Monday, May 23, 2011
Bajeti na Mustakabali wa Tanzania
BAJETI ni mpango kwa tarakimu. Kwa maneno mengine watu wakishaketi na kupanga mambo yao yote kwa matini (maneno), kazi hiyo ndefu hufupishwa na kuwa katika umbo la namba kwenye kurasa mbili tatu tu!
Kila tarakimu kwenye bajeti ni njia ama ya kupata mapato au ya gharama ya kufanya jambo fulani, lakini hatua iliyopo kati ya mipango na bajeti sio fupi. Kuna kuweka miundo na taratibu za kufanya kazi au mchakato mzima wa oganaizesheni, kuongoza na kusimamia watu katika kazi zao mbalimbali na juu ya yote kudhibiti mambo. Bila udhibiti gharama zote za kuandaa bajeti zinakuwa zimepotea bure. Udhibiti ndio jambo linalohakikisha kuwa mipango inakwenda sawasawa na ilivyo kwenye bajeti na kama kuna kasoro hatua za haraka huchukuliwa kunusuru jahazi husika.
Maana, mipango na bajeti vikishakuwa tayari sio mwisho, bali ndio mwanzo wa kazi. Shughuli zote tulizoziainisha hapo juu aghalabu hulenga kuona kwamba utekelezaji unalandana kwa asilimia kubwa na bajeti, mikakati na mipango iliyopo.
Haya yote yamerahisishwa na kile kinachoitwa serikali kwa teknohama [e-government]—mfumo unaomwezesha kiongozi kupata ripoti baada ya siku mbili au tatu kama sio saa chache, ambayo kwa mfumo wa serikali mapokeo ingelichukua miezi kadhaa kupatikana.
Ni dhahiri kutokana na ukweli huu kuwa na bajeti inayofanya kazi bila serikali kwa teknohama ni jambo la muhali na ndoto ya Alinacha.
Miaka ya kuwapangia watu kazi wasizo na ujuzi au utaalamu nazo imepita, na siri ya maendeleo ni kuwa na magwiji katika maeneo yao na sio kinyume chake. Safari kati ya mipango hadi kufikia utekelezaji sahihi sio fupi.
Njiani kuna mitihani ya kila aina, ikichukuliwa kama kitu hai italeta manufaa zaidi kwa watu na nchi yao vinginevyo, itaishia kugusagusa hapa na pale na mwisho ni kulaumiana na kunyoosheana vidole.
Sumu ya bajeti
Sumu ya bajeti katika nchi yoyote ile ni siasa. Ukiweza kutenga tu siasa na masuala ya fedha, kitaalamu na kiufundi basi unakuwa umeiondoa sumu hiyo. Ukiachilia siasa kuingilia kati ya hayo unaachia simu kuchuruzikia kila eneo unaloweza kulifikiria. Hatua ya kwanza kwa hiyo ya kuwa na bajeti inayofanya kazi na kuleta mageuzi na mapinduzi katika nchi ni bajeti kuachiwa kufanya kazi katika misingi ya uchumi huria bila ya kusiasaishwa.
Hili la kutenganisha masuala ya kifedha na kitaalamu na siasa huweza kufanikiwa tu kama nguzo kuu nne za taifa, yaani, ikulu, bunge, mahakama na vyombo vya habari vinakuwa huru na vyenye meno, kucha na misuli ya kuhakikisha kila chombo katika nchi kinafanya kazi iliyokusudiwa bila kuyumbishwa na kingine.
Bajeti haiwezi kuzaa matunda bora kama kuna udhaifu wa muundo na mfumo wa utendaji kazi katika serikali kuu, serikali za mitaa, mikoa, wizara na taasisi mbalimbali nchini.
Hali ilivyokatika nchi yetu ni kuwa uongozi wa nchi hii bado ungali unategemea mtu mmoja na taasisi iliyo chini yake na siyo mifumo na miundo ya kudumu ambayo yenyewe bila kuingiliwa na mtu ingelikuwa ikifanya kazi zake barabara. Hivi leo katika maeneo mengine ni vigumu kujua kama kiongozi huyu ni wa serikali au chama. Ukichangia na ule ukweli kuwa wakuu wa mikoa na wilaya ni watu wa kuteuliwa na sio wa kuchaguliwa na utii na uaminifu wao uko kwa chama tawala zaidi kuliko kwa wakazi wa mikoa husika na wananchi kwa ujumla wakati mwingi mengi yanafanyika ndivyosivyo kwa hasara ya umma na vita dhidi ya umaskini achilia mbali kuendelea na kuwa nchi katika dunia ya pili na siyo ya tatu.
