JAMII nzima ya Kitanzania kwa maoni yangu, imeachwa kama yatima kwa sababu watu waliomo madarakani na wenye uwezo kiuchumi wameamua kuwa jamii yao inaishia kwa wake, watoto wao na jamaa zao.
Ubinafsi wa hali ya juu uliojitokeza baada ya Azimio la Zanzibar sio tu umegubika hatima ya kiuchumi ya taifa letu, bali pia hatima yetu ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Na kwa hali ilivyo sasa hatima hiyo haiashirii kabisa mambo mazuri.
Hadi hivi karibuni ilionekana kama vile uchumi unaweza kujiendesha wenyewe bila kuingiliwa na serikali. Lakini yanayotokea kwenye sekta ya madini, usafiri na uchukuzi, maji na umeme na kadhalika vimedhihirisha kuwa bila serikali kuwa na mkono wake katika angalau kusimamia na kuoanisha masuala haya nchi haitakuwa inajua inatoka wapi na inakwenda wapi. EWURA, TCRA, TCU na vyombo vingine kama hivyo vimeanzishwa katika wakati mwafaka na sote tunaona matunda yake.
Tatizo sasa limebaki zaidi upande wa kijamii na kiutamaduni. Ni nani aangalie kwamba jamii yetu ina maadili safi na sote tunaishi kama watu wenye umoja, mshikamano na ushirikiano kama abiria katika chombo kimoja? Ni mambo gani ambayo hayapo yanastahili kuwepo ? Ni yepi yaliyopo lakini hayafai yawepo kwa hiyo mara moja tuyaondoe ? Na je, nchi hii inaweza kukaa chini na kuja na maadili ya kitaifa yatakayokubalika na kuheshimika na walio wengi au tuendelee kuishi, kufanya kazi na kufa kama tulivyozoea?
Serikali katika nchi yoyote duniani, kwa mantiki ya ni nani mwenye jukumu la makuzi na malezi ya kijamii na kiutamaduni ni sawa na baba na mama kwa wananchi wake. Watoto wakiwa na tabia mbaya na wazazi hawasemi achilia mbali kuwachukulia hatua zifaazo je, kweli jamii inaweza kuwa na maadili na mwenendo mwema hapo kesho na keshokutwa?
Taarifa za kwamba, nchi yetu haifanyi vizuri katika suala la utawala bora ni kielelezo kizuri na toshelevu cha wazazi walioshindwa kutoa makuzi na malezi yanayoendana na miaka tuliyoko na hivyo kuiachia jamii ifanye kile ikitakacho saa zote, wakati wote. Na hili linatokea kwa sababu hadi wa leo tunapozungumza eti taifa hili linagwaya kutoa tamko kuhusu ni nini baya na nini zuri, nini uovu na nini wema, nini linalofaa na lisilofaa kwa wananchi wa nchi hii.
Kwa maneno mengine ni kwamba pamoja na juhudi mbalimbali kufanyika nje ya uongozi wa taifa za kuwa na Mikakati na Mipango ya Kimaendeleo inayojumuisha maswala ya dira, misheni na maadili taifa halina kitu kama hicho (National Strategic Plan) ambayo pamoja na mambo mengine ingelichangia sana kuamua juu ya nini kiwe maadili ya taifa na nini udhaifu na uwezo wetu katika masuala mbalimbali ambayo kwa umoja wake yakishughulikiwa yanaweza kutukwamua hapa tulipo na kutupeleka mbele.
Wanaopewa dhamana ya kuongoza nchi wanastahili kutathminiwa pamoja na
mengine uwezo na mchango wao wa kuwalea wanajamii ili waishi vizuri na watu wengine, watoe ushirikianao na serikali, waendeleze mazuri na kukomesha maovu na wawe kile wanachotaka kuwa.
Kwa mujibu wa Abraham Mslow, binadamu anataka vitu vitano katika maisha yake. Vitu
hivyo ni pamoja na mahitaji ya msingi, usalama wake, kupendwa na kuthaminiwa na
wenzake, kutambulika au kujulikana na kuwa kile anachotaka kuwa.
Mara baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kwanza,
Watanzania walikuwa wakiimba ubepari ni unyama na Kenya ni manyanga'u. Hivi leo
tumeanza na tunaendelea kujenga yale yale yatakayochangia kuwa na wanyama na
manyang'au ndani ya jamii yetu, huku kila mmoja wetu akiona hili halimhusu.
Kinadharia kama wote halituhusu basi hili linaihusu serikali yoyote iliyoko
madarakani. La sivyo nchi haina uongozi unajua hatari ya kuwa na taifa la wanyama na
manyang'au. Nitajaribu kutoa mifano mchache kuhusu ambavyo jamii kwa namna moja au nyingine inachangia kuwa na watu wenye roho mbaya, wasio na utu wala ubinadamu.
Jamii inapokubali watu kugeuzwa ng'ombe kama inavyofanyika katika usafiri wa daladala hauwezi kamwe kutegemea kuwa na watu waungwana na wastaarabu. Watu hawa ni vigumu kuwa na utu na ubinadamu. Na yeyote anayepanda daladala leo akatazama watoto, wanafunzi, wazee na walemavu wanavyofanyiwa na abiria wengine, konda na madereva watajua ninachokizungumza. Utu na ubinadamu miongoni mwetu unaendelea kupungua na sisi tunakaa pembeni kama vile hayatuhusu.
Hivi leo katika miji yetu mingi wenye magari ndio wenye haki na wanaogopeka kuliko watu wengine. Baadhi yao hawaheshimu kabisa tena mbele ya trafiki sehemu za kuvukia watu watembeao kwa miguu na hata taa za usalama barabarani. Kwa yakini majuzi niliamua kusimama pembeni ya 'zebra-crossing' ili nione kama angalau kuna dereva mmoja mwenye utu na uungwana kunipisha nipite.
Magari zaidi ya 16 yalinipita na lile la 17 lilisimama lakini kiasi cha wote tuliokuwa tukisubiri kuogopa kuvuka kwa sababu waliokuwa wanakuja nyuma bado walikuwa wanakuja kwa kasi ikionesha kuwa sasa hivi 'zebra-crossing' hazina maana na halmashauri zinapoteza fedha bure.
Somo hapa ni kwamba unapokuwa na jamii ambayo mtu kwa sababu ya fedha au mali au kitu alichokuwa nacho anakuwa juu ya sheria na wasio nacho ndio wanaokuwa chini ya sheria, basi haujengi jamii yenye umoja. Daima na hasa zikitokea ajali wenye magari ndio watakaonekana wabaya na wasio nacho wanyonge wanaoonewa. Iko mirano mingi tu huko Ulaya, Marekani kusini na kaskazini na jinsi walivyoshughulikia hili, achilia sasa kinachoendelea India na China ambako tunaweza kujifunza mengi pia. Lakini kubwa hapa ni kuwa utawala wa sheria nchini kwa baadhi ya sehemu uko usingizini tena wa pono.
Inapofikia hatua ya watu wanaotajirika kwa wizi na dhuluma kuwa ndio waheshimiwa siamini kwamba, watu hao wanaweza kujirudi wao wenyewe na wasiamini na kuchukulia kwamba fedha au mali waliyo nayo inaweza kuwapa ruksa ya kufanya chochote wakitakacho.
Ikiwa watu wanafikia kuamini kuwa huwezi kwenda hospitali au kituo cha afya na uhudumiwe kama mwanadamu tena kwa unyenyekevu na mapenzi basi utu na ubinadamu unakuwa haupo hapo. Kinacholambwa hapa ni yule anayekuja na fedha ya rushwa kuwapa madaktari na manesi ili apate huduma chapuchapu.
Kama vilevile kuna ubaguzi katika kuzisaidia dini ili zijenge jamii bora, basi ni dhahiri dini isiyowezeshwa itashindwa kuwalea watoto wa waumini wake na upo uwezekano mkubwa waumini wa dini hiyo sasa au baadaye ndio watakaokuwa sio tu watu walio nyuma kimaendeleo na kimaadili. Ni muhimu kwa serikali kuweka uwiano na kutoa nyenzo za hali na mali ili kila imani katika jamii iwezeshwe kwa njia mbalimbali kuandaa kizazi cheney maadili zaidi ya ilivyo hivi sasa.
Ikiwa magereza yetu yanakuwa ni mahala pa maisha duni na yanayofanana na ya mazizi ya wanyama, huwezi kusema eti utawarekebisha wanaotoka huko kuwa raia wema. Ni muhimu tukaiga toka kwa wengine magereza yanavyostahili kuwa katika miaka hii ili kazi ya kurekebisha ifanyike lakini sio kuwafanya wafungwa waoze zaidi kuliko walivyokuwa mwanzo.
Hali kadhalika kama vyombo vya habari vinaachiwa kuvunja maadili angalau yale machache yaliyopo na hasa kwenye televisheni na redio tutakujashtukia tunajiingiza katika matatizo makubwa zaidi ya kitaifa ambayo itakuwa kazi kwelikweli kujitoa.
Katika elimu, biashara, kilimo, ufugaji, uvuvi, uzalishaji mali viwandani na kazi maofisini bado Watanzania tuna fursa ya kuzungumza na kukubaliana tuwe taifa la namna gani na hivyo kuwa na maadili ya kitaifa. Maadili hayo ndiyo yatakayokuwa kipimo cha kututathmini sisi sote kama Watanzania. Na kazi hii ni ya wote:Wazazi, viongozi, watu wa Mungu, wanasiasa na serikali.
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment