Malaria haiwezi kutoweka kwa vyandarua vya msaada
KATIKA miaka ya 1960 ilikuwa ni jambo la kawaida kwa ofisa afya wa mji kutembelea kila kaya na kuhakikisha kuwa wakazi wa kila nyumba wako salama na imara kiafya. Mojawapo ya kazi zilizofanyika ilikuwa ni kunyunyiza dawa ya kuua mbu wa malaria.
Kwa maneno mengine, kabla na miaka michache baada ya Tanganyika kupata uhuru watumishi wa serikali ya kikoloni na serikali mpya ya Waswahili zote zilifuata utaratibu wa kuwaangamiza mbu kama njia ya kupambana na ugonjwa wa malaria.
Ninalikumbuka jambo hili vizuri kwa sababu ofisa afya aliyekuwa akija nyumbani kwetu alikuwa ni Kaburu, mzungu mwekundu, mnene mwenye malaika rangi ya njano mikononi na miguuni. Naye alikuwa ameoa mwanamke wa Kichagga na aliishi eneo la Njoro. Nadhani huyu ni yule kaburu mzuri maana alikuwa hana msamaha na yeyote aliyechangia kuhatarisha afya ya wanajamii wenzake kwa mfano kuacha madimbwi ya maji ovyo karibu na nyumba au kutupa makopo na vifuu shaghala baghala.
Nilikuwa nikimuona haraka haraka nilikimbilia ndani kuitungua kadi iliyoning'inia ukutani ili aiwekee 'tiki' kila alipohakikisha kila jambo liko kama inavyotakiwa ili kulinda afya za wakazi wa nyumbani kwetu.
Halmashauri za miji zilionyesha wakati huo sio tu dhamira bali vitendo vyenye uchungu na uchu wa kulinda afya za wakazi wake.
Kumbukumbu hii njema ya mtumishi wa serikali ambaye anajituma na anajitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa jamii haipati madhara kutokana na uzembe wa mtu mmoja au watu wachache imedumu nami hadi wa leo.
Pengine ndiyo maana wakati mradi wa kupambana na malaria kwa kutumia chandarua unaanza, niliandika makala kueleza wasiwasi wangu kuwa mkakati huu lazima ushindwe kwa sababu ulikuwa unashughulikia dalili za ugonjwa na sio chanzo.
Kwa maana, wananchi hawawezi kuvaa neti na baadhi yetu kutokana na dhiki alizo nazo Mtanzania hulala huku wanapiga mateke ovyo na kurusha mikono kiasi wao wenyewe humpelekea mbu kile anachokitaka. Achilia mbali watoto wanaolala na njaa na kuhangaika kitandani kiasi cha kudondoka chini kila usiku. Na kwa makosa au kwa usahihi nikadai kuwa mradi wa chandarua kupitia ushairi wangu ni mradi wa 'wajanja' lakini hauna nia na dhamira ya kweli ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ugonjwa wa malaria nchini.
Inavyoelekea ni kwamba kuna miaka huko nyuma katika historia yetu watu walikuwa na wito na moyo wa kuitumikia jamii bila kutegemea kupata chochote toka jamii isipokuwa mishahara yao. Watu hawakudai shukrani achilia mbali kudai rushwa. Mtu alitimiza wajibu wake na kuendelea mbele bila kutazama tena nyuma.
Hivi leo watu wa namna hiyo ni nadra. Maana mfumo wetu wa kiuchumi na kijamii umejengwa kwa namna ambayo walio wengi wanataka wapate kitu bila wao kutoa mchango wowote kwa jamii.
Kuhusu kadri wengine wanavyomenyeka na huyo 'mnyonyaji' au 'mhamishaji' kupata utajiri bila ya kuifanyia jamii lolote la maana ndivyo mtu huyo anavyoonekana mjanja na bora zaidi.
Miradi ya kupambana na ugonjwa wa malaria kama ilivyo mingi mingine inasumbuliwa pia na tatizo hili la watu kunufaika na miradi hiyo bila lolote la maana kufanyika kwa wanaokusudiwa na mradi isipokuwa kwa nafuu ya muda mfupi.
Nafuu inayosababisha mradi huo uongezewe muda, urudiwe tena au mbadala ubuniwe ili watu waendelee kula.
Wakati umefika wa kuamua, ama, tuwe tunakubali miradi inayochangia kikwelikweli kutatua matatizo ya jamii au kuikubali miradi ambayo ni 'panadol' kwa matatizo ya jamii. Mingi ya miradi tuliyonayo hivi sasa ni 'panadol' na ni ajabu kama itatufikisha mbali. Kwani siku zote njia ya muongo fupi.
Hata hivyo, isije eleweka kwamba vyandarua vyenye dawa havihitajiki. Bado vitaendelea kuhitajika lakini kinachotakiwa hapa ni kuacha kuonyesha kama vyandarua hivyo ndio jawabu kamili la kutokomeza malaria nchini.
Kwa maneno mengine, vyandarua ni kijisehemu tu cha ufumbuzi wa kupunguza na hatimaye kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini. Na kazi yake kubwa ni kupunguza maambukizi ya malaria na sio kutokomeza ugonjwa huo.
