Monday, May 23, 2011

Dar kuwa bustani nzuri, ikiwa...

KATIKA sehemu mbalimbali za jiji hili kuna vijana walioanzisha biashara ya kuotesha vitalu vya miti na maua. Kwa kiasi fulani vijana hawa wanatoa huduma muhimu kwa wakazi wa jiji, sio tu kwa bustani zao mjini bali pia kwa mashamba yao viungani mwake.

Inaelekea vijana hawa wanafahamu fika kwamba, jiji linastahili kuwa na miti na mandhari ya jiji inaweza kuboreshwa kwa kuwa na maua ya aina mbalimbali yanayopandwa katika sehemu mbalimbali za jiji. Kwa upande wake jiji linaweza kuwa na habari na hili lakini pengine halioni umuhimu wake kwa sasa au linakwamishwa na upungufu wa rasilimali muhimu kama watu na vifaa.

Tatizo ni kuwa jiji halionekani kwamba, limewaona vijana hawa kama ni sehemu ya ufumbuzi wa tatizo la jiji kukosa miti ya kutosha na kukosa bustani za maua ambazo zingelifanya jiji kwa Kiswahili cha siku hizi litakate zaidi.

Ninaamini kutokana na makala haya tutawachochea viongozi wa jiji kuangalia upya uhusiano wao na vijana wenye vitalu vya maua na miti jijini na wao wakaweza kuweka mkakati moto wa kuhakikisha kuwa akili na nguvu kazi ya vijana hawa inatumika kulipa jiji mandhari mpya ambayo ikichanganywa na majengo mapya italifanya kuwa jipya na lenye mvuto mkubwa zaidi kwa watu wa ndani na wa nje.

Vijana hao wana miche ya miti ya aina mbalimbali ikiwemo ile ya upendezeshaji, mbao na matunda.

Kazi ya vijana hao, hadi sasa watu wengi wanaitazama kwa pua fupi; kwa maana wanaiona kama ni ya kimachinga na ya kuwapatia tu mapato vijana hao wala haiwezi kuwa na mchango wowote wa maana kwa jiji na watu wake na hata wageni wanaokuja kutembelea nchi yetu pia.

Wakati huo huo, ni utamaduni wa Watanzania kupanda miti kwenye siku wanayoita ya upandaji miti, bila kuwa na mpango wa nani ataupa maji na kuutunza mpaka ukue.

Katika hali kama hii miti mingi na mimea mingine inayopandwa hapa jijini huwa inakufa baada ya miezi michache kama sio wiki. Kiasili mimea ni dhaifu sana wakati ikiwa michanga. Inapokosa maji na utunzaji haikawii kunyauka na kufa. Kutokana na ukweli huu kitendo chochote cha kupanda miti na maua bila kufikiria maji ya kunyweshea na mbolea ya kurutubishia zitatoka wapi na nani ataitunza mimea hiyo kwa karibu ni kitendo kinachoweza kuitwa kwa lugha nyepesi utoto kama sio ujinga kwa wasiojua mtiririko wa shughuli za kilimo.
Ninaamini kwamba, akili na nguvu za vijana wanaoanzisha vitalu vyao vya maua na miti zikikutanishwa na akili za wananchi na utambuzi wa miti ili kukua inahitaji maji na kutunzwa tunaweza kuwa na MRADI MKUBWA WA KUGEUZA SURA ZA JIJI KUU LA KIBIASHARA LA TANZANIA.

Kuna mambo ambayo tunaweza kudai yana gharama kubwa na hatuwezi kuyafanya sisi wenyewe. Hili la kupanda miti na maua sio moja wapo. Ni aibu sisi Watanzania kama tunashindwa kugeuza mitaa, makaburi na bustani zetu zikawa na hadhi za kimataifa na kutuondolea aibu tunayoipata sasa kwa sehemu hizo kutokuwepo au kwa zile zilizokuwepo kuonekana kama takataka.

Kinachotakiwa hapa ni kuwa na mpango wa jiji wa kubadili mandhari yake ili uwe na miti na maua ya kutosha ambayo sio tu kutachangia kubadilisha uzuri wa jiji, lakini pia katika kupunguza joto linalorindima hasa katika kipindi cha Oktoba hadi Februari.

Huko Ubelgiji na Uholanzi kuna miji ambayo imejengeka kutokana na kuwa na miti, vijito au mifereji na maua yaliyopandwa kimpango. Maua na miti hiyo imekua ni kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na wa nje katika nchi husika. Hili sio jambo la gharama sana na nina hakika kwamba, wakazi wa Dar es salaam wakihamasishwa ipasavyo wanaweza kufanya jambo hili na Dar nayo ikapendeza na kuwavutia wengi.

Utunzaji huu bora wa mazingira umechangia kwa kiasi kikubwa kuijenga miji kama Brugge, Hague na Amsterdam katika biashara ya utalii na mikutano ya kimataifa.

Aidha ni muhimu kwa zoezi la kuwabadili watu fikra kufanyika ili kujenga utamaduni wa kuthamini miti, maua na mandhari iliyo njema.
Kwa hivi sasa Watanzania wengi inaelekea wanaamini kuwa hawastahili miti, maua wala mandhari bora maana ni kama jambo lisilowezekana kwao. Hivyo panahitajika kampeni ya nguvu sio tu kuhusu usafi bali pia itakayobainisha waziwazi kwamba jiji lenye miti ni bora kuliko lisilo na miti; jiji lenye bustani na maua nalo kadhalika lina thamani zaidi kuliko kinyume cha hivyo na kwamba jiji lenye misitu ya kupanda wenyewe linaweza kabisa kuibadili hali yetu ya hewa ikawa bora kwa maana yenye ubaridi zaidi kuliko inavyokuwa hivi leo.
Ninachosema ni kwamba, Jiji la Dar es salaam liwatazame vijana wenye vitalu vya maua na miti kwa jicho jipya. Kisha waweke mkakati wa kugeuza mandhari kwa kuwatumia vijana hao.

Laiti ningelikuwa ninaendesha mradi huu ningeliamua mambo yafuatayo.

Ningeliigawa Dar es salaam katika mitaa au maeneo ya kimandhari kadhaa. Ningeingia mkataba na wenye vitalu vya miti na maua.

Kazi yao kubwa ingelikuwa kwanza kuhakikisha miti iliyopo inapata maji na mbolea na kutunzwa kila siku. Kiasi kwamba jiji linakuwa na hakika ya angalau asilimia kubwa kidogo kuliko ilivyo sasa kuwa miti yote inayopandwa katika siku za kawaida na ile ya upandaji miti na viongozi na wageni waalikwa inapona, kukua na kutimiza kazi ya kupandwa kwake.

Pili kila palipokuwa bustani au panapostahili kuwa na maua pataangaliwa na vijana hawa kwa mkataba maalumu utakaolenga kuwanufaisha vijana hao kimapato na kulinufaisha jiji kimandhari.

Makampuni mbalimbali yaliyopo jijini yataombwa kushirikiana na kampuni ndogo ndogo za vijana hawa ili pia mazingira ya kila sehemu yaweze kupendezeshwa na kuwa na mvuto kwa wapita njia.

Changamoto kubwa itakuwa ni kuhakikisha kupatikana kwa maji ya kutosha wakati wote ikiwa ni yale ya DAWASCO au ya visima vitakavyowekwa kimkakati katika maeneo yote ya jiji.

Huko kando ya bahari pamoja na kuweka zege vijana hawa watachangia pia kuhakikisha kuna miti na maua ambayo kwa namna moja au nyingine vitachangia kupunguza kasi ya bahari kula pwani ya jiji.

Haya yakienda sambamba na ujenzi wa bustani za kupumzikia na ujenzi wa viwanja vya michezo kwa watoto na wakubwa bila shaka mandhari ya jiji inaweza ikawa na mvuto mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Na kutokana na hilo, jiji likapanda chati kama kivutio kikubwa cha watalii katika pwani ya Afrika Mashariki.

Aidha uimarishaji wa barabara na usafiri ili kufikia mashamba ya wanyama (zoos) na bustani za nyoka na vivutio vingine nje ya jiji utasaidia sana kuliuza jiji kwa watalii.

Pembezoni mwa mji vijana hao watapewa kazi ya kuotesha misitu itakayochangia kuifanya hali ya hewa ya Dar es salaam kuwa baridi na tulivu zaidi kuliko ilivyo sasa na kulihakikishia jiji na vitongoji vyake kupata sio tu mvua za kutosha bali pia kivuli na mahitaji yake mengine ya kinishati hapo baadaye kwa gharama nafuu zaidi bila kuharibu mazingira moja kwa moja.

Yote haya nina uhakika yanaweza kufanikiwa kama kutakuwa na mpango wa kimkakati wa jiji kuboresha mazingira na mandhari yake. Ni lazima ijulikane wakazi wa jiji wanataka na wanastahili jiji litakaloonekana katika hali gani kufikia miaka 3 au 5 kutoka sasa. Jiji liwe na miti mingapi kulingana na idadi ya watu wake, bustani ngapi za kupumzikia, misitu mingapi ya kutembelea na kufanyia mazoezi badala ya watu kufanya mazoezi katika hewa chafu ya jiji kama ilivyo hivi leo na mtiririko wa maji na upatikanaji wa mambo mengine muhimu utakuwa vipi.

Haiwezekani yote kufanyika kwa pamoja, lakini hili la kuwakabidhi vijana walio na vitalu na miti kazi ya kuhakikisha jiji linakuwa la kijani ni jambo linaloweza kufanyika mara moja. Maana sio lazima jiji litumie fedha yake. Jiji linaweza kuhamasisha makampuni mbalimbali kuchangia hili kwa kuwapa motisha ya kutangaza katika maeneo itakayokuwa imepandwa miti au kwenye bustani au kiwanja cha michezo na kadhalika.

Ieleweke kwamba, heshima ya kampuni yoyote katika nchi yoyote ile hutokana na mchango wake katika kuhakikisha mji kampuni iliko unakuwa wa kisasa na unapata huduma na mandhari za kimataifa.

No comments:

Post a Comment