KAMPUNI zinazoheshimika na kuonekana zinatimiza wajibu wao kijamii pamoja na mambo mengine, pale zinapowapatia wananchi katika nchi husika fursa ya kununua hisa zake kwa asilimia fulani.Kampuni hizi zinatambua fika kwamba, ingawa ni wao waliobeba jukumu la kubuni na kuanzisha shughuli husika, lakini lazima wakati ukifika wakubali kuwa wananchi nao wana haki ya kuwa wamiliki wa kile walichokianzisha wao.
Huku ni kuona mbali na mbele na hasa wale wanaotambua kwamba, kufanikiwa kwa shughuli moja ni mwanzo wa kufikiria kama sio kuanzisha nyingine.Hii ina maana kwamba, kampuni inaweza kuanzishwa kwa hisa za mtu mmoja au wachache lakini mwisho wa siku waanzilishi hukubali kuuza asilimia fulani ya hisa zao kwa watu wengine walio na imani na aina ya biashara inayofanyika au kampuni yenyewe au waanzilishi wake au mameneja wake na hivyo kuwapunguzia waanzishi hatari ya kubeba hisa zote wao wenyewe.
Aidha, hili hufanyika pia kudhihirisha kuwa waanzilishi hawana uchu, uroho na ulafi wa kutaka wao pekee yao wanufaike na matunda ya kile walichokianzisha wao.Mradi mamlaka za mitaji na masoko ya hisa yanafanya kazi zao inavyopasa na hakuna uwekezaji au shughuli danganyifu au bomu inapitishwa kuwa ni halali, faidifu na zenye viongozi waadilifu wenye rekodi ya kufanikisha mambo kampuni yoyote haitokuwa inawatendewa wananchi wa nchi husika haki, kama isipowagawiwa wale wanaotaka sehemu za hisa zake. Ili mradi gharama zake zote za uwekezaji zimekwisharudi.
Mathalni, heshima na uwezo wa kampuni maarufu Afrika Mashariki na ya Kati kama sio Afrika nzima ya Nation Media Group imepatikana kwa kiasi kikubwa kutokana na kampuni hiyo kutomiliki hisa zake zote.
Hisa za kampuni hii zinauzwa na kununuliwa kila siku ya kazi katika soko la mitaji la Nairobi (Nairobi Stock Exchange).Ni vizuri kwa wamiliki wa makampuni kutokuwa na ukiritimba na umimi wa kupita kiasi katika suala la uchangiaji mtaji wa kampuni yoyote ile.
Maana kwa hakika kazi kubwa katika masuala ya kiuchumi sio tu kuanzisha na kuendeleza ulichokianzisha, bali pia kuweza kudumisha kama sio kuongeza imani ya walaji kwa kampuni au biashara unayoifanya.Uchangiaji mtaji katika nchi inayoendelea kama yetu ni muhimu sana katika kukuza uchumi, jambo ambalo huongeza kipato kwa karibu sekta zote katika nchi. Isitoshe watu wenye uwezo wa kusimamia na kuendesha miradi ya kiuchumi kwa ufanisi na ufanifu katika jamii yoyote sio wengi sana. Panapokuwa na uchangiaji mtaji ziada inayopatikana huweza kutumika kuanzisha kampuni au mradi mwingine ambao utanufaika na uongozi na usimamizi wa mameneja na wanyapara walewale na hivyo kuhakikisha mafanikio yake kama ile ya miradi iliyopo.
Upo uwezekano mkubwa pia kwa kampuni inayokubali kuuza hisa zake kwa wananchi kuwa kampuni ya kimataifa kuliko kampuni ambayo hisa zake zinamilikiwa na mtu mmoja au wachache tu. Matatizo mengi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayotokea sasa Afrika yanaweza kulaumiwa kuwa kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mfumo unaowapendelea vizito na vigogo tu katika kupata na kukuza mitaji yao.
Laiti isingelikuwa 'uroho wa teni pasenti wa viongozi wetu' hivi sasa nchi hii ingelikuwa imezinduka na kutambua kwamba ardhi, mali asili, rasilimali nyinginezo, watu na vile tulivyovirithi kama watu na nchi katika taifa letu havijapewa THAMANI halisi katika mustakabali wa maendeleo yetu. Hili lingelijulikana, wananchi walioondolewa Barricks ilikowekezwa leo wasingelikuwa masikini tena; wananchi jirani na Mbuga zetu za wanyama wasingelikuwa wanaathirika na njaa na ukame; na wafanyakazi katika viwanda na mahoteli yetu wasingelilalamika ukata kila siku. Tatizo ni kuwa msimamizi mkuu, yaani, Serikali, kaenda likizo au kasepa mbele ya wawekezaji na tiara ya wasionacho inakwenda arijojo kila kukichwa. Ingawa wakubwa, asubuhi na mapema walishatoka na teni pasenti yao na sasa wala upepo wa Bahari ya Hindi huko Mikocheni, Masaki, Kawe na Msasani.
