Tuesday, May 24, 2011

Umaskini hauruhusu demokrasia ya kweli

ASILIMIA takriban 85 ya Watanzania wako vijijini. Maeneo yenye umaskini mkubwa na ambako wachache wanaishi kwa zaidi ya dola mbili kwa siku. Ni maeneo ambayo watu wakilala, wakiamka hawafakirii jingine ila jinsi ya kupata nusura ya chakula na maji kwa siku inayofuatia

Wapiga kura wengi walioko vijijini ni watu wanaoishi kwenye manyata au viota na sio nyumba zinazoweza kuitwa nyumba. Huku ndiko ambako wakati mwingi hospitali hazina dawa na ingawa kuna shule lakini shule zenyewe hazina walimu wala vifaa vya kufundishia. Ni maeneo ambayo kwa kila hali yako kinyume na maeneo ya mijini. Kiasi kwamba sasa tunazungumzia juu ya apatiheidi kati ya maeneo mjini na vijijini.

Wako wanaosema kwamba chama kinachotawala hakiwezi kuwaodnoa watu kwenye umaskini kwa sababu huu ni mtaji wake, yaani, jinsi watu wanavyokuwa maskini ndivyo ambavyo inavyokuwa rahisi kwa chama tawala kushinda.

Ukweli ni kwamba, hatua yoyote inayosaidia kuwaondoa watu kwenye umasikini na ujinga ni hatua itakayowapa wale wanaowezesha hilo kufanyika majeshi tosha

ya kupambana na wapinzani wakati wote ule. Kama kuna watu wachache wanaofikiri kuwa ili kushinda ni lazima kuwaacha wananchi kwenye lindi la umasikini mkubwa basi hao ni watu wachache na wamepotoka ile mbaya kisiasa.

Ubora wa maisha ya Mtanzania na hususan katika hali yake ya kiuchumi na kielimu ni mambo peke yanayoweza kumuwezesha kujikita ipasavyo katika harakati za

demokrasia. Umaskini na ujinga wa wananchi vijijini kwa maneno mengine ni chanzo cha wananchi kushindwa kuzielewa na kukubali siasa za kidemokrasia.

Kutokana na umaskini wao wananchi huko vijijini hawawezi kutafsiri misaada inayokwenda kwao kama hongo. Hata kama misaada hiyo ndiyo kwanza inayowafikia

wakati huu wa kampeni za uchaguzi.

Utamaduni wa Kiafrika nao umejengwa katika misingi ya kuwaheshimu na kuwazawadia wanaokukumbuka kwa kuwapa kitu fulani bila kujali muda husika. Ipo kazi kubwa ya kuchanganya mila zetu na matakwa mapya ya utawala wa kidemokrasia katika nchi zetu. Binafsi, ninaamini kutegemeana na kiwango ambacho tunauheshimu utamaduni wetu, ndivyo pia tutakavyofanikiwa katika masuala ya kidemkorasia na masuala mengine ya kimaendeleo.

Umaskini wetu unachangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya watu wetu mijini na vijijini kuishia kutumia nguvu na musuli zaidi kuliko bongo zao. Kutokana na hili inakuwa sio rahisi wao kuchakachua masuala yanayozungumzwa na wanaotafuta kura na vyama husika. Hakika bila ya kuwaondolea wananchi wetu mzigo wa kufanya zaidi kazi za sulubu tusitegemee wao kugeuka fumba na kufumbua na kuwa ni watu wanaoelewa masuala ya ksiasa kwa namna ambayo kufanya hivyo

kunaongeza mchango wao katika ujenzi wa demokrasia nchini. Uvujaji na uvimbaji musuli saa zote hauashirii hata kidogo kukua kwa demokrasia. Kwani watu kama hao hupenda zaidi kumaliza mambo yao kwa kutumia musuli na maguvu yao.
Katika nchi yoyote ile ambayo viongozi wake wanaonekana dhahiri kuwa wanaamini wao wanastahili kuishi maisha bora kuliko wale wanaowatawala haiwezi kujenga demokrasia ya kweli kwani inakuwa imeshaotesha mizizi ya watawala kama mabwana na raia kama watwana.

Serikali nyingi za Kiafrika zimejenga mifumo ambayo inafanya kupatikana kwa elimu vijijini kupitia shule zilizopo, magazeti, redio na televisheni kuwa mgumu kutokana na umaskini wa watu vijijini. Na katika nchi zote hizi ni nadra sana kukuta kuna mipango ya kufikisha habari au mawasilino vijijini iwe kwa njia ya magazeti yanayonunulika, redio zisizotumia fedha nyingi kuendeshwa na televisheni zisizohitaji umeme wa shirika la umeme la taifa kufanya kazi. Kutokona na kukosa jitihada na bidii za wazi kuwapatia watu wa vijijini kile ambacho tayari watu wa mjini wanakipata basi wananchi vijijini wanaendelea kuwa wajinga na wasioamka kisiasa na kijamii kwa hasara ya demokrasia na maendeleo kiujumla.

Bila kuiwezesha mifumo ile ile inayowafikishia watu habari na mawasiliano kirahisi na wakati mwingine bila gharama kwa msikilizaji itakuwa ni vigumu kuendeleza maarifa, ufahamu na utaalamu wa wananchi vijijini katika masuala mbalimbali. Katika dunia hii ambayo mtu anaweza akajifunza yote anayohitaji ili mradi ana mtandao na sehemu tulivu kijifunza inakuwa ni jambo la kuhoji mara kwa mara, kwanini, tunaendelea kukubali idadi ya wajinga kuongezeka nchi mwetu mwaka hadi mwaka.

Katika nchi ambayo ni watu wachache wanaopata mahitaji ya msingi muda wa wananchi walio wengi hauwezi kutumiwa kujenga demokrasia bali utatumika katika kutafuta mahitaji hayo ya msingi. Huu ndio ukweli na hatuwezi kusema vinginevyo. Kwa sababu hii chaguzi katika nchi husika zinakuwa ni jambo la maazoea na sio la kuleta mabadiliko ya msingi katika jamii husika.

Isitoshe pale ambapo baadhi ya taasisi na watu wanatumika kuwatishia wananchi kuwa jambo zuri na lenye faida katika maisha yao siku za baadaye ni jambo baya na eti bila watawala waliopo kuendelea kutawala kutakuwa na umwagaji damu katika nchi ni vigumu; kwa namna gani watu wanaweza kujifunza na kujenga imani katika mifumo na miundo ya kimageuzi inayohitajika kuwepo ili nchi ijenga na kuimarisha demokrasia miongoni mwa sehemu zake, taasisi na wananchi wake.

Ili kujenga demokrasia ya kweli lazima nchi yoyote iwe na mikakati ya kuondoa umaskini kwanza : Tofauti na usanii mwingine uliofanyika, njia kuu za kuondoa au

kuurejesha nyuma umaskini ni pamoja na

• Kuhakikisha kila familia katika nchi husika ina nyumba. Ukipatia kila familia nyumba tayari unakuwa umeuondoa umaskini kwa asilimia hamsini

katika nchi. Kwa jitihada za wananyumba wenyewe na changamoto ndani ya makazi husika tayari nyumba itakuwa inawasaidia kuingiza kipato kwa kiasi fulani.

Kwa kuwa baba na mama watakuwa hawawazi tena suala la usalama wa familia yao , kupanga na ahadi za kujenga basi watakuwa na muda mkubwa zaidi

kujiingiza katika uzalishaji mali.
• Mahitaji ya msingi msingi yanajulikana. Hii sera sio mpya. Benki ya dunia ilishaibuni na kinachostahili ni kuirejea na kujifunza toka kwa

wengine kuhakikisha kuwa pamoja na nyumba, maji, chakula, hewa safi , malazi na huduma muhimu za kijamii zinapatikana na wote katika nchi husika;
• Upo umuhimu kuhakikisha kuwa viwango vya mrahaba toka kwa wachimba migodi mbalimbali kinakuwa cha haja na sio kudanganywa na

vimiradi vidogo vya maji, shule na barabara badala ya kuhakikisha kuwa tunaipa ardhi na watu wetu thamani sawa na mitambo ya wawekezaji katika uchimbaji

madini kwa kukubali hongo za kijinga kushibisha nafsi zao binafsi;
• Serikali isipuuze ushauri wa wananchi na wataalamu kuhusu suala la kupunguza ukubwa wa serikali na gharama zake mbalimbali kwa

kuangalia sera zake za ununuzi na matumizi ya magari ya kifahari;
• Tumekuwa tukiiendesha nchi kama matawi ya chama au klabu za mpira, hivyo wakati umefika wa kuendesha maeneo ya nchi kama kampuni

na sio klabu au shamba la bibi;
• Miaka hamsini baada ya uhuru tujiulize kwanini pamoja na kuzalisha mamia ya wahandisi wa ujenzi bado tunashindwa kujenga barabara na

reli zetu wenyewe. Na badala ya kuyapa kandarasi makampuni ya nje hivi hatuwezi kuajiri wahandisi na mafundi waliobobea kiteknolojia na kimenejimenti toka nchi

kama Cuba , Uchina , Romania , Russia , Hungary , Bulgaria na kadhalika na kazi hizi za ujenzi wa barabara na reli tukazifanya wenyewe? Hili linaweza

kupunguza umaskini wetu kwa zaidi ya asilimia 15;
• Wakati wa ziara ya mgombea urais kupitia tiketi ya CCM huko Geita tumeona adha ya maji wanayopata wakazi wa eneo hilo. Hii ni pamoja na

ukweli kuwa ziwa Victoria na Tanganyika hayapo mbali sana na eneo husika. Kwanini tunashindwa kutumia kwa mapana na marefu maji ya maziwa na mito tuliyo

nayo? Ninavyojua mimi ni kwamba, Mmisri hataki tuchote maji kwa juu, lakini tukichimba mitaro chini kwa chini kama kule Palestine na maji yakatiririka. Wapalestina

na shida zao zote hivi kweli tunakubali watushinde pia kiakili? Basi angalau tujufunze kutoka kwao!
Umaskini wetu unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama tutajaribu kurahisisha watu kufanya biashara na nchi za nje na vile vile kufanya kazi nchi za nje.

No comments:

Post a Comment