KWA MUJIBU wa vyanzo vinavyoaminika, Tanzania kichakula iko salama. Lakini usalama huo unategemea kuwa chakula kilichopo hakitakuwa kinauzwa nchi za nje na kupaacha nyumbani patupu.
Pamoja na hayo, hali ya hewa iliyojitokeza Ulaya na Asia mwaka huu inaashiria kwamba panaweza kuwa na tatizo la kupatikana mvua na chakula cha kutosha mwaka huu; pia hali ya ukame na ukosefu wa maji katika sehemu mbalimbali nchini kuongezeka.
Kusini mwa Tanzania, huko Msumbiji hivi sasa kuna mafuriko. Ingawa taarifa za hali ya chakula zinatutia moyo lakini haya yote hayaashirii kwamba mwaka huu utakuwa na chakula cha kutosha. Na hata kukiwa na chakula cha kutosha kwa kuwa milango ya Tanzania iko wazi usiku, haielekei kama chakula kitabakia hapo kilipo na sio kupelekwa nchi za nje na hivyo kusababisha uhaba wa chakula nchini.
Kwa maneno mengine, taarifa za hali nzuri ya chakula 2008/9 zimewafanya watu wajisahau na kutokumbuka kuwa kama majirani wana njaa, wakikichukua chakula hicho basi wao ndio watakaojikuta na njaa kali zaidi!
Kwa mujibu wa taarifa za usalama wa chakula Oktoba 2008-Machi 2009, pamoja na kuwa chakula kipo cha kutosha, mijini bado bei yake ni nje ya uwezo wa Watanzania walio wengi. Watu wanaweza kwa hiyo kuwa na njaa sio kwa sababu chakula hakipo lakini hawakimudu kutokana na bei yake kuwa kubwa mno.
Taarifa hiyo imeonya kwamba kwa upande wa mifugo kuna hatari ya Homa ya Bonde la Ufa na kwa upande wa mhogo upo uwezekano wa ugonjwa wa mchirizi wa rangi ya udongo unaoshambulia mihogo kutokea pia. Hili likitokea wanaokula mchicha, sukuma wiki na kisamvu watazidi kuongezeka. Protini itaadimika zaidi ukizingatia pia kwa hivi sasa ni wachache wanaomudu kununua samaki.
Hata hivyo, taarifa hii imeshindwa kuonesha ni kuwa nchi jirani zenye uhaba wa chakula na zitakazofungua milango yao kupokea chakula kutoka Tanzania kihalali au kwa haramu zinaweza kuongeza hali ya kutokuwa na usalama wa kutosha kwa upande wa chakula.
Utafiti wa kijuujuu uliofanywa maeneo ya Himo na vijiji jirani mkoani Kilimanjaro unaoenesha kwamba mahindi husafirishwa nje ya nchi kila usiku.
Himo imegeuka ni kituo kikubwa cha kuhifadhi bidhaa hiyo haramu kabla haijasafirishwa kwenda nje. Wenye nyumba pale Himo wanafukuza wapangaji ili kukodisha majengo yao kwa wasafirishaji haramu wa mahindi.
Nyumba moja sasa inakodishwa kwa kati ya 150,000/- na 300,000/- kwa usiku mmoja. Na hii imesababisha wenye nyumba kuona kodi za pango la wapangaji wa kawaida ni sawa na chakula cha kuku kwao!
Hili linaweza kukupa picha ya biashara nzuri ya ulanguzi wa mahindi na nafaka nyingine inayoendelea kaskazini mwa Tanzania. Lakini ni ishara nzuri kuwa baada ya muda sio mrefu kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula katika mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida na Dodoma.
Na sijui ni nini kitakachowazuia walanguzi wa Kaskazini mashariki ya Tanzania kuhamia maeneo mengine ya nchi kupanua biashara yao ya ulanguzi kwa ajili ya kupata faida kubwa zaidi.
Nina hakika Zimbabwe, Kongo, Burundi na Zambia nazo zina upungufu mkubwa wa chakula na hivyo ni rahisi pia kwa mikoa jirani na nchi hizo kuwa na njaa mwaka huu!
Huko Kenya, inaelekea mahindi yanahitajika sio tu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa nchi hiyo bali pia kuna makundi kadhaa ya watu wanaoyasafirisha mahindi hayo kwenda Sudan ya Kusini, Somalia na Ethiopia.
Bei za nafaka nchini kutokana na hali hii haziwezekani tena kushuka wakati tunaelekea kwenye masika tarajiwa. Mvua ikinyesha patakuwa na afueni kutokana na mazao kama ndizi, viazi na mihogo. Isiponyesha hali itazidi kuwa mbaya.
Njaa na siasa
Huko nyuma, njaa ikija karibu na kipindi cha uchaguzi mkuu inakuwa ni neema na baraka kwa wanasiasa walioko madarakani.
Misaada ya chakula iliyokuwa inatolewa, aghalabu, ilikuwa ikigeuzwa kuwa tenda zenye maslahi makubwa kwa wachaguliwa wachache na chama kilichopo madarakani.