Mbu wafuatwe walipoMapambano dhidi ya malaria yanaendelea takriban kwenye kila nchi iliyo katika ukanda wa ikweta. Mikakati mbalimbali imezaa matunda tofauti. Lakini wale waliofanikiwa zaidi ni wale ambao wameamua kuwafuata mbu wanakotokea au kwenye mazalio yao na sio wale wanaongoja mbu waingie kwenye makazi ya binadamu.
Baadhi ya nchi ambazo zimeonyesha mafaniko makubwa na ambako tunaweza kujifunza mikakati mipya dhidi ya malaria ni pamoja na Cuba, Costa Rica, Venezuela, Vietnam, Zanzibar na nchi kadhaa za Amerika ya Kusini na ya kati.
Hapa Afrika kwa sababu za kisiasa na njaa kali ya wataalamu wetu miradi mingi dhidi ya mbu ni ile ambayo ya kumpa ngao mwananchi dhidi ya kuumwa na mbu na sio ile ya kumuangamiza mbu.
Na hili limelazimishwa pamoja na sauti kadhaa zilizoiona mikakati kwa sura inayostahili kuonekana toka mwanzo, kwamba ni ile isiyo na uwezo wa kutokomeza malaria bali kutuliza kwa muda na pengine baadaye kutokea mlipuko mkubwa zaidi wa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.
Mkakati wa kufuata mbu wa malaria kwenye mazalio yake ni mkakati wenye faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuangamizwa kwa mbu na wadudu wengine wanaosababisha maradhi mengine, kupunguza gharama za ujenzi, kupunguza gharama za matibabu; kupunguza idadi ya vifo, kupunguza kuathirika watu kwa dawa za kupuliza kwenye majumba na kuleta utulivu na amani katika nyumba.
Ugonjwa wa malaria una athari nyingine mbaya isiyotajwa mara kwa mara. Nayo ni ile inayofanya watu wasiweze kuwajibika ipasavyo kikazi, kifamilia na kimaisha.
Nini kifanyike?
Ninapendekeza kuwa wakati umefika kwa wote wanaohusika kwenda kujifunza toka nchi zilizoorodheshwa hapo juu. Kwa hiyo ni muhimu kwa bajeti maalumu kuandaliwa kwa ajili ya mkakati mpya wa kupambana na malaria na ikiwezekana bila kutegemea misaada toka nchi fadhili.Watanzania lazima wamiliki vita dhidi ya malaria wao wenyewe badala ya ilivyo sasa ambapo inaonekana kuwa vita hivyo vinamilikiwa na watu wa nje.
Tujipange wakati tunasubiri taarifa kwa hao watakaokwenda kujifunza mapya nchi za nje ili tuanza kuwa na mipango, taasisi na nguvu-akili na nguvu-kazi ambayo kazi yake ni kupambana na mbu kwa namna yoyote.
Kuhakikisha kuwa kila nyumba angalau mara mbili kwa mwezi inafikiwa na taasisi husika ili mbu wauawe na mazalio yao yasambaratishwe.Pawe na kadi katika kila nyumba inayoonyesha dawa na kazi nyingine zilizofanyika katika matumizi ya kuwapiga vita mbu.Kushirikiana na wale wote ambao tayari wamejikita katika mikakati ya kumuangamiza mbu kama njia kuu ya kutokemeza malaria nchini mwao.
Miradi kama hii ya kupambana na mbu kwa kutumia vyandarua au kupambana na ukimwi iangalie uwezekano wa kupunguza mishahara na marupurupu wanayopata wakubwa na watumishi. Pale watu na taasisi ikitathminiwa na kuonekana kweli imefikia malengo yake na jamii na nchi imepiga hatua katika jambo hilo ndipo watu wapewe bonasi zao.
Ieleweke kwamba, miaka ya kuona fedha za wafadhili kuwa sio hela yenye uchungu imekwishapita. Ni lazima tuionee uchungu fedha ya wafadhili kama tunavyoionea uchungu fedha yetu.
Ninakumbuka kutokana na ukubwa wa misaada ya malaria inayotoka nje mara ya kwanza nilipoandika kuonya kwamba dawa sio chandarua bali kuangamiza mazalia ya mbu nilichukiwa na wakubwa wote toka chini hadi juu. Ninaami kwenye hili historia daima itkuwa upande wangu.
Neti ni mbwembwe tu na kitega uchumi cha wachache, lakini mwisho wa siku ili mbu wasiwe kero hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili ni kuangamiza mazalia yao pale Jangwani. Kama kipanya alivyosema,'labda pia tuwe tunapika na kupakua tukiwa ndani ya chandalua' ndio Tanzania bila malaria itawezekana.
Hili ni muhimu katika miaka hii ambayo imegundulika kuwa nchi zisizopata misaada au zinazopata misaada kidogo ndizo zinazoendelea kuliko zinazopata misaada mikubwa. Wafadhili wanatafakari na sisi tutafakari !
Saturday, May 7, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment