lakini uamuzi huo huo ukazaa matunda katika wakati tofauti.

Aidha, tunajua fika kuwa oganaizesheni hai ambayo ina kila nafasi ya kuendelea mbele siyo ile inayotupa au kusahau maamuzi na mipango yake ya zamani bali ni ile inayoyaweka katika kumbukumbu ambazo zinaweza kurejewa na kufanyiwa kazi na pengine safari hii kufanikiwa.

Yapo maamuzi na sera mbalimbali zilizopitishwa tokea tupate uhuru. Nyingi ya sera na maamuzi hayo yalikuwa na nia njema ya watunzi wake kuona wanachangia katika mabadiliko toka hali duni kwenda bora ya watu wao. Na bado yanahitajika kwa kuwa yanahusu maadui zetu wakubwa watatu: ujinga, maradhi na umaskini. Maadui ambao hadi wa leo bado tunapambana nao na dalili za ushindi zinaonekana kuwa ngumu na mbali kuliko tulivyotarajia.

Watanzania bado ni taifa maskini, kiwango cha wanaojua kusoma na kuandika hakipandi bali kinashuka; maradhi mapya yanazuka na hivyo kuongeza idadi ya maadui tunaotakiwa kupambana nao kwa rasilimali zile zile, hadi leo Watanzania walio wengi wana dhiki ya maji, lishe bora, mazingira salama na safi na nyumba na makazi yanayostahi na kuwapa watu kiburi cha kujiona ni taifa linalojua lilikotoka na linalokwenda na sio taifa la kideiwaka tu.

Matatizo yetu ni yale yale, lakini kila serikali mpya ikiingia madarakani ama kwa kujua au kutokujua inazungumza kwa namna ambayo inaonekana kama tatizo hilo halijawahi kushughulikiwa huko nyuma, hatujui nini kilichofanyika, kwanini wenzetu walikwama, gharama gani zilitumika na ni masomo gani ambayo tunastahili kuwa tumejifunza ili katika kulishughulikia tatizo hilo hilo katika awamu mpya tujue wapi pa kuanzia na kuishia.

Tuchukulie kwa mfano aibu ya kuwa taifa ambalo maelfu ya watoto wake wanakufa kutokana na utapiamlo hali Elimu ya Kujitegemea pamoja na faida zake nyingine ilitakiwa isaidie katika kuwapa watoto wetu lishe bora. Kukatisha jambo rahisi sana lakini kulianza upya kazi kweli.

Chukulia pia suala la nyumba bora na makazi. Miradi yake ilianzia kwa hisani ya Benki ya Dunia nadhani enzi za Marehemu Bryceson ambaye ametuachia kumbukumbu njema katika hili. Katika mikoa na kanda mbalimbali ilizuka mipango ya mashirika binafsi na halmashauri na taifa lenyewe kuhusiana na jinsi ya kupambana na umaskini kuwapatia watu wetu nyumba bora. Hivi leo mwaka 2010 inaibuka mipango mipya kama vile hakuna chochote kilichowahi kufanyika kuhusiana na eneo hili. Katika hali kama hii itakuwa kila siku tuna mwendo wa mbele nyuma.

Suala la Kilimo ambacho husemwa ni uti wa mgongo wa taifa limeshapitia vipindi vya maazimio, sera na mikakati mbalimbali. Lakini hakuna jipya hapa. Kinachotakiwa ni Watanzania kuwa na kilimo cha kisasa na hivyo kutosheleza mahitaji yao yote ya chakula na pia kuzalisha mazoa yatakayotuwezesha kuwa na viwanda vya msingi kama vile vya nguo, viatu, vinywaji, vyakula vya kusindika na kuhifadhi ziada kwa ajili ya matumzi wakati wa dhiki.

Ninaamini sababu zifuatazo [sio zote] kwa kiasi fulani zimechangia hali hii ya kuwa na taifa lisilo na kumbukumbu ya kazi zake zilizofanyika huko nyuma na hivyo kuonekana kama kwa kila jambo Watanzania eti wanaanza jambo jipya:

*Kukosa maktaba ya kumbukumbu za mipango, sera na miradi ya kitaifa hai na inayofanyiwa kazi wakati wote kuonesha viongozi wapya katika wizara, idara na sehemu nyingine za kazi wapi chombo chao kilipotoka, kilipofika na kinakotakiwa kwenda.

*Kutofuata kikamilifu misingi na kanuni bora za menejimenti na utawala;
*Uchelewaji wa mabadiliko na kubadilika kila inapohitaji;
*Kupiga vita mabadiliko na uvumbuzi wa njia mpya za kufanya kazi;
*Kiwango duni katika uvumbuzi na ugunduzi wa mambo na njia mpya;
*Matumizi duni ya teknolojia mpya inayoweza kurahisisha sio tu kuweka kumbukumbu bali pia kufunza na kuendeleza wahusika;
*Siasa mbovu zisizojenga kwenye yaliyofanywa na waliotangulia bali kujaribu kufanya jambo lolote hata kama lilikwishaanza huko nyuma lionekane kuwa ni kitu kipya;
*Udhaifu wa vyombo vya ufuatiliaji na udhibiti ikiwa idara ya utumishi wa umma na mkaguzi mkuu wa serikali na vingine kama hivyo.

Nini kifanyike?

Ili taifa liweze kuwa na kumbukumbu ya shughuli zake mbalimbali ipo haja ya kutumia teknolojia kuhakikisha kuwa maamuzi, maazimio, mipango, mikakati, malengo, sera, tathmini, mwitiko, nyaraka mbalimbali, miongozo ya uendeshaji idara, wizara, makampuni na kadhalika vilivyokuwepo zamani vinatafutwa na kuhifadhiwa pengine katika kitu kitakachoitwa maktaba au makumbusho ya maamuzi, sera, mipango,mikakati na mwitiko mbalimbai ya kitaifa, kiwizara, kimkoa, kiwilaya hadi ngazi ya chini kabisa inahifadhiwa.

Pamoja na kuhifadhiwa kuwepo na mtandao utakaomwezesha kiongozi au mwananchi yeyote kurejelea na kunasua chochote anachokitaka ili katika kuendeleza jambo fulani asiwe analazimika tena kugundua gurudumu jipya la maendeleo. Moja linatosha. Kazi ni kulisukuma lifike kileleni linakotakiwa.

Pili ni muhimu kutoa elimu ya menejimenti na uchumi kwa lugha ya Kiswahili ili hata yule mtendaji wa chini kabisa katika wizara, idara, mkoa, wilaya, tarafa, kata aweze kujua umuhimu wa maamuzi na uongozi wake katika kuiendeleza nchi na jamii yetu.

Hili likifanyika tutakuwa tunawawezesha viongozi na wananchi wengi zaidi kukumbuka kwamba 'njia hii tulishapita na kulikuwa na chatu mmeza watu na hatukwenda mbali, vipi hawa jamaa wanataka kutupitisha tena njia hii yenye hatari ile ile.
Chuo Kikuu cha Mzumbe kina uwezo kabisa kama kikiwezeshwa kutafsiri masomo haya ya uchumi na menejimenti kwa Kiswahili na pia kuwa na mtandao nchi nzima wa kuwafundisha viongozi wa juu na wa chini elimu hii muhimu katika uongozi.

Ipo haja pia ya kuainisha fursa, matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania, kwa maana, ya kuainisha masuala haya bayana halafu kuandalia mikakati ya kuyashughulikia. Hili litafanyika, hata hivyo, vizuri zaidi kama kila idara, wizara na kiongozi nchini watashirikishwa katika kujua matatizo na maadui wetu wa zamani na wapya ni wepi na tuwashughulikie vipi ili tushinde tena kwa haraka kuliko wengine wanavyodhania.

Tuna matatizo na fursa mbalimbali kama sio changamoto katika vita dhidi ya ukimwi, utapiamlo, malaria, unene wa kupindukia kwa wanaokula vizuri mno na magonjwa mengine ya kuambukizana.

Tuna changamoto pia katika suala la kila mwananchi kuwa na nyumba bora, maji safi, umeme na mazingira safi na salama. Tuna changamoto la usafiri na uchukuzi usiowakera au kuhatarisha maisha ya wanaotumia barabara.

Tuna changamoto karibu katika kila sekta ambazo zinahitaji kwa hakika kujua tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Na ni baada ya kuyajua hayo yote ndio tunapoweza kukaa na kuandaa pengine mipango na mikakati ya kimaendeleo ya aina mpya na inayorejelewa kila kipindi bila kuingiliwa na tashwishi za kisiasa au ubinafsi na hivyo kusababisha kutofanikiwa.


Nimalizie kwa kusema kwamba bila taifa na viongozi wake kuzingatia kwa makini kule tulikotoka, tulipo na tunapokwenda; kuthamini kilichofanywa na wengine huko nyuma; kujifunza kutokana na makosa ya wengine na kulikumbusha taifa kuwa linalotakiwa kufanyika sio jipya ila ni muendelezo wa lile ambalo hadi leo halijafanikiwa itakuwa ni kazi kweli kujikwamua hapa tulipo.

Hili inahitaji kuijuza historia kama ilivyo. Kupiga vita wanaokataa mabadiliko na uvumbuzi wa njia mpya za kufanya kazi na kuwa na serikali ya wachache, lakini inayochangiwa mawazo na fikra na wengi katika kutatua matatizo ya wananchi na kuzichangamkia fursa na changamoto za kimaendeleo ziliopo mbele yao pale walipo.

No comments:

Post a Comment