Je, mwaka huu, hali hii pia kama ikitokea inaweza ikatumika kisiasa kwa watu kujisahau na nafaka yote ikishapelekwa Kenya ndio watu washtuke kuwa tuna upungufu wa chakula na kuanza kuhaha kuomba msaada wa chakula ili ugeuzwe nyenzo ya kisiasa au wafadhili hivi sasa watakuwa wamekwishafunguka macho na kukataa mtego huu?
Kuanzia Iringa, Kilimanjaro hadi Dar es Salaam, nchi wakati fulani ilikuwa na maghala yaliyohifadhi tani kadhaa za vyakula katika kile kilichojulikana kama Mkakati wa Taifa wa Uhifadhi Nafaka. Je, mradi huo upo. Je, hivi leo tunajua tuna akiba kiasi gani ya chakula na hususan nafaka ili kama mvua zitakataa Machi mwaka huu tuwe na uhakika kwamba tunaweza kubangaiza hadi Machi 2010?
Hali ya maji nayo pia sio nzuri. Na sote tunajua kuwa maji yakikosekana basi kunazuka matatizo ya kila aina nchini ikiwemo umeme kukosekana muda mrefu, mitambo na mashine za uzalishaji mali kuzimwa; na huduma mbalimbali kuathirika kwa hilo.
Je, tuna mkakati gani wa kuwa na njia mbadala za kupata maji? Mvua zikinyesha, je, tutaweza kuvuna maji badala ya kuyaachia yaishilie tu baharini? Au ni nini kinachoweza kufanyika ili maji ya Ziwa Victoria, Tanganyika, Rukwa na Nyasa na mengineyo yawe na faida kwa Mtanzania achilia mbali kumhakikishia uhai wake hapa duniani?
Tanzania imekwishaamua kuwa nchi yenye kufuata mfumo wa soko huru kiuchumi. Na haipendezi kuona tena serikali inalazimika kuingilia kati mambo ya kibiashara. Lakini kwa kuwa chakula ni jambo linalogusa uhai wa mtu haiwezekani serikali kukaa pembeni na kuwaachia wajanja wachache kuwaingiza walio wengi katika mashaka ya njaa na uhitaji kutokana na tamaa ya faida ya haraka haraka.
Ni lazima serikali wakati wote iwe inajua hali halisi ya chakula sio kwa kubuni au kusikia bali kwa kutathmini hali halisi kama ilivyo nchini. Hata kama kuna akiba ya taifa, akiba hiyo isitumike kwa ajili ya tatizo la kujitakia.
Kwa hiyo ni lazima kuhakikisha nchi inafungua biashara ya chakula kwa namna ambayo watu wanakuwa huru kuuza ziada lakini wawe na nidhamu ya kubakiza chakula cha kutosha kila mwaka.
Uuzaji chakula nje unaweza ukawa ni njia ya kuliongezea taifa pato na hivyo kuwapa Watanzania fursa ya kuchagua vilivyo bora zaidi. Lakini uuzaji huo usifanyike kwa namna ambayo chakula kinauzwa bila watu kujua akiba iliyopo. Aidha isifanyike kwa njia ambazo zinaikosesha serikali pato linalotokana na kodi za uuzaji bidhaa nje. Pato ambalo lingejazia mapengo yanayojitokeza katika bajeti ya nchi.
Serikali ya awamu ya nne ina wizara saba ambazo zikishirikiana na kukawa na ushirikishwaji wa majeshi yetu tunaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika muda mfupi kiasi tusichofikira.
Kuna takriban Wizara saba ambazo zikiwa na ushirikiano mzuri kazi ya kuleta mapinduzi ya kilimo inaweza isiwe ngumu kama tunavyofikiria, zikiwamo Wizara ya Fedha na Uchumi,
Viwanda, Biashara na Masoko; Kilimo, chakula na Ushirika; Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa;
Maji na Umwagiliaji; Maendeleo ya Ufugaji na Uvuvi na ile ya Maendeleo ya Miundombinu.
Wizara ya Ulinzi na JKT?
Kuna wanaoweza kuuliza hata nayo Wizara ya Ulinzi pia? Jibu ni ndio kwa sababu binafsi ninaamini jeshi letu bado linaweza kuwa na mchango mkubwa katika utengenezaji wa vifaa na zana za kilimo, umwagiliaji maji na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Ushirikiano wa karibu wa wizara hizo unahitaji kwa sababu shibe ndio changamoto ya kwanza kwa serikali yoyote ile. Ni rahisi mengine kufanyika ila lazima kwanza watu wawe wameshiba vinginevyo tutakuwa tunajidanganya.
Barua-pepe: sammy.makilla@columnist.com
Vikwazo kwa Demokrasia nchini KATIKA makala hii nitajaribu kudhihirisha vikwazo vikuu vya kukua na kuimarika kwa demokrasia nchini. Vikwazo nitakavyovizungumzia leo ni pamoja na kukosekana kwa katiba mpya; kuwepo kwa chama-dola kinachotamalaki kila nyanja ya maisha nchini; kuwa na Baraza la Mapinduzi linalopindua uhuru na haki za binadamu Zanzibar wakishiriana na wale wasiotambua wajibu wao katika mfumo wa vyama vingi na umaskini wa Vyama Mbadala. Kwa wale wanaotaka kujifunza zaidi juu ya vikwazo basi waone makala zilizoko katika http://demokrasiaafrika.blogspot.com.