Ipo haja ya kuwa na miundo na mifumo huru na hasa serikalini kiasi ambacho kama vile kule Uingereza au Marekani Waziri Mkuu au Rais na chama chake wanapoondolewa madarakani serikali haitikisiki hata kidogo.
Mdhibiti mkuu peke yake hawezi kufanya kazi ya maana kama ukaguzi haushuki hadi ngazi ya chini kabisa inayoguswa na mipango na bajeti. Mengi yanatokea katika ngazi za chini za serikali za mitaa, mathalani, bila mkaguzi mkuu kuona ndani.
Zipo habari za mabilioni yaliyotolewa kwa serikali hizo za mitaa kujengea uzio makaburi au kujenga masoko mapya au kuwezesha ujenzi wa hiki au kile kuisaidia jamii husika lakini fedha hizo zimepotelea hewani na mfumo uliopo sio tu haukamati hili hauwapi wananchi nafasi ya kufikisha malalamiko yao ili hatua zinazofaa zichukuliwe.
Tunaamini kuwa kiwango cha elimu cha madiwani na viongozi wengi wa serikali za mitaa kinachangia sio haba katika utendaji duni na maovu mengi yanayotokea huko. Ndiyo maana tunaishauri serikali ifanye haraka ya kuanzissha Chuo Kikuu nchini kitakachotoa shahada ya kwanza, uzamili na udaktari au falsafa kwa Kiswahili kwa viongozi wetu wa serikali za mitaa na wengine wanaotaka. Katika tafiti binafsi nimebaini kwamba kuna maofisa chungu nzima serikalini ambao hawajahawi kukutana na kuzungumza na Mzungu/Mwingereza moja kwa moja zaidi ya kumuona barabarani. Ikiwa kama hivi ndivyo, hivi kweli ni haki kumlazimisha mtu kujifunza somo kwa Kiingereza kama hatokaa akitumie Kiingereza hicho ? Ni kama vile kumlazimisha Mwandishi wa Habari wa Chombo cha Habari cha Kiswahili eti ajifunze Uanidishi wa habari kwa Kiingereza au lugha ambayo hatokaa aiandikie.
Nimetembelea sehemu mbalimbali duniani, lakini nilichokigundua ni kuwa maendeleo HUANZA tu pale nchi inapotambua na kuanza kutumia nguvu ya KIMTAJI NA KIMAENDELEO iliyomo ndani ya lugha yao ya taifa. Kwa mfano, Imarati na Uarabuni kwa ujumla, Uyahudi, Norway, Portugal, Indonesia, Malaysia, Korea Kusini, Vietnam na kadhalika. Wale wanaoshabikia Kiingereza au Kifaransa na lugha nyingine za kikoloni, kwa kawaida huwa wanakuwa na mwendo wa mbelenyuma, kwa mfano, Zimbabwe, Angola, Cote d'Ivoire, Kenya, Rwanda, Burundi na nchi kama hizo.
Pengine Waziri wa Fedha na Bunge lingevuta hatua moja nyuma safari hii na kuanza kutathmini thamani ya Mali asili zetu mbalimbali na kuzipa thamani mpya za kimtaji wa kimaendeleo. Baadhi ya vitu hivyo ni pamoja na Lugha ya Kiswahili; Ardhi yetu yenye madini inayouzwa au kukodishwa sawa na bure; Malezi yetu ya kijamaa; utamaduni wetu; urithi wetu na maliasili zetu; Mashirika yetu ya umma yanayobinafsishwa bila sisi kunufaika kitu na mengineyo kama hayo..
Suala la kuchukulia kupunguza gharama kama njia ya kuingiza mapato pia sio kitu kilichotiliwa mkazo sana. Lakini hili linahitaji kufanyiwa kazi ili kuliongezea taifa kipato kutokana na kuzuia gharama zisizo za lazima au kuzuia mianya inayoruhusu fedha za umma kufujwa na wajanja wachache. Bajeti inatambua kwa yakini umuhimu wa uzalishaji mali na utoaji huduma bora katika kukuza mapato ya serikali.
Kinachokosekana ni mikakati mahsusi ambayo inaeleweka na inaweza kutumika na mwananchi wa kawaida ili naye atoe mchango wake hata ukiwa mdogo kiasi gani.
Maana, kwa yakini akili ni nywele na kila mtu ana zake . Tusiidharau sekta yoyote wala mtu yeyote ambaye anaweza kutoa mchango katika kukuza kipato cha Mtanzania. Ili bajeti itoe mchango uliokusudiwa, wakati wote tuwe macho kutowabebesha watu mzigo usio wa lazima na hususan uchaguzi unapopita hili likiashiria kuwa bajeti ilikuwa ya kisiasa na mengine yote yalikuwa ngonjera kwa wajingawaliotakiwa kufunika kombe kafiri apite.
Pamoja na nchi hii kukubaliana na ushauri wa Umoja wa Mataifa kutumia asilimia 1.0 kwa utafiti, bajeti imechukukulia suala la utafiti na maendeleo au R&D kama linahusu tu kilimo. Labda kwa sababu za sera ya ‘Kilimo Kwanza’. Lakini ukweli ni kuwa kila suala la kiuchumi, kijamii, kiteknolojia, kiutamaduni na kisiasa linahitaji kuwa na R&D kwa malengo ya kunasa makosa, kujisahihisha na kufanya shughuli husika kwa njia au namna bora zaidi na kwa ufanisi na usanifu mkubwa zaidi. Katika hili la utafiti na maendeleo ni dhahiri kuwa Watanzania tuko nyuma kiasi cha kutisha hata tukijilinganisha tu na nchi nyingine za dunia ya tatu achilia mbali nchi zilizoendelea.
Bajeti yetu haiwezi kuvunja ungo endapo hakuna utafiti wowote wa maana unaofanywa kutuwezesha sisi wenyewe kuwa watawala wa maisha yetu na uchumi wetu. Utafiti na maendeleo ndio jambo pekee litakalotuwezesha kuwa na ubunifu na utundu zaidi katika kugundua njia mpya za kuongeza mapato na kupunguza gharama. Ni sawa kuanzishwa vitengo mbalimbali, lakini kama ilivyo katika sekta binafsi upo umuhimu wa kulea na kutunza rasimali watu yenye uadilifu, uaminifu, muruwa na upendo na jamii.
Na bajeti hizi zinastahili kufanywa na kuchapishwa kwa Kiswahili. Hii biashara ya kufanya tafiti na kuzitoa kwa lugha ambayo asilimia 95 ya watu wenu hawaizungumzi ninaona kama vile ni 'kujiuza' kwa wageni ambako hakuna tofauti na ukahaba, hata kama ni Mzungu ndiye aliyetoa fedha hizo za utafiti. Akitaka atafsiriwe baadaye baada ya kazi kwisha na kutoka katika Kiswahili.
Muulize mwekezaji yeyote wa ndani au wa nje, atakwambia tatizo kubwa la Tanzania ni kwamba mtu hawezi kuwaamini, kuwategemea wala kuwatumainia. Yule yule unayemwokoa kwa kumpa ajira ndiye anayekuchimbia kaburi asubuhi kweupe akuzike hata siku zako hazijafika. Wafanyakazi wa Kitanzania ni wababaishaji, wezi, matapeli, waongo, wahuni na hutaka kutajirika kwa mtaji usio wao.
Sioni popote panapoelezwa nia na makusudi ya serikali ya kulea na kutunza rasilimali watu yenye upendo na nchi na watu wake, kuchapa kazi, uzalendo, utii, uaminifu, uwazi na uwajibikaji kwa wale wanaowaajiri.
