Monday, May 23, 2011

Usimamizi, udhibiti wa sekta binafsi katika elimu

VYUO na shule binafsi vina sehemu muhimu sana katika kuchangia kumjenga mtoto wa Kitanzania kuwa raia aliyeelimika, aliyejijua na kutambua yuko duniani kwa ajili ya nini na nani, aliyestaarabika na anayetambua wajibu wake katika jamii.

Hakuna mzazi asiyetambua katika miaka hii umuhimu wa mwanawe kupata elimu nzuri kwa faida sio tu ya mtoto lakini pia ya wazazi hapo baadaye wanapokuwa wazee na hawana njia ya kujiingizia kipato cha kujitosheleza tena.

Kwa sababu hii, wazazi wengi wanakuwa tayari kujinyima wao ili watoto wao wapate elimu iliyo bora kabisa kwa faida yao ya baadaye.

Hata hivyo, baadhi ya vyuo na shule kutokana pengine na kutokuwepo na chombo cha kudhibiti maamuzi na utekelezaji wao katika uendeshaji shughuli za kutoa huduma hii muhimu ya elimu sasa zimeanza kuwa kero kwa baadhi ya wazazi.

Vyuo na shule hizi ambazo zimeanza kuwa kero ni zile ambazo ada zao ukilinganisha na wenzao zimekuwa zikipanda kila mwaka bila kuwepo na sababu muhimu kwa wao kufanya hivyo.

Ni katika muktadha huu tunapenda kuungana na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine ambao wameanza kuzungumzia umuhimu wa kuwa na bodi za kusimamia na kudhibiti vyuo na shule binafsi ili visiwe vinamkomoa mzazi bila sababu ya msingi.

Kubwa zaidi ambalo linazungumziwa ni haja ya kuhakikisha ada zinazotozwa sio kubwa kupita kiasi. Lakini ada ni jambo moja tu katika msururu wa mambo mengine ambayo yanastahili pia kushughulikiwa na ambayo yanachangia katika haja ya kuwepo na bodi maalum ya kusimamia na kudhibiti mwenendo wa mambo katika utoaji elimu kupitia sekta binafsi.

Masuala ambayo kwa haraka haraka naweza kuyataja na pengine baadaye watu wengine kuyaongeza ni pamoja na masuala ya uongozi katika sekta binafsi; hadhi na viwango vya majengo ya vyuo na shule; motisha na ubora wa rasilimali watu; upatikanaji walimu katika kila somo, ubora wa chakula na malazi, elimu ya kujitegemea, michezo, muziki na sanaa, elimu nje ya darasa, nafasi ya dini
vyuoni na shuleni, nafasi ya siasa katika vyuo na shule, mapato na matumizi katika taasisi, udhibiti wa gharama, maofisa serikali na mtazamo wao kwa wahitimu wa vyuo na shule binafsi na umuhimu wa shule na vyuo binafsi kupata ruzuku toka serikalini kama vile baadhi ya shule za kidini zinavyopata.

Uongozi katika sekta binafsi ya elimu na hususan katika shule za msingi na sekondari aghalabu hauna usimamizi na udhibiti kabisa. Kutokana na hili zipo shule nyingi za binafsi ambazo wakuu wake wa shule hawana taaluma ya elimu wala kiwango cha elimu katika masuala ya menejimenti kwa kiwango cha kutosha kuwa mameneja wa shule.

Ikumbukwe mkuu wa shule hana tofauti na meneja katika sekta nyingine. Upo ushahidi wa kutosha kuwa wakati mwingine mkuu wa shule anakuwa ni mme au mke wa mwenye mali au ndugu au rafiki ya mwenye mali, lakini hana sifa nyingine ya kuongoza sehemu kama hiyo. Matokeo yake ni matatizo yasiyokwisha katika taasisi husika na uendeshaji mbovu wa shule kwa ujumla. Upo umuhimu wa bodi tarajiwa kuweka viwango na kudhibiti nani anakuwa mkuu wa shule na sifa anazostahili kuwa nazo.

Suala jingine ni kuhusu hadhi na viwango vya majengo ya baadhi ya vyuo na shule hapa nchini. Kuna shule ambazo zimeruhusiwa kuchukua wanafunzi wakati ambapo shule hizo hazina madarasa, mabwalo ya kulia; vyoo na bafu za kutosha. Na baadhi ya shule hizo ujenzi ungali unaendelea jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi wanaosoma katika maeneo kama hayo.


Kuhusu motisha na ubora wa rasilimali watu
ni kwamba shule nyingi zina walimu ambao hawana shahada ya kwanza achilia mbali ubingwa katika kufundisha masomo wanayofundisha na hususan sayansi na mahesabu. Matokeo yake tunawalaumu wanafunzi kufeli kumbe walimu wa masomo husika hakuna. Walimu katika shule nyingi wanalipwa mishahara midogo na ajira yao si kitu cha uhakika wakati wote. Kutokana na hili ni walimu wachache wenye wito kwani wengi wao ni wapita njia ambao wanasubiri kupata kazi bora zaidi ili waachane na ualimu mara wapatapo kazi nyingine bora zaidi.

Walimu wengi ni waoga au wanaamini ni kazi bure kushawishi wenye mali wanaotafuta faida kupitia huduma ya elimu kuwaongezea mishahara na ubora wa maslahi yao. Wenye mali kwa hiyo wanaendelea kuwadanganya walimu kuwa wanawalipa mshahara na walimu nao wanaendelea kuwadanganya wenye mali kuwa wanafundisha ipasavyo. Kwa yakini, wengi wao sasa wanafanya tuisheni majumbani kwa matajiri na hao ndio wanaoheshimiwa kuliko waajiri wa walimu.

Ingawa shule nyingi zinaonesha kuwa zinatoa masomo yote kama zilivyoruhusiwa, lakini ni chache sana ambazo zina walimu kwa kila somo husika. Mathalani, shule kadhaa zinaweza kumtegemea mtu mmoja tu kwenye mji au wilaya husika kufundisha hisabati au misingi ya uhasibu, au kemai, fizikia na elimu ya viumbe. Mwalimu anayefundisha shule zote hizi ni kwa kuwa anapenda hela, lakini hawatendei haki wanafunzi mia tatu au mia nne au zaidi anaowafundisha. Ni muhimu kwa kila shule kwa hiyo kuwa na mwalimu katika kila somo.

Katika miaka hii ambapo tumeanza kuzungumzia uwezekano wa shule na vyuo vyetu kujijenga na kukaribisha wanafunzi toka nje kikwazo kimoja kikubwa kinachoonekana leo ni ubovu wa chakula katika shule na vyuo vyetu. Kihistoria sehemu zilizokuwa zikipewa chakula cha ovyo, kwanza ni magereza, ikafuatiwa na JKT na kisha shule na vyuo. Tabia hii ya kuona shule na vyuo kwamba ni mahala watu wasipostahili kupata lishe bora haifai kukubalika na haistahili kuendelea kukubalika.

Njia ya kuhakikisha watoto wetu wanaokuwa mashuleni wanapata chakula na lishe bora ni kurudisha tena somo la elimu ya kujitegemea kwa namna wazazi watakayopenda kama ni wazazi kukubali watoto waoto wafanye kazi za kilimo, ufugaji, uvuvi na uzalishaji mali mwingine au wazazi watakuwa tayari kulipa wafanyakazi wa nje watakaolima mashamba na bustani na kufuga wanyama kwa ajili ya nyama na maziwa kwa watoto wao.

Ni muhimu pia kuangalia ubora wa makazi na malazi katika shule na kukaribisha uwekezaji wa watu wengine nje ya shule kujenga nyumba bora na salama karibu na shule zinazoweza kupangishwa na wanafunzi, lakini zikawa chini ya usimamizi na uangalizi wa utawala wa shule.

Taifa letu linazorota katika michezo na sababu shule na vyuo vingi binafsi vinapuuza sana michezo. Upo umuhimu wa kurejesha michezo shuleni na vyuoni kwani umuhimu wa michezo kwa maisha ya wavulana na wasichana inajulikana na yeyote aliyesomea saikolojia ya elimu na makuzi ya vijana.

Kuzuka kwa wanamuziki wanaotupigia nyimbo zinazopigwa ala na mashine kunatokana na ukweli kuwa si shule za umma wala binafsi zinazofundisha kwa dhati muziki na sanaa.
Mwanafunzi hakamiliki kwa kusoma tu darasani. Kuna kitu kianchoitwa elimu nje ya darasa. Hii ni elimu inayotokana na kumtembeza mwanafunzi sehemu mbalimbali kujiunza mazingira yake na kumfanya pia mtalii wa ndani katika nchi yake ili kuona urithi anaosthaili kujivunia na kuulinda. Upo umuhimu wa bodi kuhakikisha kuwa wanafunzi katika shule na vyuo vyote wanapata fursa ya kupata elimu nje ya darasa.

Kama tunavyojua shule na vyuo vyetu vingi vinapokea wanafunzi wenye dini mbalimbali. Upo umuhimu wa kuainisha majukumu ya uongozi wa shule kwa watoto wa dini mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa dini yao. Baadhiya shule zinadaiwa kuwanyima wanafunzi wa dini nyingine mahala pa kuabudu na vilevile, mathalani, kwa waislamu wakati wa mwezi wa Ramadhani wakuu wa shule huwa hawajali wanafuturu nini, wakati gani na mahala gani.

Kama tunataka kujenga upendo na undugu kati ya dini zetu lazima tabia kama hii ikomeshwe. Ni haki ya kila mwanafunzi kusali na kufanya ibada zake nyingine kwa mujibu wa dini yake.

Ni haki ya kampuni nchini kutunza siri ya mapato na gharama zake. Lakini siamini kuwa ni haki ya chuo na shule kuficha mapato na gharama zake. Wazazi wanastahili kujua kila shilingi inayoingia na inayotoka.

Baadhi ya shule binafsi na wazazi wanalalamika kwamba wakuu wa wizara ya elimu nchini hawawatendei haki kwa maana huwabagua wanafunzi wanaosoma shule binafsi. Hili hutokea pale wale wa msingi wanapomaliza shule na kuchaguliwa kwenda sekondari ya serikali. Mara nyingi wahitimu hao hupangiwa shule za mbali na makwao na halafu eti hutakiwa kuwa wanafunzi wa kutwa.

Ijulikane wazazi hao wanajinyima ili mtoto wao asome shule binafsi na sio kwamba wao ni matajiri kama watumishi wa serikali wanavyodhania.

Aidha, hapana sababu yoyote kwa shule na vyuo binafsi kunyimwa ruzuku na serikali wakati ambapo kuna baadhi ya shule zinajinoma kwa ruzuku kama hiyo.

Bodi ihakikishe kwamba kama kuna ruzuku basi ruzuku hiyo inatolewa wazi kwa shule na vyuo vyote kwa vigezo vitakavyowekwa na kufuatwa bila kupindwa.


http://www.blogger.com

No comments:

Post a Comment