Mathalani, katika baadhi ya nchi zetu wawekezaji toka nje na ndani ya nchi wakati mwingine ni lazima wahonge aukuwakubali wanasiasa au mangimeza wa serikali kama sio wake na watoto wa makundi hayo ya watu kuwa wanahisa katika kampuni wanazoanzisha kabla hawajaruhusiwa kuwa na kampuni au biashara hapa nchini.
Kutokana na hili unakuta ni wale tu ambao tayari walikwishakuwa na mitaji au ambao wamo katika chama tawala ndio wanaopata urahisi wa kuwa na mitaji. Miaka inapita na wananchi wengine wanaona kwamba kuna kundi fulani kama vile wale nguruwe katika kitabuc ha SHAMBA LA WANYAMA ndio wanaofaidi maisha peke yao. Matokeo yake vijana wanachoka kusubiri na nchi inaweza kusambaratishwa kwa vitetndo vinavyodhamiria kurekebisha hali hii ikiwemo uwezekano wa kuwa na harakati za uamsho kama zinazotokea huko Misri na Maghreb na kwingineko Uarabuni. Tofauti yetu ni kuwa sisi ni kwa sababu za umaskini na ukapa unaokithiri siku hadi siku, wakati wenzetu wanakula na kushiba lakini wanataka demokrasia. Kwa hiyo kushiba na demokrasia ni kurwa na Doto na hili tusilisahau. Na mtaji wa kuwaacha wananchi waendelee kulowa katika umaskini si mtaji wa uhakika, ni mtaji kivuli na lolote linaweza kutokea.
Ni jambo la kheri basi kwa walioko madarakani kuondoa hili na kuanza kuufumua mfumo uliopo ili kuruhusu mgawanyo mpya rasilimali za nchi ili kuhakikisha umoja na amani nchini vinakuwa ni vitu vya uhakika kivitendo na sio kwa maneno tu.Katika mfumo wa soko huru ambako upo uwezekano mkubwa wa kampuni binafsi kuwa nyingi na kubwa zaidi kuliko ya serikali na uwajibikaji kijamii kwa kampuni kama hizo, kwanza na juu ya yote ni kuhakikisha kuwa hayelei ukiritimba wa watu wachache kumiliki hisa za makampuni yao. Kwa maneno mengine,kampuni kubwa na zinazotoa huduma kwa sehemu kubwa ya jamii yanawajibika kuuza asilimia fulani ya hisa zao kwa walaji wao na hivyo kuwafanya baadhi ya walaji wakubwa kwa wadogo kuwa pia ni wamiliki wa kampuni husika.Kwa mantiki hii kampuni kama vile zile za simu -TTCL, Airtel, Tiggo, Zantel, Vodacom, Sasatel na kadhalika; kampuni za uchimaji madini na mafuta; kampuni za usafirishaji wa angani, majini na nchi kavu; mashamba makubwa ya kilimo na mifugo; uvuvi mkubwa baharini; miradi ya elimu kupitia shule na vyuo; hospitali na miradi ya nishati na maji zitakuwa zinawajibika ipasavyo kijamii kama zitafikiria uwezekano wa kuuza angalau asilimia 40 za hisa zao kwa wananchi kupitia soko la mtaji la Tanzania au Afrika Mashariki.
Hapa hakuna suala la kupenda au kutokupenda kuuza hisa kwa wananchi. Hili lazima liwe ni shurti letu Watanzania. Vinginevyo, tutaamini makampuni hayo ama yanamilikiwa na viongozi wa serikali au makuwadi wao.
Ikiwa sehemu ya hisa itakuwa imeuzwa kwa wananchi basi haitakuwa rahisi kwa mashirika haya ya simu za mkononi kuuzwa kila muda wa msamaha wa kodi unapokwisha. Na pengine tutaanza kuwa na kampuni za simu za mkononi za kudumu zaidi kuliko hizi zinazobadili majina kila baada ya miak 3.