Anzisha vitengo au kamati mia au elfu za usimamizi na ukaguzi, lakini bila kumbadili Mtanzania hulka na nidhamu yake kuna kazi kubwa katika kuhakikisha bajeti inafanya kile ilichokusudia kwa nchi na watu wake. Hivi katika miaka na enzi hizi, serikali yetu inastahili kweli kuandaa hesabu zake na taarifa kwa bodi na wakaguzi kwa Kiingereza?
Bila shaka umefika wakati wa kufanya masomo au elimu ya uchumi, menejimenti na fedha ipatikane kwa wingi katika Kiswahili ili kuhakikisha mawazo mazuri yanayokuwemo katika mipango yetu sio tu yanafika hadi chini kwa wasio wasomi bali pia yanafanyiwa kazi na kuchangia kubadili uchumi na jamii yetu kwa namna bora zaidi.
Maendeleo hayatoki juu...
Matumizi ya Kiingereza nchini kwetu yametokana na kiasi kikubwa kuwa pamoja na uhuru wetu eti ni Uingereza na watu wao na pengine Marekani ambao leo tunawakumbatia kuliko hata Waingereza kwa kiingereza chao pia ndio wanaoweza kutunusuru na umaskini wetu.
Nina mashaka kama miradi ya mbu na chandalua, ukimwi na mingineyo kama hiyo ambayo ndio maeneo pendwa yao makubwa ndiyo mamboyatakayotusaidia kweli kupambana na umaskini, ujinga, maradhi na kuwa nyuma kimaendeleo kikwelikweli na sio kisaniisanii tu!
Aidha, huko nyuma nchi hizi zilikuwa mbele kweli kimaendeleo. Hata hivyo, Japani, Uchina, Korea na Imarati wanawapangua mmoja baada ya mwingine na leo wasiofunguka macho wanaendelea kupelekea watoto wao Magharibi (jua la maendeleo linazama), badala ya Mashariki ambako kunakuchwa. Labda maajabu yatokee, lakini binafsi ninaamini hii siyo miaka ya Uingereza na Marekani tena, bali hii ni Miaka ya Imarati, Uchina, Marekani ya Kusini, Ulaya ya Mashariki, Urussi na dada zake na sio vinginevyo!
Unajua maisha ni kuchagua na Watanzania sasa wana fursa ya kuchagua kwenda Magharibi au Mashariki. Kwa bahati mbaya, wenzetu wa CCM na serikali yao wameamua kutupeleka zaidi Marekani pamoja na shaka kubwa za Watanzania juu ya jamaa hawa na mustakabli wetu.
Kuna mambo ambayo ninaamini tutaonekana ni wajinga kama tutaendelea kuwategemea watu wa nje.
Masuala hayo ni pamoja na uwezo wa kujitosheleza kwa chakula, nishati na uwepo wa viwanda vya msingi nchini. Aidha, miaka kama hii kutegemea nchi za nje kujenga barabara, reli, bandari na viwanja vyetu vya ndege ni ishara ya nchi isiyo na dira wala inayojua inakotaka kwenda. Vitu vyote hivi ni lazima tuvishughulikie sisi wenyewe penda tusipende ndio kweli tutakuwa tunajinasua na umaskini.
Tusitegemee kamwe watu wa nje kama tulivyoona RITES na TRC kilichotokea, hata wakiwa marafiki kiasi gani. Labda tuelekee kwenye aina ya urafiki kati ya Marekani na Pakistan, pengine....
Bajeti haiwezi kufanya kazi nzuri ikiwa pia muundo wa nchi uko hobelahobela, unapwaya katika maamuzi na unachukua muda mrefu katika utekelezaji wa masuala ya msingi ambayo vinginevyo yangeliweza kushughulikiwa kwa haraka zaidi. Hiki kinachoitwa Decentralization by Devolution sio kitu kipya bali ni mvinyo ule ule katika chupa mpya. Nao sio mwingine ila sera ya mwasisi wa taifa hili aliyoiita Madaraka Mikoani.
Leo Decentrealization by Devolution inataniwa na baadhi ya watu kuwa Doing by Doing nothing [D by D] kwa sababu kwa ukweli mwananchi wa kawaida haoni dalili yoyote kwamba maamuzi yanafanywa na viongozi wake wa mkoa na sio viongozi wa juu wa kitaifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment