Monday, May 23, 2011

Mahakama ya Rufaa imethibitisha katiba mpya inahitajika

WANAOTULETEA maafa, balaa na matatizo na hata umwagaji damu Afrika aghalabu ni wale wanaotaka kutawala jinsi wanavyotaka na ambao hutaka kutumia siasa badala ya katiba na sheria za nchi kutawala.

Wakati wananchi wa Kenya karibuni watapigia kura pendekezo la Katiba mpya nchini mwao, Tanzania iliyoitangulia Kenya katika kukubali demokrasia ya kisiasa

haijaona umuhimu wa kuwa na katiba mpya licha ya mapungufu mengi ambayo watu wengi nikiwemo mimi tumekwishaonesha mapungufu yake. Kwa kifupi katiba

tuliyo nayo haitofautiani na kutumia taipureta katika karne ya kompyuta.

Hata hivyo, masuala kadhaa yaliyozuka ndani na nje ya nchi hivi sasa yanaashiria kuwa kukataa katiba mpya nchini Tanzania ni jambo ambalo linakaribia

kupoteza sababu na mantiki katika kila nyanja ya maisha, siasa na kazi.

Mathalani, kadhia ya mgombea huru na jinsi mhimili wa sheria ulivyoterereka na kukwepa wajibu wake umeonesha wazi kwamba bila ya kuwa na katiba mpya

jambo hili litafanywa kwa mizengwe na matakwa ya chama tawala na sio kisheria wala kidemokrasia. Hii ina inamaanisha kuwa ipo hatari kubwa ya nchi kuendelea

kuongozwa kwa haja na matakwa ya mtu au watu, badala ya kuwa na mifumo hai inayofanya kazi bila kuingiliwa na utashi wa mtu katika maeneo mbalimbali ya

utawala na uongozi wa nchi.

Katiba iliyopo sasa inakubali na kuamini katika uhuru usiokuwa na kikomo ndani ya sheria za nchi. Wanachokitaka wengine ni kuweka mipaka kwa uhuru wa

Mtanzania, hususan ule wa kuchagua na kuchaguliwa ndani au nje ya chama cha kisiasa.

Tukio lingine ni lile la kupitishwa kwa itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki. Inaelekea Tanzania imekutwa katika hali ya kuwa bado imeshusha kaptula yake

na inataka faragha ya muda kujiweka sawa. Badala ya mambo haya, hata kufanyika kwa msaada wa ushauri na utafiti wa wasomi wetu, wataalamu na mabingwa

wa nyanja mbalimbali; inaelekea yanafanyika bado kisiasa na matakwa ya watu fulani ikidhihirisha kuwa hata tukipewa miaka 20 hatutaweza kubadili chochote.

Kusahihisha jambo hili ni lazima pawe na katiba mpya na itakayobainisha waziwazi ni kwa kiasi gani nchi hii itatoa ruhusa ya kumegua uhuru wake katika kutafuta

umoja wa Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla. Ni lazima tuwe na katiba inayoona mbali kwa miaka hata zaidi ya hamsini. Sio katiba iliyoishia katika uhuru

na Azimio la Arusha.
Kuna wanaoamini kwamba, Tanzania haiwezi kuendelea kama kila kitu kitakuwa kinaamuliwa kutoka Dar es salaam. Jamaa hao wanaamini ipo haja ya kuwa na

mikoa huru kiuchumi na kijamii kama tunataka kuendelea kwa uhakika na haraka zaidi. Tishio kwa umoja kupitia ukabila hivi sasa sio kubwa kama tishio la ukabila

wa kichama. Je, uziri wa jambo hili haulifanyi kuwa katika katiba mpya ?
Wakati Zanzibar ina mahakama ya Kadhi kama ilivyo kwa Kenya na Uganda na suala hili limo katika Katiba ya nchi zao ambazo ukitoa visiwa vya Zanzibar, ni nchi

zenye Wakiristo wengi zaidi kuliko Waislamu. Chama tawala hapa nchini kimefikia uamuzi wa kukataa mahakama ya kadhi isiwemo katika katiba kinyemela.

Jambo linaloacha ufa wa kutisha siku zijazo za Waislamu wenye siasa kali kwenda njia nzima na kuwa na shariya, maana hawakujumlishwa na eti kwa kisingizio

cha kuogopa gharama ambazo zinatumika kwa wananchi wale wale wanaochangia hazina ya taifa kwa kodi na matumizi yao mbalimbali. Uamuzi huu unakuwa

sio tu undumilakuwili bali pia ni wenye kuning'inia kwa kamba ya shinikizo za nje na hauashirii mahusiano mema kati ya imani zetu za kidini katika miaka ijayo.

Sehemu kubwa ya Waislamu hawaitambui BAKWATA, lakini kwa sababu moja au nyingine serikali bado inashinikiza kuwa BAKWATA peke yake ndio mwakilishi

halali wa Waislamu. Hili si jambo njema, ni lazima pawepo na katiba mpya ili kudhihirisha wazi uhuru wa kila dini kujiundia wenyewe vyombo vya kuwawakilisha

katika masuala mbalimbali. Taasisi inayoonekana kufadhiliwa na kulindwa na serikali haiwezi kukubalika kuwa mwakilishi halali wa wanaimani wanaohusika.
Kuna wanaoamini kwamba, vyombo vya habari vya serikali ni mzigo kwa walipa kodi usio wa lazima. Je, hili halionyeshi kuwa kuna haja katiba mpya ambayo

pamoja na mambo mengine itaangalia pia nini uwe uhusiano wa vyombo vya habari na serikali; vyombo na vyama vya siasa na vyombo hivyo na wananchi ? Kwa

wengi, vyombo hivi kama vilivyo vingi vinginevyo vinaonekana ni mianya kwa baadhi ya watu na taasisi kula fedha za umma bila ya wachungaji kupiga mayowe na

wakati mwingine bila kujua.

Dai mojawapo kubwa la vyama mbadala nchini ni kuwepo kwa tume huru. Tume ambayo haitaegemea upande wowote na hivyo kusimamia chaguzi huru. Je, ni

kwa kiasi gani hili linaweza kukamilika bila ya kuwa na katiba mpya?

Tangu tupate uhuru azma moja yetu kubwa ilikuwa ni kupunguza tofauti kati ya miji na vijiji, wakulima na wafanyakazi, matajiri na maskini. Je, hili limefanikiwa kwa

kiasi gani? Hivi ubaguzi kati ya miji na vijiji inaweza kuondoka bila ya kuwepo katiba mpya ?

Kuna watu wa makabila mbalimbali nchini ambao wanaamini kwamba, redio zingelikuwa zinatangaza kwa lugha za makabila yao sio tu wangelihabarika, kuelimika

na kustareheka zaidi, lakini mapambano yao ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yangelikuwa rahisi zaidi. Lakini sheria na katiba iliyopo havielekei kuoana katika

kauli za kama iwepo au isiwepo ruhusa. Isitoshe wanasiasa wa kale lakini wasiothamini utu na utamaduni wetu hawalikubali hili. Wanaleta hofu ya bure ambayo

inastahili sasa kuwa dhidi ya wanasiasa wenye ubaguzi wa kichama nchini. Nchi kwa hiyo inatawaliwa kwa uoga badala ya hoja za msingi zenye mantiki

inayokubalika.
Habari za mama na mabinti wetu kujifungua barabarani na chini ya miti haziachi kusikika toka huku na kule. Madaktari na manesi wetu wanalaumiwa kwa roho

mbaya, lakini hili linaanzia kwenye mishahara mibaya. Je, kweli bado hatujaona haja kuwa na kipengele ndani ya katiba mpya kinachozungumzia kwa kina ni nini

iwe sera ya afya kwa wananchi wetu-wenye nacho na wasio nacho daima dawamu? Haisemi lolote jinsi ya kuboresha hospitali hizo ili ziweze kutibu wanaopelekwa

nje kutibiwa na wagonjwa kutoka nje na nafuu inayopatikana iwe ni ile itakayoweza kutoa tiba ya bure kwa watu masikini.
Kuna suala la usafi, mipango miji na utunzaji mazingira mijini na vijijini ambalo, hata hapa Dar es Salaam wanapoishi wakubwa linaelekea sio tu kwamba halina

mwenyewe, bali hakuna viwango vya kumzawadia mtu zabuni ya kusafisha mji. Matokeo ya hili ni kuwa msafisha mji na vyombo wanalitia jiji uchafu na sura mbaya

zaidi. Je, jiji halistahili kusahihishwa na katiba mpya?

Suala la madini na migodi, pamoja na kuwepo na sera mpya bado linastahili kuingizwa ndani ya katiba kwa namna ambayo watu na madini yetu yataonekana

kuwa na thamani zaidi kuliko wawekezaji na mitambo yao na vizawadi vya barabara, shule na zahanati wanavyotudanganya navyo. Zanzibar inadai mafuta ni yake

wakubwa bara wanasema mafuta ni yetu. Tumfuate nani? Dawa si katiba mpya?

Kuna wanaoamini kuwa mashirika kama yale ya hifadhi za jamii yanastahili kwa kiasi kikubwa kumilikiwa na wanachama wenyewe na sio na serikali na wanasiasa.

Wanadai umilikaji wa sasa hivi unawanyonya na kuwapunja wanachama kwa njia nyingi. Makato ya mwanachama yakigeuzwa ni hisa ndani ya mashirika hayo

wanachama watafaidika zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. La sivyo, basi pawe na uhuru wa kuanzisha hifadhi huru za jamii kwa kila tarafu.

Kuna wanaoamini, Tanzania yenye viongozi wanaotaka kweli kuwaondoa wananchi wake toka kwenye umaskini ina uwezo kwa kutumia rasilimali zake yenyewe

kujengea kila familia nchini, mjini na vijijini angalau nyumba ya vyumba viwili. Jambo hili sio tu litatengeneza ajira kubwa na pato kubwa kwa nchi na watu wake bali

pia litaondosha aibu ya kila Mtanzania kuwa na mradi wa kujenga nyumba ya kuishi badala ya kujenga biashara au kiwanda.

No comments:

Post a Comment