KUMEKUWA na mtindo wa chama tawala kuunda nafasi katika bunge kila mara kwa ajili ya makundi. kama vile ya wanawake wa chama, wasomi wanawake wa chama, vijana wa chama, wazee wa chama, wazazi wa chama na kadhalika. Je, haya yanayofanyika sio kulifanya bunge kwa kuwa na wabunge wasiochaguliwa na je, mbunge anayepatikana kwa namna hii anakubalika kama mwakilishi halali wa wananchi? Je, hapa hatupandi mbegu za ubaguzi kati ya vijana, wazee,
wazazi, wanawake na makundi mengine katika jamii ? Kwanini mwakilishi wa vijana asichaguliwe na vijana wote wa Tanzania kwa ujumla wao? Hali kadhalika,
Wazee, wanawake, wazazi na wengineo?
Kuna tofauti gani kati ya wabunge wanaowawakilisha wananchi na wanaowakilisha sehemu fulani ya Watanzania wakijifanya ni wawakilishi wa watu wote katika
kundi husika? Ni kwa namna gani hili linaorojesha demokrasia nchini?
Je, bunge linalokuwa na wawakilishi waliodhaminiwa na chama fulani na hawakuchaguliwa na wananchi bali wachache tu miongoni mwa makundi fulani ya kijamii
ni chachu au dekio kwa demokrasia na siasa za uwakilishi ?
Hivi tunawezaje kuboresha siasa za uwakilishi na demokrasia nchini ? Na uwakilishi huu ambao sio wa wananchi bali makundi katika jamii hauleti dhana mpya ya
uwakilishi wa makundi katika jamii ambao unahitaji bunge lake la kipekee ?
Asili ya chama tawala kuanzisha makundi maalum ndani ya chama ambayo hatimaye hutafutiwa wawakilishi wake ni jitihada sio tu za kuyapa makundi hayo nafasi
ya kulinda maslahi yao, bali pia kuongezea chama tawala isivyo halali nafasi ya kuwa na wawakilishi au wabunge ambao hawakuchaguliwa na wananchi ili
kuimarisha nafasi na nguvu yake katika bunge kama chombo cha utungaji sheria. Hili haliwezi kuwa ni kuimarisha demokrasia, bali ni kinyume chake.
Kadri miaka inavyopita ndivyo makundi yenye maslahi tofauti na yale yaliyokuwepo yanazidi kuongezekaMathalani, maslahi ya wakazi wa mkoa fulani tofauti na wakazi wa mikoa mingine sasa ni kitu kilicho dhahiri. Wakuu wa mikoa na wilaya waliopo hawawakilishi kiukweli maslahi ya wakazi wake bali yale chama husika. Hivyo, mikoa inahitaji uwakilishi mwingine mzito kuliko uliopo.
Hivi leo tuna mikoa 30 nchini lakini mikoa yote hii kutokana na mfumo uliopo inachukuliwa kwamba ni sawa kwa kila kitu na kwamba mkoa mmoja hauna maslahi tofauti na mkoa mwingine au wilaya moja haina tofauti na wilaya nyingine au tarafa moja haina tofauti na tarafa nyingine au kata moja haina tofauti na kata nyingine..
Hili sio kweli.
Hivi sasa kuna utitiri wa vyama ambavyo katika hali ya sasa havitarajii kuwa na uwakilishi wowote wa maana katika bunge lililopo. Lakini vyama hivyo ni sehemu
muhimu ya kuchota fikra kuhusu mipango na maamuzi mbalimbali ya kitaifa na ya ngazi za chini.
Zamani wote tuliitwa watumishi wa umma. Lakini hivi leo tofauti kati yetu ni kubwa. Daktari halingani na mtumishi wa ofisi ya waziri mkuu na maslahi yake ni tofauti
kabisa na mbunge achilia mbali waziri.
Hili linaashiria sasa makundi ya watumishi au wafanyakazi au wale wanaojiajiri ni mengi na sio moja. Maslahi ya maprofesa, wahadhiri, walimu, madaktari,
wahandisi, mafundi, waandishi, manesi, wanakilimo, wanateknohama,wanaufugaji, makarani, wafagiaji,wahudumu, matarishi, ofisa ubalozi, ofisa elimu,
wanamamlaka, mahakimu, wabebaji mizigo na kadhalika, hayafanani.
Wazee wenye hekima na busara wanaozidi kuongezeka toka safu za uongozi na utumishi serikalini hawana lolote muhimu la kuchangia kwa namna inayofaa katika maendeleo ya nchi zaidi ya kuitwa kuwa wageni rasmi kule na huku. Je, kina Mzee Mwinyi, Mkapa, Salmin, Warioba, Msuya, Mtey, Malecela kukiwa na bunge la pili na uwakilishi wao tutanufaika au tutapata hasara ?
Ndivyo ilivyo kwa wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wamachinga, wanamabenki, wanautalii, wauzamafuta, wachimba madini, wanaosogezwa pembeni na
wachimba madini, wawekezaji, wenyedaladala, wenyemabasi, wenyemeli, wenyendege, wanaoekezewa kwao, sekta binafsi, shule binafsi, vyuo bbinafsi na
makundi kama hayo.
