MIPANGO, mikakati na bajeti zetu hadi wa leo zimekaa mkao wa kutokuwa na haraka hata kidogo kama vile Mtanzania ataishi milele na hivyo hakuna ulazima wa kufanya jambo lolote kwa haraka.Ukubwa, uwezo wa kifedha, idadi ya vitu katika utekelezaji, kasi na utekelezaji na udhibiti wake ni mambo yanayomkatisha tamaa kabisa Mtanzania kwamba ataishi na kuona nafuu katika maisha yake.
Kwa wengi wao inaonekana kuwa watakufa kabla nafuu yoyote haijapatikana katika familia, mitaa, kata, vijiji na miji yao. Hii ina maana mtu anajiona mnyonge, mdogo sana na asiye na uwezo na ambaye yeye binafsi hawezi kuleta mabadiliko yoyote katika jamii husika.
Kisaikolojia hii ni alama 'toa' kubwa sana na kwa uhakika haimpi mtu sababu, ari, nia wala kutaka kuwa na uwezo wa kuchangia lolote katika maendeleo ya nchi kama hii kwa maana anaamini atakufa tu bila kufaidi chochote! Vinginevyo inabidi atafute njia za mkato kujinasua kimaisha.
Vinginevyo mtu anaanza kuamini kwamba kama umezaliwa masikini basi lazima ufe masikini tu, na ni matajiri, watoto na jamaa zao tu katika nchi husika wanaoweza kuwa matajiri. Ufa wa kutisha unajengeka kati ya walonacho na wasionacho. Taratibu ufa huu huja kuiangamiza jamii na kulisambaratisha taifa husika kama ilivyotokea kwingineko duniani miaka ya huko nyuma.
Abraham Maslow yule mtaalamu wa saikolojia anasema kuna ulazima wa mtu kupata na kuridhika na mahitaji yake ya msingi ndio awe na sababu ya kuwa na motisha, ari na hamu ya maendeleo na kuzikubali changamoto za kimaisha katika kufanya mambo makubwa zaidi.
Mahitaji hayo ya msingi katika ngazi yake ya motisha ni kitu cha chini kabisa katika ngazi hiyo kuonesha kweli ni mambo ya msingi sana.Yanajumuisha pamoja na mambo mengine upatikaji na utoshelezaji wa mahitaji muhimu ya kila siku ya mwanadamu kama chakula, maji, hewa safi, malazi, makazi/nyumba, mavazi, tendo la ndoa, huduma za elimu, afya na michezo au burudani.
Ni pale tu mahitaji haya ya msingi yanapopatikana ndipo mtu anapoanza kufikiria mahitaji katika ngazi za juu zaidi. Mahitaji katika ngazi za juu zaidi ni pamoja na usalama wa mtu na mali yake; kujinoma kwa kupendwa au kukubalika na wanajamii wengine; kutambulika katika jamii aliyomo na hata nje ya jamii yake na la juu kabisa kupata fursa ya kuwa kile kitu ambacho mtu huyo anapenda 'awe' katika maisha au umri wake hapa duniani.
Nionavyo mimi, hali ilivyo hivi leo, Watanzania walio wengi hawana na hawaoni sababu ya kuwa na motisha ya kufanya lolote achilia mbali kuongeza bidii, maarifa au juhudi katika lile wanalolifanya kama jambo hilo halina moja kwa moja faida kwa upande wao.
Watanzania baada ya kuvurugwa na siasa zilizopita hawaaminiani na hakuna anayetaka kushirikiana na mwingine katika suala la maendeleo.
Waulize wanaohusika na mambo ya ushirika, vijiji na shughuli zote za pamoja na hadithi zao hazitofautiani. Kila anayejiunga na taasisi hizo hujifikiria yeye kwanza kabla ya wengine. Na hajali kuharibu taasisi nzima endapo anaweza akanufaika yeye binafsi na uamuzi au jambo atakalolifanya.
Huu ni msiba kubwa katika taifa leltu na sote tunapaswa kuvuta hatua moja nyuma na kujuliza hivi kweli kwa mtindo huu-Tutafika?
Nitachukulia mfano, mmoja tu kwa kuheshimu mchango wa Profesa Anna Tibaijuka katika nafasi zake mbalimbali ikiwemo ile ya sasa ya Uwaziri wa Ardhi, Ujenzi wa nyumba na uendelezaji makazi ya binadamu.
Mahitaji ya nyumba kwa Watanznia kwa taarifa iiiyotolewa na Benki ya Dunia katika kuufikiria Mradi wa Mikopo/Fedha za Nyumba ni makubwa mara kadhaa kuliko kiasi watu na taasisi zilizopo zinazoweza kukileta katika soko. Taarifa hiyo pamoja na mengine inasema hivi: 'Jumla ya nakisi ya makazi ilikadiriwa kuwa nyumba milioni 2.2 mwaka 2000.
Kati ya miaka ya 1990 na 2001, wastani wa mahitaji ya viwanja kwa mwaka jijini Dar es Salaam ulikuwa viwanja 20,000, wakati wastani wa upatikanaji wake kwa mwaka ulikuwa chini ya viwanja 700, kukiwa na upungufu wa asilimia 97 ya mahitaji. Kwakuwa Watanzania wengi hujenga nyumba zao taratibutaratibu kwa miaka kadhaa, upatikanaji wa ardhi ni muhimu kwa ajili ya makazi.
Kwa ngazi ya taifa, mahitaji ya ardhi iliyopimwa kwa mwaka kati ya miaka 1991 na 2001 yalikuwa viwanja 150,000, wakati upatikanaji ulikuwa wa wastani wa viwanja vilivyopimwa 8,000 kwa mwaka, kukiwa na upungufu wa asilimia 95 kwa mwaka.'
Hivyo hakuna la kusisimka wala kufurahia unaposikia kuna shirika ambalo lina mpango (halijaanza kutekeleza) wa kujenga nyumba 15,000.
Hii kwa Watanzania inakuwa kama tone la maji katika bahari ya mahitaji yao. Maana ukweli ni kuwa hata Watanzania wenye nyumba hivi leo kuna baadhi yao ni sawa na kama hawana nyumba. Misonge, manyata na tembe karne hii si nyumba tena. Kwa maneno mengine zaidi ya asilimia 70 ya familia za Kitanzzania zinahitaji nyumba.
Na mpango na mkakati wa namna hii ni wa kizamani, umepitwa na wakati na ni miongoni ya ile inayopangwa wakati wanaopanga wakijua fika wengi wa wanaopangiwa watakufa kabla ya utekelezaji wake kufanyika. Yaani ni mipango isiyotoa imani, matumaini wala mategemeo ya nafuu yoyote wakati wa uhai wa mtu.
Haiwezekani kwa taasisi na wawekezaji binafsi waliopo hivi leo kutatua tatizo la nyumba kwa wingi na kasi inayohitajika. Bila shaka Shirika la Nyumba limefanya kazi kubwa sana katika miaka iliyopita.
Hivi sasa ni wakati wa kulipa shirika hilo jukumu la kuiingiza nchi katika hadhi ya mataifa yaliyo katika dunia ya pili kwa kulishughulisha zaidi na ujenzi wa Makao Makuu Dodoma na miji ya kisasa lakini sio tena ujenzi wa nyumba za makazi. Hili la makazi linahitji gia mpya ambayo itategemea zaidi ushirikishwaji jamii na miradi ya kijami inayojiendesha kibiashara na kwa kanuni za kileo za menejimenti na uboreshaji katika maeneo yote ya nchi yetu.
Ujenzi wa nyumba ni muhimu katika maendeleo yetu. Lakini kazi hiyo inachangia zaidi kuondoa umaskini na uhitaji lakini sio kuleta maendeleo ya kiuchumi. Tunahitaji NHC kuwa National Housing and Infrastructure Construction Company ili kuondokana na makandarasi bomu waliojaa nchini kwa hivi sasa.
Nimewahi kulizungumzia hili lakini pengine nilizungumzie leo kwa namna nyingine. Mimi ninaamini kwamba nyumba bora, safi na salama kwa kila familia Tanzania inawezekana. Tena kwa kasi ya ajabu na haraka sana.
Na inawezekana kwa namna ambayo ujenzi huo wa nyumba utawanufaisha Watanzania walio wengi kwa njia mbalimbali ikiwemo ajira, elimu, ujuzi, kipato, afya, usalama wa mtu na kupata msingi au mtaji zaidi wa watu kujiendeleza kwa njia iliyo rahisi zaidi kulivyo inavyofikirika leo.
Ninasema hivyo nikiamini tuna matatizo ya ajira, miji na vijiji bila mpango, wananchi kukosa nyumba bora, Watanzania wengi kutumia muda wao mwingi kudunduliza na kuwaza juu ya ujenzi wa nyumba, nchi kunuka umaskini na kukosa mvuto kwa watalii, fursa haba za kuanzisha biashara zinazojilipa na mengine kama hayo.
Ninaamini kwamba, tukiachana na miradi na mipango iliyopitwa na wakati na tukaamua kurudia machache yaliyomo katika Azimio la Arusha na kujitegemea basi vijiji, miji na mikoa kwa ujumla inaweza ikajipanga kwa namna ambayo ujenzi wa nyumba kwa kila familia unafanyika kama mkakati wa kuiinua jamii yetu kwa pamoja kutoka umasikini wa chini kabisa na kuja kwenye umaskini wa kati.
Mikoa ijipange kwa kujigawia kazi za kufanya kuhusiana na ujenzi wa nyumba hizo nchi nzima kwa maana kuwe na mikoa inayotengeneza matofali au paa au madirisha au milango au tallzi au vifaa vingine vinavyohitajika katika nyumba. Fumba na kufumbua tutakuwa na uzalishaji na ubadilishanaji ambao unaiunganisha mikoa yetu katika azma moja kuu, yaani, nyumba kwa kila familia.
Tunapozungumzia suala la kuwa na mikoa huru kiuchumi na kijamii ni changamoto inayozua mvutano kati ya pande mbili. Pande moja ni ile inayotaka kutawalal nchi kama ilivyokuwa ikitawaliwa toka enzi za Mwalimu Nyerere na Ujamaa na upande mwingine ukiwa wale wanaoamini kwamba soko huru, mfumo wa vyama vingi na utandawazi unatusukuma penda tusipende kuelekea kwenye mfumo unaoruhusu zaidi watu kujitawala wao na maeneo yao wao wenyewe na sio kutawaliwa toka mbali na waliko.
Zama za kuwadanganya Watanzania kwamba ni rais au serikali ndiyo inayotoa hela na ndiyo yenye uwezo wa kufanya hili au lile sasa limepitwa na wakati. Maana katika miaka hii nchi yetu iko njia panda. Inaweza ikachagua kuwa na serikali ya watu 'safi', kwa ajili ya watu wote na inayoendeshwa na watu. Au iwe na serikali ya wezi, kwa ajili ya wezi na inayoendeshwa na wezi. Itihari na chaguo ni leltu wenyewe. Na katiba mpya ni ufunguo muhimu katika kutuepushia balaa la kuja kuangukia kwenye aina hiyo ya pili ya serikali.
Lakini kubwa zaidi tunalolisikia na tunalolijua sote ni kuwa wananchi hawalalamiki juu ya vyama wala viongozi bali ni viongozi wanaolalamika juu ya vyama na viongozi . Wananchi wanalalamika juu ya matatizo, shida, dhiki, upungu au ukosefu wa hiki na ughali wa maisha. Kwa hiyo kilio cha wananchi ni matatizo. Na kadri serikali inavyokuwa mbali na sio palepale mkoani ndivyo matatizo hayo yanavyoendelea kutosikilizwa achilia mbali kushughulikiwa.
Makosa yaliyofanywa na awamu za serikali zilizopita isiwe sababu ya kushindwa tena kufufua moyo wa kiujamaa na kiudgu na kujitegemea na sote tukachukuiwa na mkondo wa ubepari na ubinafsi na kuwasahau masikini wa nchi hii.
Bado Watanzania wana kila sababu ya kuwa na ujima, udugu, ushirikiano katika yale mambo yanayoweza kuwahakikisha upatikanaji wa mahitaji yao ya msingi. Ubinafsi, kujitenga na kila mtu na lwake havina mwisho mzuri.
Mikoa hiyo itapanga majukumu kwa wilaya, tarafa, kata, mitaa au vijiji na kuratibu na kudhibiti shughuli zote ili kuhakikisha zoezi zima linafanyika kwa ufanisi na ufanifu wa hali ya juu.
Na pengine huu ni wakati muafaka wa kuchochea uanzishwaji wa taasisi za kijamii ambazo zitaendeshwa kwa faida ya wananchi na sio kwa manufaa ya wanasiasa na malengo yao, ikiwemo uanzishwaji wa Taasisi za Kijamii za Ujenzi wa nyumba katika mikoa mbalimbali. Na kama ikiwezekana kufufua benki ya nyumba kwa gia mpya ikiwa sasa imebatizwa Benki ya Kijamii ya Ujenzi wa Nyumba za Kuishi. Badala ya kuwa na wateja mmoja mmoja benki hii inaweza ikawa na Nyumba Mtaa Community Banks [ NYUMCOBA ] vikiwa ni vikundi vya kijamii vyenye azma ya kumuwezesha kila mwanachama kuwa na nyumba yake. Vikundi hivi vitakuwa ni zaidi ya mkopo kwani ndani yake pia kutakuwa na vikundi vya waashi, seremala, fundi maji, fundi umeme, fundi paa na kadhalika ambao katika miingiliano ya kibiashara itaiwezesha jamii kuzalisha pato si haba la ndani kutokana na ukweli kuwa sababu moja ya umaskini wetu ni kukosekana kwa miradi ya kutosha ya ujenzi wa nyumba, majumba na miundombinu.
Serikali itaingilia kati kwa kurahisisha utoaji wa mbegu-mtaji, usafiri na ruksa kwa majeshi yetu mbalimbali ambayo hayamo vitani kwa hivi sasa kuingia kwenye vita ya kumkomboa Mtanzania na kukosa nyumba ikiwemo wanajeshi wenyewe.
Imesemwa kwamba Serikali ina mpango wa ku'showcase' mafanikio yetu katika miaka 50 iliyopita. Vyema. Lakini ninaamini hakuna atakayekula na kunufaika na yale yaliyofanyika au yasiyofanyika katika miaka 50 iliyopita. Ila kila familia Tanzania itakumbuka miaka hii 50 ya uhuru ikiwa kutakuwa na mpango na mikakati kamambe ya kuhakikisha kuwa hatua za mwanzo za kutekeleza ndoto ya kila familia kuwa na nyumba Tanzania imeanza kuwa kweli wakati wa kusherehekea miaka yetu 50 ya Uhuru.
Serikali na chama kitakachojusuru kufanya hili kitatawala nchi hii kwa miaka 50 tena ijayo. Hili likidharauliwa au kushindikana tubaki na yetu macho maana kuna wengi tu wamekwishaazimisha miaka yao 50 ya Uhuru Afrika na asubuhi kuamka hawana mahala pa kulala, chakula wala matumaini yoyote katika maisha yao.
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment