Monday, May 23, 2011

Masoko ni muhimu kufanikisha kilimo kwanza

ARDHI inayofaa kwa kilimo Tanzania inasemekana ni kama kilomita za mraba886,037. Hi ni sawa na ardhi yote inayofaa kwa kilimo kwa nchi nne za Afrika Mashariki, yaani, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

Hili linaonesha kwamba kama kweli kaulimbiu ya Kilimo Kwanza itafuatiliwa kwa dhati na umakini

wa hali ya juu Tanzania inaweza ikapunguza umasikini wake kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, Kenya ndiyo inayoongoza kwa pato la taifa ikiwa ni dola za Kimarekani 1,125 kwa mwaka. Aidha Uganda, Rwanda na Burundi zote zinaipiku Tanzania katika pato la taifa. Tanzania katika Afrika ni nchi ya 50 kimapato. Inafuatiwa na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia na Malawi.

Zaidi ya asilimia 60 la Tanzania bado linatokana na kilimo. Hata hivyo, kilimo hicho ni cha kizamani na ambacho hakioanishi sio tu matakwa ya soko la ndani na wateja wake bali pia bado hakijaweza kuoanisha matakwa ya masoko ya nje na uzalishaji kisayansi hapa nchini ili wakulima wanufaike zaidi na wateja wa nje. Vilevile bado kilimo Tanzania sio huru kama vile ilivyo biashara au uzalishaji viwandani. Haya ni masuala muhimu ya kisera ambayo yanahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kaulimbiu ya Kilimo Kwanza iweze kufanikiwa.

Kwa ujumla Kilimo kwanza hakiwezi kufanikiwa kama hapatakuwa na jitihada angavu na za wazi kuoanisha mambo kadhaa ambayo ni kwayo tu ndipo azma nzima ya Kilimo Kwanza inaweza kufanikiwa.

Katika makala hii nitajaribu kuonesha umuhimu wa kuoanisha matakwa ya walaji na aina ya kilimo chenye faida kwa mkulima na nchi kwa ujumla.

Kwa mapana na marefu, mipango iliyopo sasa inaelekea imefanyika kwa haja ya kukidhi zaidi mahitaji ya ndani ya nchi. Lakini kama wengi tunavyojua kilimo hiki aghalabu hakiwi na manufaa makubwa kwa mkulima. Ni kilimo kinachoweza kumpatia mkulima riziki lakini sio rahisi kumtajirisha mkulima.

Kwa maneno mengine ili kilimokwanza kiwe na faida zaidi kwa mkulima ni lazima kiwe cha aina mbili. Kwanza, kile cha kutosheleza mahitaji ya nyumbani na pili ziada au mazao tofauti ya kuuza nje.

Ili kufika huko ni lazima kujenga daraja kati ya walaji wa nje na mkulima. Kwa mfano, baadhi ya wakulima huko Kenya na Uganda sasa hivi huwa hawalimi bila kuwashirika walaji wa EU au Ulaya. Walaji hawa hutoa ushauri wa mambo mbalimbali ikiwemo ardhi inayofaa kwa kilimo cha zao husika, ubora wa zao hilo, wingi wa zao hilo na jinsi ya kuhifadhi na kusafirisha zao hilo ili lifike katika hali inayokubalika katika soko la Ulaya.
EU ni sehemu moja tu katika dunia hii. Kuna nchi pia kama Uchina, India, Russia, Marekani ya Kusini na Kati, Afrika Magharibi, Kaskazini na Kusini ambazo zinaweza kuwa wateja wazuri wa mazao ya wakulima wa Tanzania. Kazi ni kutafiti na kujua masoko hayo yako wapi na kisha kujenga ubia wa biashara ya kilimo na nchi husika na watu wake.

Jambo hili linastahili kuwa ni mojawapo ya kazi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Haiwezekani kuachia mikoa au wakulima kufanikisha hili.
Ni dhahiri basi kuwa kutoa mafunzo katika elimu ya masoko na mikakati ya kunufaika na masoko hayo ni kazi inayostahili kwenda sambamba na mipango mingine katika Kilimo Kwanza. Bila elimu hii jitihada zote zitaishia katika upofu wa kutojua na kutokuwa na mahala pa kuuza kile kilichozalishwa.

Wakati huo huo ni muhimu kuwaeleza wakulima sasa wana soko huru kwa mazao yao na hakuna atakayelazimishwa kumuuzia mlanguzi iwe shirika la umma au mtu binafsi.
Hili lifuatiwe kwa vitendo vinavyoonesha kumsaidia kila mkulima kuweza kuuza anachokizalisha popote pale anapotaka bila kikwazo chochote.

Ni muhimu pia kwa serikali ikishirikiana na mabenki na vyombo vingine vya fedha kuhakikisha kuwa matumizi ya teknolojia na sayansi katika kilimo yanaongezeka siku hadi siku. Bila hivyo, itakuwa ni vigumu kuweza kuzalisha kwa wingi, ubora na kwa wakati kama walaji watakavyotaka.

Sio lazima tulime kila kitu. Ni bora zaidi kuchagua mazao, mifugo na samaki wachache ambao tunaamini mazingira yetu yatatufanza tuzalishe kilicho bora kuliko watu wengine duniani. Kwa namna hii tutajenga uwezo utaotufanya kutegemewa katika bidhaa fulani fulani duniani wakati wote kuliko watu wengine.

Aidha ni lazima tuwe na mikakati ya kuoanisha tabia,mahitaji na ukubwa wa masoko na uzalishaji mazao tutakayoamua kuzalisha. Hili ni muhimu ili kujenga tabia ya kuaminiwa na soko kwamba wakati wote tutakuwa tunaweza kuzalisha kile soko inachokitaka tena kwa wakati unaokubalika.

Hivi sasa walaji wa Ulaya wana aina na viwango vya mazao wanayokubali kununua toka nchi zinazoendelea. Ni lazima tujue vitu hivyo. Matakwa haya yanaweza yakatofautiana na yale ya Russia au Uchina au Marekani ya kusini. Ni lazima tulitofautishe hili na hivyo kumpa mlaji kile anachokitaka. Kwa maneno mengine ni muhimu kumuonesha mteja kwamba yeye ni mfalme na sisi ni watwana kwake. Maana inasemwa kuwa mtumikie kafiri upate mradi wako.

Unyenyekevu huo ni kitu kigumu kwa wengi. Lakini ni mojawapo ya sifa muhimu ya kumpata na kuendelea kuwa na mteja wa aina yoyote ile. Bila unyenyekevu wa namna hiyo hatutaweza kuyalinda masoko tutakayokuwa nayo. Haya yote yanahitaji maarifa au elimu ya namna fulani kwa wazalishaji mazao mbalimbali hapa nchini. Na kama ndivyo hivyo tuhesabu hili pia nalo ni eneo la uwekezaji utakaokuja kuwa na matunda mema kwa upande wetu.
Mtihani mkubwa ulio mbele ya taifa hili na wakulima na washika dau wote katika Kilimo Kwanza ni ule wa kuwepo kwa mifumo ya uchukuzi na logistiki toka pale zao linapolimwa hadi kufika mezani kwa mlaji huko nchi za nje.

Ili Kilimo Kwanza kiwe na mafanikio yaliyokusudiwa ni lazima vyombo na njia zetu za barabara, reli, anga na majini zifanye kazi bila matatizo.

Ipo haja ya kuimarisha mifumo iliyodorora ya barabara na reli; kama ilivyo haja ya kununua vyombo vya majini na angani vitakavyochangia kuondoa tatizo la uchukuzi wa mazao yatakayolimwa na wakulima mbalimbali nchini.

Wakati umefika wa kutoa tena kipaumbele kwa ujenzi wa miundo mbinu husika kwa kuelekeza rasilimali za taifa katika maeneo mbalimbali yatakayochangia kasi ya kukua kwa uchumi wetu na kupunguza umasikini nchini.

Kwa viongozi wetu wanatakiwa wajiulize kama ni bora kununua magari ya kifahari au matrekta na ndege na meli za kusafirisha mazao ya mkulima kwenda kwa walaji nchi za nje ?

Upo umuhimu wa kuangalia pia uwezekano wa serikali kuuza majengo yake yote mjini Dar es salaam kwa bei nzuri na kuhamia Dodoma kwa ulaini huku wakiliacha Jiji la Dar kuwa jiji la Biashara asilimia mia kwa mia.

Hili likifanyika sio tu tutakuwa na Makao Makuu ya nchi yanayofanya kazi iliyokusudiwa bali pia tutakuwa na malori ya barafu, treni za barafu, meli za barafu
na ndege za barafu kusafirisha mazao yetu ndani na nje ya Afrika kwa urahisi na kwa faida kubwa zaidi kwa watu na nchi yetu.

Jambo lingine muhimu ni kuangalia upya nafasi ya ujasiriamali jamii katika kilimo kwanza.

Ujasiriamali jamii katika kilimo ni aina ya uwekezaji utakaotegemea rasilimali na nguvu za wananchi katika kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo kwa kusaidiwa na serikali, mabenki na vyombo vingine vya fedha na ikiwezekana pia kwa ubia na walaji toka nchi za nje. Kwa namna hii, idadi ya wanaowekeza na watakaonufaika na kilimo itakuwa kubwa japo watakaokuwa wanashughulika na kazi za kilimo moja kwa moja itakuwa ndogo. Maana kadri uzalishaji mali unavyoongezeka katika kilimo kwa kutumia sayansi na teknolojia ndivyo idadi ya wafanyakazi wanaohitajika inavyopungua. Hawa wanaopungua wataingia katika sekta za biashara na huduma ambazo kwa wakati huu zitakuwa zikipanuka na hasa kama KIlimo Kwanza kitalenga pia katika kuwanufaisha watalii na wageni wanaokuja nchini mwetu.

Katika siku zake za mwanzo Kilimo Kwanza kinastahili kupata nafuu ya kodi na ada nyingine kwa kiwango cha juu kabisa. Hii ni kutoa nafasi kwa wakulima kujenga uwezo na rasilimali muhimu zitakazorahisisha wao kutoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya viwanda na sekta nyingine hapo baadaye.

No comments:

Post a Comment