Wakati makundi ya sasa yanayochomekwa na vyama vya kisiasa bungeni kama vile vijana, wanawake, wazee, wazazi, wanavyuo watachaguliwa kwa kupitia makundi ya kitaifa na siyo ya kichama kupitia wilaya na mikoa.
Kwanini mabunge mawili
Kuna umuhimu wa kutenganisha wabunge kati ya wabunge wanaochaguliwa na wananchi kwa ujumla katika jimbo na wabunge wanaochaguliwa na kundi fulani
katika jamii ili kulinda, kutetea na kuimarisha maslahi yao kitaifa.
Umuhimu wa kwanza ni kwamba, ukiwaondoa wabunge wa kuchomekwa bungeni utaliacha bunge asilia kama chombo mahsusi kwa ajili ya kuwasilisha maslahi ya wana jimbo kwa upande mmoja na yale ya kitaifa kwa upande mwingine bila kujali mtu anatoka kundi au jimbo gani. Hawa wanahitajika ili kuimarsiaha umoja wa kitaifa kwa kuepuka siasa za mwamba ngoma, ngozi kuvutia kwake.
Lakini kuwa na bunge la wawakilishi wa makundi katika jamii ambalo litaondoa mchezo wa hatari wa kuwa nao ndani ya bunge, linastahili kuundwa na wanaochaguliwa moja kwa moja na wananchi ni njia muhimu ya kuiondoa hatari ya kuvunja umoja na mshikamanowa kitaifa kwa kuwapa nguvu na mamlaka watu wasiostahili kuwa nayo kupitia ndani ya bunge asilia ambalo linastahili kuwa ni la wajumbe waliochaguliwa na wana majimbo yao.
Bunge la asili litabaki kama nilivyosema bunge la wajumbe wanaochaguliwa na wananchi. Wabunge wake watatoka kwenye majimbo. Maamuzi yao hayataathiriwa na watu wasiochaguliwa na wananchi -maana hii ni haki wanayosthaili kuwa nayo ila kwa pale bunge la pili litakapoanzishwa.
Demokrasia kwa njia yoyote ile itakayotafsiriwa hatima yake ni kwamba, kila mwananchi akiwemo yule asiye na uwakilishi wa moja kwa moja kuwa na haki na usawa mbele ya sheria, kiuwajibikaji serikali na maisha ya kijamii. Demokrasia haina maana kwamba, wanaoshinda kura basi wale, wanywe na wawe na hali na mali bora zaidi ya wengine.
Inapofikia maslahi binafsi kuangaliwa ili kulinda umoja wa kitaifa ni muhimu kuwe na bunge la pili litakalowakilisha moja kwa moja maslahi ya makundi yao.
Bunge kama hilo huundwa kwa kila kundi katika jamii. Kwa mfano, miongoni mwa wafanyakazi au watumishi yatapatikana makundi kadhaa yanayowakilisha tarafu mbalimbali, kwa mfano, wawakilishi wa madaktari, walimu , wahadhiri, wahasibu, makarani, wanamahoteli, maofisa kilimo, manesi, waandishi wa habari, wahandisi
nakadhalika.
Wakulima wanaweza wakawa na makundi yanayotokana na mazao wanayolima; wafugaji kutokana na mifugo wanayofuga; wavuvi kutokana na samaki au maliasili maji wanayovuna; wafanyabiashara kutokana na bidhaa wanayouza; wanaviwanda kutokana na bidhaa wanayozalisha; wana migogi kutokana na madini wanayochimba au ku chakata na kadhalika. Ndivyo itakavyokuwa kwa makundi mengine.
Mabunge haya mawili yatafuata utaratibu ambao hakuna jambo litakubalika endapo kuna kura nyingi za kupinga katika bunge lingine.
Kwa mfano, bunge asilia linaweza kupitisha nyongeza kwa wabunge au kwa watumishi wa umma lakini bunge la makundi katika jamii likakataa. Basi jambo hilo litabidi lirejeshwe tena kunakohusika ili lifumwe upya kwa ajili ya kuwakilisha baadaye tena katika mabunge yote mawili kwa majadiliano na muafaka utakaokuwa na manufaa kwa washikadau wanaohusika.
Kuna kauli na maamuzi mengine yanayofanyika hivi sasa na Rais au Ikulu, lakini kwa kweli maamuzi na kauli hizo zingestahili kutolewa katika mabunge haya mawili na mabaraza ya mawaziri. Badala ya rais kuwa analaumiwa kwa mambo yasiyomhusu sasa atakua na wakati zaidi wa kufanya yanayomhusu yeye kama kiongozi wa nchi na sio ya watendaji na watungaji sheria. Kwa maneno mengine, utenganishwaji majukumu ya rais, mahakama na bunge sasa kitakuwa ni kitu
chepesi zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.
Mihimili hii ya kitaifa na hususan mabunge hayo mawili yakifanya kazi zake sawasawa masuala kama mikataba mibovu; dhuluma dhidi ya makundi fulani katika
jamii; ubabe wa baadhi yetu na mambo kama hayo yanaweza kudhibitiwa vizuri zaidi.
Kuwepo kwa bunge la juu na bunge la chini sio tu kutawapa Watanzania uwakilishi mpana zaidi bali pia kutachangia upangaji, ufikiaji maamuzi, utekelezaji, udhibiti
na usimamizi bora zaidi wa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Tuesday, May 24, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment