Monday, May 23, 2011

Barabara za Dar na dawa mujarabu ya foleni

UONGOZI wa Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni uliwapa jamaa wa Sumatra changamoto kuhusu mchango unaotakiwa toka kwao, ili kupunguza matatizo ya

usafiri na wasafiri jijini.

Wiki kadhaa zilizopita, gazeti hili lilikuwa na makala iliyoshauri kuwa ni vyema jiji likawa na Mamlaka yake yenyewe ya Usafirishaji kwani wale waliopo hivi sasa,

yaani Sumatra na Tanroads, pengine wana kikombe kilichojaa mno na hawawezi kuyashughulikia matatizo ya jiji kikamilifu na kwa uhakika kama inavyotakikana.

Tunaamini pia kwamba, Tanzania ya leo inahitaji mtazamo na mkakati mpya wa kushughulikia maendeleo au ukosefu wa maendeleo katika maeneo tofauti.

Eneo hili la usasirishaji na uchukuzi sio eneo lenye matatizo ambayo hatuwezi kuwa na akili ya kuyatatua sisi wenyewe kwa kutumia rasilimali watu na rasilimali

nyinginezo zinazohitajika.

Pengine shida yetu kubwa, ni kuwa inawachukua muda Watanzania walio wengi kuelewa kuwa maendeleo ni neno linalotumika badala ya kutatua matatizo. Kwa

maneno mengine, kutatua matatizo ya watu au nchi ndio maendeleo.

Adha ya usafiri na foleni zinazoandamana nazo si habari mpya. Sasa ni sehemu iliyokubalika shingo upande na kila mkazi wa jiji. Lakini kweli unaweza kukubali

matatizo na papo hapo ukapata maendeleo au ustaarabu hata ule wa bure. Ninaamini, haiwezekani kwa Watanzania kuendelea ikiwa tabia yao itakuwa ni

kukubali kuishi na matatizo ya aina mbalimbali; yawe ya barabarani au nje yake.

Binadamu yeyote anayeshindwa kupambana na mazingira yake na matatizo yanayomzunguka hahesabiki kama binadamu hai. Na baadhi ya viongozi na

wananchi wa Tanzania, hivi sasa kwa bahati mbaya wameangukia katika kundi hilo la watu wanaokubali kuishi na matatizo yanayotatulika miaka nenda rudi.

Makala haya yatakuwa sio kwa faida ya wafu ninaowazungumza bali wale walio hai na wasiokubali kabisa kushindwa kudhibiti mazingira yao na kukabiliana na

changamoto za kila aina zilizo mbele yao na kila inapowezekena kugeuza changamoto hizo kuwa fursa za kimaendeleo, kiuchumi na kibiashara.

Mahala pa kuanzia kabla ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lolote ni kujua tofauti kati ya dalili na chanzo halisi cha tatizo.

Tatizo la foleni jijini linachangiwa na uamuzi wa kihistoria wa kujenga mji huu kando ya bandari ya Dar es salaam. Ikulu, waziri mkuu, wizara, ofisi za mabalozi,

benki, vyuo, mahospitali, ofisi za jiji, Tanesco, Posta, mashirika ya simu, Dawasco, makao makuu ya polisi, reli, shule za msingi na sekondari zenye majina, ofisi

kuu za vyama, bunge la zamani na kadhalika; vyote vilikuwa hapa.

Hii ina maana kwamba, mkazi wa Dar es salaam yoyote mwenye kazi au shida fulani lazima atumbukie katikati ya jiji hili. Je, hapa kweli tunashindwa kumjua

mchawi ni nani.

Je, hali ingelikuwa kama hivi kama tungelitawanya maofisi mbalimbali ikiwemo yale ya mawizara kwenye vitongoji nje ya eneo hili kuu la kibiashara jijini?

Isitoshe wapo wanaoamini kuwa hivi leo kuna maofisi ambayo yamepitwa na wakati kuwemo katikati ya mji. Ofisi hizo ni pamoja na Ikulu, Hospitali ya Muhimbili,

wizara karibu zote, benki, posta na kadhalika kama ilivyokuwa wakati tulipohamisha kituo cha mabasi Kisutu kikawa angalau mbali na kati ya mji.

Na kuna wanaodai kwamba, kama serikali ingelikuwa haifanyii mzaha suala la kuhamia Dodoma leo adha inayowapata wakazi wa Dar isingelikuwa hivi ilivyo. Wao

wanashauri nini? Wanashauri serikali ijipe muda kuuza majengo yake yote yaliyomo kati ya mji ili fedha itakayopatikana iende kujenga Dodoma na ofisi ndogo za

serikali maeneo ya Kibaha au Chalinze.

Wanachokiona wao ni kuwa asilimia kubwa ya watu wanaolazimika kuingia kwenye chanzo cha foleni, yaani, kati ya jiji watahama kwani sasa watalazimika kwenda

nje ya mji na sio kuingia ndania ya jiji.

Lakini pia kwa sababu za Kiusalama kuna wale wanaosema kwamba, kama itatokea Tsumani Dar es Salaam saa za kazi, basi watumishi wakuu wote wa serikali

wataangamia. Ni nini kitachotokea kama moto mkubwa kama ule wa London kwenye miaka hiyo ukizuka katikati ya jiji tena saa ambazo ndio kwanza foleni

zimekuwa kama mkufu wa sisimizi ?

Hili linatupeleka kwenye chanzo kingine cha tatizo la foleni hapa jijini. Ni dhahiri barabara za kutokea ni chache mno. Watu wengi kama patazuka baa kama

yaliyotajwa hapo juu watalazimika kuacha magari yao na kutimka kwa mguu. Ama hakika itakuwa kizaazaa na wengi watakufa njiani kwa hofu na uoga achilia

mbali kwa moshi au maji yatakayowaandamana.

Barabara za ringi

Miaka sio mingi iliyopita nikiandikia gazeti la Business Times, mara baada ya kutoka Ubelgiji nilitoa rai kwamba, tuangalie uwezekano wa kujenga barabara za ringi.

Barabara za ringi ni aina ya barabara zinazouzunguka mji ambazo ni maarufu kwenye miji mbalimbali huko Ubelgiji na zimechangia kumaliza matatizo ya usafiri na

uchukuzi nchini humo.

Barabara hizo ni za mduara zikizunguka mji mzima kwa ngazi tatu au zaidi. Na katika kila ngazi kuna ukomo wa magari yanayoruhusiwa kuingia ndani ya ringi au

jiji. Mathalani, malori makubwa ambayo ni kawaida kuzagaa hapa jijini huwa hayaruhusiwi kuvuka ringi ya tatu. Mizigo yao huwekwa kwenye magodauni yaliyomo

humo na kuingizwa katikati ya jiji na malori madogo ya tani 2 hadi 3.

Barabara hizi za ringi zinaruhusu pia kujenga utando wa barabara wa aina ya utando wa buibui ambao unarahisisha watu kuingia na kutoka katikati ya jiji kwenda

pembezoni ya mji. Katika miji mingi ya Ubelgiji makazi ya watu walio wengi na wanaojali afya zao hayako katikati ya mji bali pembezoni mwa mji. Katikati ya mji

wanafunzi ndio wanaoishi humo zaidi.

Hii ina maana kwamba, barabara za ringi zina tabia ya kuzusha miji ya satelaiti pembezoni mwa uliokuwa mji asilia. Miji ya pembezoni kwa kawaida huwa bora,

misafi na yenye huduma zote muhimu ziwe za kibiashara, kiserikali au kibinafsi na hakuna tena mtu anayelazimika kuingia katikati ya mji ili kupata huduma.

Chanzo kingine cha matatizo yetu ya usafirishaji na uchukuzi ni kushindwa kuwatumia wasomi na watafiti wetu ipasavyo ili tuwe na ufumbuzi wa ndani wa matatizo

yetu. Ninaamini, hakuna nchi ya Kiafrika itakayoingiza mguu wake kwenye barabara ya maendeleo ya kweli na uhakika bila kuwa na uwezo wa kujenga barabara

na miundombinu yake mingine yenyewe.

Yapo mambo ya kusaidiwa toka nje, lakini kwa hakika sio ujenzi wa barabara, chakula, kilimo na viwanda vya msingi. Tuamke katika hili na kupiga vita umaskini

haitakuwa tena ni ndoto bali kitu chenye uyakini na uhalisia unaothibitika.

Katika kazi hii ya kuleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi ieleweke hata hivyo, kuwa wababaishaji, wazembe na wale wanaoahirisha mambo kila

kukichwa hawastahili kuwepo. Hao wanastahili kuwa mbali kabisa na sekta hii ambayo ina hatari ya kuchafua umoja na amani ya nchi kuliko kitu kingine chochote

fumba na kufumbua.

Aidha, tusiogope kubomoa ili kujenga upya. Kwa wanaoenda na wakati katika masuala ya nadharia mbalimbali za kileo watakuwa wanafahamu kuwa hivi sasa ipo

nadharia inayoongelea kubomoa ili kujenga (destructive construction) ili mambo mapya na bora zaidi yawezekane kuwepo.

Tuwahimize wahandisi, wasanifu na wataalamu wetu waanze kubadilika kwa kuzingatia kwamba, fedha sio kila kitu. Hakika heshima ya Mtanzania kesho na

keshokutwa haitapatikana kwa mtu kuwa na fedha nyingi au kuwa tajiri, lakini kutokana na mtu huyo atakachowafanyia Watanzania na Waafrika wenzake.

Ufumbuzi wa tatizo hili pia unahitaji kutumia hekima na busara zinazoendana na ukubwa na gharama wa miradi inayofikiriwa. Nchi hii iko taabani kiuchumi, dunia nayo imechafuka, wafadhili wanatuchoka, je, kweli barabara za juu zinastahili kuwa kwenye ajenda ?

Au ni kitu fikirifu na tafakarifu zaidi kuzungumzia ujenzi wa tramu, barabara au reli za chini kwa chini, madaraja ya kuondoa msongamano upande mmoja wa kakutano au matumzi ya mabsi au treni ziendazo kasi mjini ? Kinachoonekana, hata hivyo, ni kuwa yanazungumzwa mengi katika kuwapooza na kuwapumbaza wananchi lakini hakuna hata kimoja kinachofikiwa kwa undani wake, na hususan juu ya faida na hasara zake, na hasa unapozingatia kauli ya viongozi kuwa hawawezi kudhibti kuingia kwa magari nchini. Maana, kwa upande mmoja, hapa kuna tatizo la kisera na pia tatizo la mipango miji. Ingelifaa serikali ihamie Dodma, kwnai hili linaweza kupunguza foleni kwa asilimia 30. Kisha nyumba zote zilizokuwa maofisi ya serikali ziuzwe na pajengwe jengo moja refu litaloweka wizara zote (sio 60 bali wizara chini ya 15 tu). Kisha wahusika na ardhi na nyumba waanze kupanga mipango ya kuwa na eneo litakaloitwa New Dar es salaam, kama ilivyokuwa huko Marekani enzi hizo na leo kinachoendelea huko Dhakka, Bangladesh.

No comments:

Post a Comment