Hisa hizo ndogo ndogo ni muhimu sana katika kuimarisha kampuni machoni mwa wadau mbalimbali; zikiwemo benki, wafadhili na taasisi za fedha za kitaifa na kimataifa. Hili linakuwa muhimu zaidi wakati nchi wafadhili zinapoofikiria kusaidia nchi zetu zaidi kupitia shughuli za kiuchumi na sio katika bajeti ya serikali.Jambo hili linaongeza uwazi na hivyo kuondoa baadhi ya kampuni kuendelea kudanganya mamlaka ya ukusanyaji kodi na serikali kwamba, bado hawapati faida katika shughuli wanazozifanya.Jambo hili kwa kuwa pia linatoa fursa sawa kwa wananchi wa kawaida kama ilivyo kwa vigogo na vizito kuwekeza katika kampuni kubwa na madogo kunaepusha ufisadi ambao pia unakua kutokana na kuwepo kwa kampuni mengi yenye mwanahisa mmoja au wachache ambao wanatumia aina mbalimbali za udanganyifu; hivyo kuipunguzia haziana uwezo wake wa kugharamia mipango na miradi mbalimbali ya kimaendeleo nchini.
Ni rahisi kuona pia kampuni zenyewe zinajijengea heshima ya kipekee kwa jamii husika, maana wananchi wataziona kuwa haziwakamua tu ili zifaidike zenyewe, lakini pia zinataka kuirudishia jamii kile kinachostahili kwa maendeleo ya wengi.Faida nyingine za kampuni kubwa na zinazotoa huduma au kuwagusa wananchi wengi kwa wakati mmoja kutoa sehemu ya hisa zao kwa walaji ni pamoja na kusaidia kupiga vita umasikini, kupatia umma elimu ya uwezekezaji na ujasiriamali na kukuza na kupanua mzunguko wa fedhaa pamoja na kukuza uwezo wa nchi kimtaji.Ninaamini kama serikali na mashirika husika yanashindwa kuona umuhimu wa shirika kuwepo kwenye soko la hisa na uuzwaji na ununuzi wa baadhi ya hisa zake wakati wowote, basi kuna uziwi na upofu wa namna fulani katika kuoanisha sera ya kupambana na umasikini, uwekezaji na mchango wa wazawa katika maendeleo ya nchi yao.
Kampuni za simu za mkononi zina njia nyingi za kutengeneza fedha kwa wingi kiasi ambacho ninaamini hata TRA bado hawajaona hili kwa undani. Uungwana kwa wenye makampuni haya ni kuwa wakweli lakini na TRA nayo isikae mkao wa kuwala sana au kuwafilisi. Wenye makampuni hayo pia waache kuwafanya Watanzania ni watoto kwa kuwadanganya kwa michezo ya bahati nasibu na badala yake wakae mkao wa kuanza kuwauzia wananchi hisa bila upendeleo au uonevu.
Njia mojawapo ya kuvisadia vijiji masikini ni kuweka minara yao pale badala ya kuwalipa matapeli wanaokwenda kununua ardhi sawa na bure na kuipima na kisha kuwauzia au kuwkodishia wenye simu kwa bei nono kabisa. Wengi wanadai wamedhulumiwa kwa namna hii.
Aidha kampuni au shirika lolote linaloamua kukaribisha ununuzi wa baadhi ya hisa zake na wananchi wa husika; kwa maoni yangu itakuwa inajenga msingi imara wa kuendelea kuwepo kwake hapa nchini kwa faida yake na faida ya nchi na wananchi wa nchi mwenyeji. Watakuwa sio tu wanajiasilisha na nchi na watu wake bali pia wanajikuribisha nao na kujenga uhusiano utakaohakikisha ufanisi na ufanifu mkubwa siku zijazo.Vinginevyo kwa makampuni machoyo na yenye ubinafsi wa kupindukia yatajikuta na upinzani mdogo, lakini unaoashiria kukua ulioanizishwa na michakato na miradi ya ujasiriamali jamii.
Michakato na miradi ya ujasiriamali jamii ni jibu la wananchi kwa kampuni zisizotaka kutoa hisa zao kwa wananchi kwani hudhamiria kuanzisha biashara au mradi kama huo wa wachoyo ili wao na wafaidike kwa kuwa watoa huduma na wakati huo huo watumiaji wa huduma hiyo.
KAMWE, hata hivyo mashirika hayo hayawezi kutudanganya sisi ni washirika wao na wanatujali bila ya sisi kuwa wamiliki angalau kidunchu wa makampuni hayo ya simu za mikononi na mengine kama hayo.
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment