IKIWA tunataka wengine watupende, lazima tujipende kwanza sisi wenyewe. Hivi ndivyo ilivyo pia kwa jiji, miji, vijiji, mitaa na nyumba zetu. Kama tukitaka tuvutie zaidi majirani zetu au watalii au watu wengine inatulazimu kubadilika na kuanza kutengeneza mazingira yanayopendeza na kukubalika na watu wanaojipenda, wastaarabu, maridadi, mlimbwende, wasafi na wanaojiheshimu.
Ni vyema tuanze kujiuliza kama tunataka miji yetu iwavutie wageni ni mambo gani yanayolifanya miji hiyo hivi leo ishindwe kuwavutia watalii na wawekezaji au wakazi wapya?
Je, mojawapo ya tatizo linalochangia miji isikubalike hivi sasa kiutalii ni huduma duni na ghali? Tukilinganisha huduma zetu na za wenzetu kama Nairobi, Kenya, Mahe, Seychelles, Port Louis, Mauritius, Kampala, Uganda, Kigali, Rwanda na kadhalika sisi tupo wapi katika chati ya ubora?
Ni miji gani duniani ambayo inatia fora katika utalii ambako tunaweza kwenda kujifunza? Na malengo yetu yawe kufanana na nani? Na nini kitufanye sisi tuwe tofauti na miji mingine. Utofauti, tambua kuwa ni muhimu sana, na ndio utakaomfanya mtu kuchagua kuja Dar es salaam, Tanzania na sio kwenda Nairobi/Mombasa, Kenya!
Hivi hoteli zetu za 'Kiswahili' zinaweza kusimamiwa pia na Tanzania Bureau of Standards (TBS) ili pawe na viwango vinavyokubalika kiasi ambacho kwamba mtalii yoyote toka nje akubali kula huko na asiwe na wasiwasi wa afya yake? Hili haliwezekani au linawezekana? Kwa wanaosema haliwezekani watembelee hoteli kadhaa zilizokuwa za Kiswahili ambazo sasa zinavutia pia watalii papa hapa jijini!
Jiji na wakazi wake wana mipango gani kuongeza sehemu za starehe za kutosha katika jiji letu? Tunajua ni aina gani za starehe ambazo mzungu anayetoka Ulaya, Mchina au Mhindi au Mjapani toka Asia, au Mwarabu toka Lebanon atazitaka na kuzifurahia hapa nyumbani. Tuna mikakati gani ya kujitosheleza kwa sehemu hizo za starehe ambazo sio tu ni kiburudisho bali pia kivutio kikubwa kwa wageni?
Kuna mipango gani ya kuongeza aina ya viwanja vya michezo na ubora wake vinavyoweza kuwavutia wageni? Je, tuna kiwanja cha mbio za magari ambacho chaweza kufaa kwa mashindano ya Forumala 1 siku zijazo?
Tuangalie pia jinsi ya kuwa na viwanja vinavyofaa kwa mbio za baiskeli na pikipiki kiasi cha kuwapa vijana wetu wanaotupigia makelele na mapikipiki yao mitaani nafasi ya kuwa na kitu bora zaidi cha kufanya bila kuleta usumbufu kwa wakazi wengine?
Hivi hatuwezi kuwa na mbio za Marathoni kati ya Dar na Bagamoyo -kila mwaka na mashindano hayo yakavutia wanamichezo na maelfu ya watalii kila yanapofanyika? Yatia moyo kusikia kampuni ya Vodacom imeamua kusaidia kuwepo kwa mbio za aina hii ambazo zitaanza karibuni. Hii ndiyo njia kamapuni nyingine zinazotakiwa kufuata ili kusapoti na kuendeleza sio tu michezo bali mvuto wa miji yetu kwa watalii na wawekezaji.
Na mchezo huo ukienda sambamba na michezo mingine ya riadha hatuwezi kuwa na kipindi kizuri tu cha kuwatahini wanariadha wetu na wakati huo huo kufanya biashara kubwa ya utalii toka wateja wa nje na ndani ya nchi?
Hapa jijini kuna hoteli za maana sana lakini la ajabu ni kwamba ni chache tu kati ya hizo zina 'swimming pools'. Je, tutafanya nini ili upatikanaji wa maji uwe rahisi kiasi cha kuwa na mabwawa ya kuogelea sio tu kwenye hoteli kubwa kubwa, bali pia kwenye hoteli ndogondogo?
Hoteli kubwa kwa ndogo huwa zinatania au zinafanya kweli inapokuja kwenye sala la tiba na afya. Hivi kuna hoteli yoyote yenye zahanati kama sio hospitali ya maana ndani ya majengo yake au jirani ambayo yatamuhakikishia mgeni usalama wake ikiwa kama ataugua ghafla. Au mtalii atapaswa kusubiri masaa kadhaa kabla ambulensi haijaja, na akifika huko dokta asiwepo, na dokta akiwepo kuwe na sarakasi tunazoziona huko Temeke na Amana-kiasi cha mpaka mtu kupoteza maisha kimzaha mzaha tu?
Hivi Bwana Sumaye alipoondoka kaondoka na watendaji wote waliokuwa wakijitahidi kiasi cha kutia moyo kuhusu usafi wa jiji. Huduma hiyo imebinafsishwa lakini hivi leo ni maeneo ya wakubwa ndio labda kuna usafi lakini maeneo ya Manzese na kwingineko uswahilini ni balaa tupu.
Hivi, tumejipanga vipi kuwa na wafanyakazi kwenye mahoteli na sehemu zingine za biashara wanaoweza kuzungumza sio tu Kiingereza bali pia Kijapani, Kihindi, Kichina, Kihispania, Kiswidishi, Kirussi na kadhalika? Je, watalii wanapenda miji yenye baadhi ya watu wanaozungumza lugha zao au miji ya watu wasiozungumza kabisa lugha zao?
Je, jiji la Dar es salaam linaweza kujipanga upya kukawa na viwanja vya michezo kwa wakubwa na watoto, bustani za kupumzikia, misitu kama ile ya Laufpark kule Baden Wurtenburg, Ujerumani ambayo inatokana na maeneo yaliyochimbwa au majalala yanayogeuzwa kuwa misitu midogo?
Hivi haiwezi kutokea fumba na kufumbua ikawa katikati ya Dar es salaam na pembezoni mwake kuna misitu yenye ukubwa wa angalau asilimia 20 ya eneo lenye majengo la jiji hali ya hewa hapa jijini itakuwaje? Itawafanya watalii walikubali au walikatae jiji kama eneo la kuishi kwa muda?
Na hivi kweli hakuna wenye uwezo wa kuanzisha Bustani ya Wanyama katika maeneo jirani na Pande au Chalinze au Kimanzichana ili watoto wetu wa shule wajue punda mlia au twiga au swala alivyo bila kwenda mbali sana na jiji? Na, je, hili halitawavutia pia watalii wajao Dar? Idara ya Wanyama Pori inahitaji msaada gani ili iweze kufanya jambo kama hili kibiashara?
Niliwahi kutembelea maeneo ya sadani, Bagamoyo na kukuta hoteli zilizojengwa kwa makuti na mikeka. Je, wabunge wa Pwani hawana mkakati wa kuiga toka kwa wazungu waliofanya haya ili wakazi wao wajikomboe na umasikini kwa kuwa na hoteli ya kitalii inayojengwa kwa gharama sawa na bure lakini watalii watakayoihusudu. Katika mahoteli yao ni vyoo, bafu na taa tu ndivyo vitu vinavyoagizwa toka nje!
Hili linaendana na swali la je, ni utamaduni upi mgeni au mtalii anaouona Jijini kwetu ambao unamfanya aamini kuwa huu ni utamaduni pekee wa Kitanzania na wakazi wa eneo hili la Pwani ya Tanzania? Au tunawaonesha vilevile walivyovizoea kuviona kwao au katika nchi zingine zinazobabaisha pia katika biashara hii yenye manufaa kwa nchi na watu wake kama ikiendeshwa vizuri?
Katika jiji kama Dar ambalo hivi leo kwenda mahala kama Mbagala au Bunju unaweza ukajikuta unatumia masaa mawili kama sio matatu -mtalii atakuwa na uvumilivu wa kufurahia utalii wake kweli? Ni nini kifanyike ili mahala pa mwendo wa nusu saa kweli iwe nusu saa na sio vinginevyo?
Je, ni mabadiliko gani yanayoweza kufanywa katika Uwanja wa ndege, bandari na vituo vya mabasi ili sehemu hizo peke yake viwe ni vivutio vikubwa kwa utalii. Je, Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere unaweza ukafanana na Dubai?
Je, bandari ya Dar es salaam wanakoingilia na kutoka watu linaweza kuwa kituo cha starehe ya aina yake kwa wanaosafiri na wasiosafiri. Je, viwanja vyetu vya mabasi vinaweza kuwa vivyo hivyo pia?
Baada ya kusema hayo nimalizie tu kwa kukubali kuwa Dar es salaam kama jiji ina fursa mbichi kadhaa ambazo kama zikitumika sio tu vitafanya maisha ya wakazi wa jiji hili yawe bora zaidi bali pia yatatuletea heshima na jina nchi za nje. Baadhi ya fursa hizo ni:
. Fursa ya utali wa anasa na starehe-ambao wanaokuja zaidi ni watu matajiri au wakubwa wenye uwezo wa kifedha na wanataka kupumzika na kutumia tena kwa fujo. Hawa wanapendelea zaidi maeneo yenye fukwe.
. Fursa ya utali wa michezo-ambao huvutia zaidi wapenda michezo ya aina mbalimbali. Hili, hata hivyo, linahitaji nchi kuwa na miundo mbinu ya michezo kama vile basketiboli, riadha, ngumi, mbio za magari, mbio za pikipiki na baiskeli, mbio za marathoni, tenisi, golfu na kadhalika.
. Fursa ya utalii wa wanafunzi, kielimu na kitaaluma-ambao wanaokuja ni walimu au wanafunzi wanaotaka kujifunza na kuandika insha au vitabu maalum juu ya fani fulani ya maisha, uchumi au jamii hapa nchini.
. Kuna utalii wa wastaafu-ambao aghalabu baadhi ya nchi za Ulaya hutenga fedha ili wafanyakazi wao wazee waliostaafu waje kupumzika Afrika hasa wakati huko kwao kuna baridi kali.
. Ipo fursa pia ya utalii wa wafanyakazi ambao wao wenyewe au makampuni yao huandaa safari kuja Afrika ili wafanyakazi wao wapumzike na kisha warejee wakiwa na nguvu na ari mpya ya kufanya kazi zao kwa faida yao na waajiri wao.
. Kuna fursa ya utalii wa kiuchumi na kibiashara-ambao wanaokuja pamoja na kutaka kupumzika huangalia pia maeneo ya kuwekeza. Wakisharudi makwao hujipanga upya na pengine kuamua kuhamia moja kwa moja jijini au popote nchini kwetu kwa kuwa pamekidhi ndoto na mipango yao ya baadaye.
Tukijipenda sisi wenyewe kwanza, bila shaka na wengi wengine karibu na mbali watatupenda pia. Tuifanye miji yetu kuwa safi na bora kwani hii nayo ni njia isiyo ghali ya uwekezaji utakaokuwa na faida kubwa kwetu na vizazi vyetu.
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment