Tuesday, May 24, 2011

Nani anayestahili mshahara mzuri?

KATIKA nchi nyingi za Kiafrika na zilizobaki nyuma kimaendeleo, hadi leo suala la mapato kutokana na mishahara lina walakini ambao unachangia nchi hizo

kubakia masikini miaka nenda rudi.

Walakini huu ni kule kuonekana kutokuwa na haki au uwiano kati ya mshahara mtu anaoupata na mchango wake kwa maendeleo ya nchi na watu wake.

Mfumo huu wa mishahara umerithiwa toka kwa wakoloni ambao walikuwa wameamua kujilipa wao walivyopenda bila kujali kuwa wanajenga au wanaharibu nchi.

Hivi leo ili mradi tu unaingia kwenye duru za utawala katika ngazi kuanzia ile ya wilaya kwenda za juu una uhakika wa kulipwa mshahara na masurufu mengine

manono bila ya kuwepo kwa taratibu za kuangalia kama mchango wako una thamani ya mshahara unaolipwa.

Katika hali kama hii kuna idara, wilaya, mikoa na wizara ambazo watu wanaamini kuwa zinaingiza hasara mara mbili kwani kuna watu wasiochangia maendeleo ya

sehemu husika au pengine wanavuruga mambo huko, lakini bado pia wanalipwa vizuri tu.

Hatusemi viongozi hawastahili kulipwa vizuri. La hasha. Lakini kuna ulazima katika miaka hii ya sasa ambayo watumishi wote wa umma wanaweza wakafutwa kazi

na watu wengine pengine wenye uwezo mkubwa zaidi yao kuchukua nafasi hiyo na kazi yao ikawa bora zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma, kuhakikisha kuwa

tunaoanisha mapato ya mtu na mchango wake kwa maendeleo ya jamii na yale ya nchi kuanzia ngazi ya udiwani hadi uwaziri.

Kwa maneno mengine, kila shilingi anayolipwa mtu lazima ionekane yeye anachangia kurudisha shilingi ngapi katika hazina ya nchi.

Dunia ya leo imebadilika. Nchi haiwezi kuendeshwa kama biashara isiyokuwa na hasara na faida. Ikiendeshwa kwa namna hiyo, yanayotokea Ugiriki hivi leo

yanaweza kuwa ni mambo ya kawaida katika nchi zetu baada ya miaka michache.

Ni lazima tuendeshe nchi zetu kama vile tunaendesha makampuni binafsi ya watu ambayo yanajali na kufuatilia kwa karibu thamani ya mtu na mchango wake kwa

faida na ufanisi wake; vilevile haikubaliki kufanya matumizi ya fujo yanayoweza kuhatarisha hatima ya chombo husika.

Kwa maneno mengine, Tanzania ni kampuni kama kampuni nyingine yoyote. Wananchi wake ni waweka hisa katika serikali yao. Ama serikali hiyo inaweza

kuendeshwa kifaida au kihasara na wao ama wakafaidika na faida hizo au wakala hasara kutokana na uongozi mbovu.

Njia za mawasiliano, elimu na maarifa yaliyopo, maendeleo ya teknolojia mbalimbali na changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu zinatulazimisha

kuhakikisha kuwa tunaachana na utamaduni uliopitwa na wakati wa kuamini eti serikali haiwezi kufilisiwa au kuishiwa.

Lakini, kubwa zaidi ni lile la mabadiliko ya kimtazamo na kimsimamo kuhusu ni watu gani ambao kwa kweli ndio wanaostahili kulipwa mishahara mizuri ili kazi yao

izae matunda yatakayochangia watu wengine pia kupata mapato na maisha mazuri.

Kuna mamna mbili za uwezekano hapa. Unaweza ukalipa kundi la watu ambao hawana mchango wowote katika kuwawezesha kihali na kimali wananchi na

hivyo fedha yote ikaishia kwenye matumbo ya watu na miradi isiyochangia kabisa maendeleo ya nchi na watu wake, auunaweza ukawa na mfumo wa uzalishaji na

ugawaji mapato ambao unayapa makundi muhimu katika jamii uwezo wa kifedha ambao unakuwa ni chachu katika maendeleo ya watu wengine.

Kwa maneno mengine, taifa linaingiza mapato kila mwaka, lakini ni nani anayepata mapato haya na anayafanyia kitu gani, nayo yanachangia vipi maendeleo ya

nchi na watu wake? Aidha, ni muhimu kujua ni kwa namna gani nchi inaweza ikawa na mfumo wa fedha hususan katika matumizi ambao hauchangii kujenga kila

siku tabaka la wenye nacho na wasio nacho.

Ni vizuri kuangalia kuwa je, mishahara wanayopata mawaziri, makatibu wao, wakuu wa idara na mamlaka mbalimbali, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na

wengineo kama inaendana na mchango wao kwa maeneo husika. Maana upo uwezekano wa kumlipa mtu mshahara kwa miaka 5 hata 10 na mtu huyu asiwe na

chochote cha kuonyesha katika eneo lake la kazi. Ndio maana kuna wanaopendekeza katika nafasi mbalimbali za ajira; iwe kwa kuchaguliwa au kuteuliwa

panakuwa na mshahara wa kushikilia nafasi hiyo na ziada ya hapo iwe inalipwa baada ya kuona mhusika amefanya mambo yanayonekana katika eneo lake.

Kuna wanaouliza kwanini nchi kama Imarati, Malaysia, China viongozi wanajirudisha nyuma kwanza ili wananchi wapate na pale wananchi wanapokwamuliwa

kiuchumi na kijamii ndipo viongozi nao wanapoanza kujiangalia.

Tumeua karibu mashirika yote ya umma, lakini yaliyobakia mikononi mwa serikali ndiyo yaliyochoka kuliko wengine. Tatizo ni nini. Mbona Uchina bado wanamiliki

mashirika mengi ya umma na inasemakana sasa yanafanya maajabu ikilinganishwa na zamani?

Nchi au mkoa au kampuni sio fedha au mtaji au majengo au mitambo au ardhi bali ni watu. Tatizo letu kubwa hapa inaelekea liko katika kumsoma, kumwelewa na

kumtumia mwanadamu kwa namna ambayo anaridhika, anafurahia na anakuwa radhi kujitoa ili kuchangia maendeleo ya wenzake na nchi yake. Binadamu yeyote

anayeona kwamba yeye anatumika tu kama chombo au mashine na wenzake au serkali yake hawezi kuwa na uaminifu, utiifu, uadilifu na kujituma kama yule

anayejiona yeye ni mbia au mwenye hisa katika taasisi husika.

Mfanyakazi kama mtoto hukua kwa jinsi umleavyo. Mtoto ukimlea bila mapenzi, kwa kumwita mwizi, mwongo na kumwaminisha kwamba kushindwa kwake kuwa

na maisha bora sio kosa la mzazi bali ni la mtoto unategemea nini kwa kizazi chako hicho?

Huko Malaysia, China, India na Imarati pamoja na nchi nyingi tu za Kiarabu na zile za Marekani ya Kusini na Kati ambao kimaendeleo hatukuwa tumepishana sana

kwenye miaka ya 60 wameligundua hili. Ni pale tu walipoanza kumpa mtu wao thamnani na kumuamini ndipo watu wao walipoanza kufanya maajabu.
Ninaamini tukiwa na siasa na sera za kujifunza kutoka kwa wengine ziara kwenye nchi kama hizo zinaweza kutufungua moyo, roho, macho na masikio kwa kiasi

kikubwa.

Wakati mwingine, huwa najiuliza kwamba, hivi wanasayansi, watafiti, walimu, madaktari, manesi, walinzi na wanausalama, wahandisi, wajenzi na watu wengine

kama hao wanaochangia moja kwa moja kukua kwa pato la nchi ndio wangelikuwa wanalipwa vizuri kuliko wanasiasa; nchi yetu ingelikuwa wapi?

Huko Norway leo kwa kuwa mwalimu au daktari analipwa vizuri mno hafikirii kabisa ubunge au uwaziri au ubalozi. Kwao huwa ni shughuli kutafuta watu wa kujaza

nafasi kama hizo, kiasi ambacho wakati mwingine vivutio hupaswa kuwekwa ili watu wazikubali nyadhifa kama hizo.

Ni kawaida ya binadamu sikuzote kutaka apate yeye hata kama wengine wanakosa. Kwa Waafrika husemekana wapo wanaoshughulikia wengine ili wakose

kabisa.

Hayo yote tisa, kumi ni kwamba, haitakaa hata siku moja mtu kuridhika na anachokipata kama mshahara au kipato kingine. Na anayejua kiatu kinamfinya wapi

hawezi kukaa kimya bila kuonyesha na hasa pale anapojua kuwa kuna mianya kama sio mitaro na mahandaki yaliyoruhusiwa kupitisha kile ambacho kilistahili

kwenda kwake kwenda kwa wengine.
Vilevile nchi kujikuta ina watumishi wa umma wasio na ubunifu wala uzuzi katika kuwawezesha watu kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo na pia kugeuza matatizo

kuwa ni fursa za watu na nchi kuingiza pato zaidi. Wa mbili, kwa kweli, havai moja!


Kampuni, kujitangaza na mchango kwa jamii..... Sammy Makilla KWANZA , nisionekane kwamba sina shukrani. Ninazishukuru kampuni zote za Tanzania na za

nje ambazo hivi leo zinapigana vikumbo sio tu katika kujitangaza, bali la zaidi katika kuirudishia jamii ( kama wanavyosema wao) kile jamii inachowapa wao. Hata

hivyo, kuna mambo kadhaa ambayo yamekuwa yakiendelea kama sehemu ya kujitangaza na sehemu ya kuisaidia jamii ambayo kidogo yananitatiza. Mathalani,

hivi kweli kupiga rangi nyumba kama sio banda bovu ni njia nzuri ya kujitangaza ? Sitaki jibu sasa hivi hebu fikiria wewe kwanza. Swali jingine, hivi kuwahimiza watu

katika nchi maskini wao wenyewe kutumia ili ndio washinde zawadi nayo pia ni njia sahihi ya kuitangaza na kuirudishia jamii kile inachopata toka kwa wanajamii

husika? Halafu tujiulize pia maswali haya: Jamii yetu iko wapi ? Tunataka iende na ifike wapi na lini? Kwanini ? Na kuna matatizo au vikwazo gani vinavyochangia

jamii yetu kuwa hapa ilipo kiujumla kama jamii maskini? Lengo la makala haya ya leo ni kuonesha kwamba kupaka rangi nyumba mbovu; kuhamasisha watu

kutumia (consumerism) na kuwahimiza watu wajione tofauti na wanajamii wenzao kwa hili au lile pengine inaweza ikawa sio njia sahihi ya kujitangaza na

kuirudishia jamii kile kinachostahili kurudishwa.

Nitajaribu kuonyesha mambo mbadala ambayo kama yakifanyika kampuni hizo zenye kujisikia zina wito wa kuwajibika kijamii zitakuwa zimefanya mambo bora na

ya maana kweli kweli. Maana kinachofanyika hivi sasa na kampuni mbalimbali nchini ni sawa sawa na kumpa mtu mzima 'pipi' au kitu kingine kitamu, kama vile

bado mtu ni mtoto wakati ugonjwa wake ni wa kiutu uzima." Yapo mambo mengi yanayoweza kufanywa na makampuni hapa nchini ambayo sio tu yatachangia

kubadili maisha ya wananchi bali pia kuongeza maradufu au zaidi faida za makampuni hayo. Nitajaribu kuorodhesha na kuelezea kwa uchache baadhi ya mambo

hayo nikitaraji kuwa huwa ni mwanzo wa mjadala wa ushirikiano kati ya wananchi na makampuni mbalimbali hapa nchini yatakayolenga sisi wote kuwa washindi.

Ni muhimu kama kweli kampuni zinataka zionekane zina nia ya kumsaidia Mtanzania kujiingiza katika kurahisisha kupatikana kwa zana za uzalishaji mali katika

kilimo na viwanda vidogo vidogo kwa mamilioni ya vijana wa nchi hii, ambao sio rahisi kupata mtu wa kuwaajiri. Kitendo cha kuwawezesha watu hawa kujiajiri ni

kitendo kitakachohakikisha makampuni hayo siku za mbele kuwa na wateja wanaongezeka badala ya kupungua. Kitendo hicho kinaimarisha amani na

mshikamano nchini kitu muhimu kwa mafanikio ya makampuni yote nchini. Ninaamini kwamba njia nyingine ya kuwajibika kijamii kiutu-uzima ni kuwasaidia walimu

na wahadhiri kwa hali na mali ili walimu na wahadhiri wawe na hali bora kimaisha na hivyo kuboresha elimu zaidi katika ngazi ya msingi, sekondari na vyuo.

Ninaamini, mathalani, kampuni A inaweza ikawadhamini walimu kadhaa wa mahesabu; kampuni B Kemia; kampuni C Fizikia; kampuni D-Utalii; kampuni

E-Biashara na kadhalika. Wao wenyewe wataamua nini cha kufanya, lakini mwisho wa siku walimu hao wanajikuta wana muda zaidi wa kujitolea kuboresha elimu

kuliko ilivyo hivi sasa. Kampuni zitaweza kujitangaza kwa walimu au wahadhiri hao kuitwa. Kwa mfano, mwalimu wa mahesabu wa Sasatel, Ali Bakari wa shule ya

Benjamin Mkapa amesema… Sambamba na hili ni kuwasaidia madaktari na wauguzi ili wafanze tiba na uganga bora zaidi. Hapo napo kitakachofanyika kwa

mfano ni kampuni moja kudhamini madaktari wa magonjwa ya watoto kwa kupunguza gharama na kuchangia pengine mkopo wa ujenzi wa nyumba au

ununuzi/utunzaji wa gari kwa mhusika au ulipiaji ada wa mtoto wa daktari au muuguzi nao pia wakaitangaza kampuni husika, mwalimu wa kemia wa Pepsi Cola,

Mary Mangesho amesema kwamba ....... Tunapokuja kwenye ngazi ya wananchi wengi ni muhimu kuangalia upatikanaji wa nishati ya nafuu zaidi, hususan

umeme wa mafuta, maji, jua au upepo kwa matumizi ya nyumbani chapuchapu ili kuchangia kupanda kwa ubora wa hali ya maisha ya mwananchi, kumkinga na

maradhi ya kutumia nishati hafifu na za hatari na vilevile kumrahisishia ununuzi na matumizi ya vifaa bora vya nyumbani vinavyohitaji nishati hiyo pia ikiwemo vile vya

kampuni zitakazochangia kupatikana kwa nishati hiyo. Tatizo jingine kubwa katika miji yetu ni lile la upatikanaji maji. Kampuni zikichangia kufanya upatikanaji maji

kirahisi vitakuwa vimemkomboa mwanamke na kazi inayotumia muda wake mwingi, lakini siyo ya uzalishaji mali moja kwa moja. Muda unaookolewa hivi

utawasaidia watu hao kujiajiri katika kazi yenye kipato na tija zaidi na hivyo kuwapa uwezo wa kununua bidhaa zaidi kutoka kwa makampuni mbalimbali hapa

nchini. Kazi hii ya ufikivu wa maji majumbani na mashuleni sio rahisi na hatuwezi kuwaachia watu au makampuni fulani tu au serikali yenyewe kuifanikisha. Pale

inapowezekana wale wenye uwezo na hasa makampuni makubwa nayo yachangie pia kwa wanajamii kupata maji safi na salama. Vilevile upatikanaji wa maji ya

uhakika utachangia sio haba kuwa na miti, bustani na maua yanayopendezesha mitaa na miji yetu. Na hili nalo litachangia kujenga mvuto wa miji yetu kwa watalii

kwa miji yetu kuonekana ni ya kistaarabu zaidi. Vijana wengi wa kitanzania hawana ajira. Na hakuna njia bora zaidi ya kuwasaidia kuliko ile ya kuwawezesha wao

wenyewe kujiajiri. Ni kweli wanamichezo sasa hivi wanapata fursa hiyo, lakini vijana wote sio wana michezo. Kadhalika sio michezo yote inayofadhiliwa kwa kiasi

hicho; kwa hiyo bado kuna umuhimu wa kuyaangalia wanayoweza kufanya vijana ikiwa ni pamoja na kazi za kilimo, viwanda vidogo vidogo, sanaa, uigizaji filamu,

uandishi wa vitabu, uchoraji katuni, uchekeshaji, matumizi ya kompyuta kuzalisha vitu mbalimbali na kuona ni kwa namna gani kampuni zinaweza kujipanga na

kuwasaidia vijana wetu ili wajikomboe kiuchumi na wakati huo huo waweze kutoa mchango wao unaohitajika sana katika maendeleo ya nchi yetu. Katika hili

kampuni zinaweza kujipanga na kuanzisha mfuko wa maendeleo ya ujasiriamali miongoni mwa vijana Tanzania ambao utasimamiwa na watu wanaoaminika na

wenye utaalamu unaostahili na kazi yake kubwa itakuwa ni kuwahamasisha vijana kuja na mawazo juu ya nini kinachoweza kuwakomboa. Kisha taasisi hiyo

iwape elimu na maarifa katika masuala hayo pamoja na kuwafungua macho kwa kuwapeleka nchi za nje kujifunza zaidi ujasiriamali katika eneo husika. Baada ya

hapo itawafadhili kwa mkopo usio na riba utakaochangia uanzishwaji na uendelezaji wa wazo na hatimaye mradi wao. Katika mikoa Kando ya Ziwa kuna tatizo

sugu la kisasi na wizi wa mifugo ambalo juzi limeishia kwa mauaji ya watu 17 wa ukoo mmoja kuuawa kikatili. Huko mradi wa kisaikolojia na kijamii ili kumaliza

ubabe na ukatili miongoni mwa watu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ungelitoa mchango mkubwa katika kumaliza tatizo hilo ambalo serikali na vyombo vyake mpaka

hivi leo vinakiri ni zito kuliko wanavyofikira wao. Kuna hatari ya ujinga kurudi tena Tanzania je hatuwezi kupeleka sinema za kila mwezi kwa magari huko vijijini ili

kuwaongezea elimu, burudani na starehe wananchi ? Bila shaka mradi huu sio tu utafanya kazi hizo hapo juu bali pia utakuwa ni njia kubwa ya matangazo ya

biashara husika kufika vijijini kirahisi.
Kinachohitajika hapa ni kwa kampuni hizo kuja na kuanzisha kampuni ya kupeleka sinema mitaani na vijijini itakayokuwa ikijiendesha yenyewe kibiashara. Jambo

lingine linaloweza kufanywa na kampuni zinazoamini kuwa wananchi ni wabia wao wa kudumu ni kuchangia kuifanya mitaa, vitongoji, vijiji na miji yetu kuwa safi na

salama zaidi. Bila maneno mengi wote tunajua umuhimu wa usafi na usalama katika maisha yetu. Hili likifanyika ni dhahiri kampuni hizo zitakuwa zinajiongezea sio

tu heshima bali kuaminiwa kwao mbele ya macho ya wananchi. Hali kadhalika kampuni hizo zinaweza kusaidia kuwepo kwa usafiri wa kistaarabu na heshima

zaidi kwa umma kwa kuwaleta wataalamu na ikiwezekana wawekezaji waweze kushauri watu na nchi ni mambo gani yanaweza kufanywa ili wenye daladala na

mabasi mengineyo wafanye kazi zao kiungwana na kistaarabu zaidi. Wito mwingine ni ule wa kufadhili michezo mbalimbali zaidi ya mpira wa miguu kupitia shule

za msingi, sekondari na vyuo vikuu. Hakika nchi hii haiwezi kuendelea kimichezo kama shule na vyuo havishirikishwi kikamilifu katika kuandaa wachezaji na

washindani wa kesho. Kubwa zaidi katika hili ni kwamba, kwa kufanya hivyo kutachangia pia umoja, udugu na mshikamano wa wanafunzi na vijana wa Kitanzania

popote walipo. Pamoja na hili ni lile la kusaidia kuanzishwa kwa ujenzi wa viwanja vya michezo kwa kila shule, chuo, kata, kijiji na mji nchini kama kusudio la awali

la kuwa na miundombinu ya kisasa nchi nzima itakayotuwezesha pia kujiandaa kwa kuwa wenyeji wa mashindano makubwa ya kimataifa siku za baadaye.

No comments:

Post a Comment