Kuachia watu wawe na demokrasia ya kina na pana kunataka moyo. Ni jambo ambalo halitofautiani sana na kukubali binti anayependwa na kuaminika nyumbani kuolewa. Wazazi huwa na taabu sana kutokana na mazoea kuamini kuwa watapata amani na huduma waliyoizoea kutoka kwa mtu mwingine. Lakini wakati ukifika umefika. Hakuna njia ya kuzuia yanayopaswa kutokea. Maana wakati ni ukuta na ukiupiga kofi au ngumi utaumiza tu mkono wako mwenyewe. Demokrasia kama mwali lazima apewe wananchi. Hatuwezi kuendelea kumlazimisha kukaa ndani mwetu milele. Mliopo madarakani amueni Demokrasia Ruksa ! Ili hili lifanyike yapo mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika kwanza.
Mambo hayo ni pamoja na: Kuandikwa Katiba Mpya. Katiba mpya sio jambo la kisiasa au kiserikali tu. Katiba mpya ni makubaliano mapya yaliyostahili kuwepo kati ya watawala na watawaliwa tangu siku ile nchi hii ilipoamua kuwa nchi ya siasa za vyama vingi. Tumechelewa. Na wakati ni huu. Afrika nzima inaitazama Tanzania kuona kama tumekua na kukomaa kisiasa au la. Tusikubali kutanguliwa na tutoto vya jana kisiasa katika hili. Umuhimu wa katiba mpya ni kwamba utamaliza kabisa matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kutoka mfumo wa vyama vingi uanze. Baadhi yake ni pamoja na haki na uhuru wa watu kuzungumza, kukutana,
kuandamana na kuunda au kuua vyama; vyama kadhaa kujiunga na kuwa kimoja kwa hiari yao wenyewe; matumzi ya redio, magazeti na televisheni ya umma; haki ya kumiliki mali zilizozalishwa na wananchi wote kwa pamoja; nafasi za makundi ya vyama vyote ya vijana, wazee na wanawake tofauti na yale ya kichama na kadhalika. Katiba hiyo inatakiwa kuandikwa na wawakilishi wote wa wananchi ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wetu wote kwa angalau miaka 50 ijayo. Hili sio jambo la kufanywa na wanasiasa au wanasheria wachache hasa ukizingatia tofauti za kijamii, kiuchumi na kisiasa zilizopo leo. Ni jambo linalohitaji ushirikishwi wa washika-dau wote wa Kitaifa.
Demokrasia nchini hapa haiwezi kabisa kukua na kuimarika kama tunaendelea kuwa na chama-dola ambacho kwa heri au shari kinaathiri maamuzi na utekelezaji wa mambo mbalimbali. Ikumbukwe wanasiasa ni watu. Na kila mmoja wao ana matarajio na matamanio yake. Ni rahisi kwa chama-dola kujikuta kinachanganya maslahi binafsi ya viongozi wake na maslahi ya umma. Mathalani, katika sakata la ufisadi linaloendelea hapa nchini kwa hivi sasa. Pengine viongozi wa kisiasa kweli wamenufaika kwa kiasi fulani lakini wananchi walio wengi wamekula hasara. Tatizo la chama-dola ni kuwa mawaziri wake aghalabu hujali tu maslahi ya chama na sio ya wananchi wote.
Kwa hiyo maamuzi hufanyika sio kwa manufaa ya Watanzania wote bali kwa sababu chama fulani kitanufaika na maamuzi hayo au vyama fulani vitaumizwa na maamuzi hayo. Katika bunge la chama-dola tatizo ni hilo hilo. Bunge la namna hiyo hujali zaidi maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya wananchi. Hili linapotokea uwakilishwaji wa wananchi na wabunge wao huwa umeorojeshwa kiasi cha kuwa hauna maana wala mchango wowote wa maana katika maisha ya wananchi waliowapeleka wabunge hao bungeni.
Ukiritimba wa chama-dola huathiri hata uongozi wa mikoa na wilaya. Katika mikoa na wilaya nyingi kinachoogopa huko sio serikali yenyewe bali chama kinachotawala. Matokeo yake utakuta kuna unafiki zaidi kuliko kujitambua kwa viongozi hao na kubaini mchango unaotakikana toka kwao na jamii wanayoiongoza. Hali hii inajitokeza pia katika tawala za mikoa na uongozi vijijini na mijini. Pale chama tawala kinapofika mpaka huku nacho kikawa ni chama-dola basi hakuna lolote la maana kidemokrasia litakalopikwa na kuiva huko.
Ili demokrasia ya kweli iwepo ni muhimu kutenga kabisa shughuli au kazi na wajibu wa serikali mbali na ule wa chama tawala. Hili linawezekana linataka tu kutambua kuwa chama tawala ni sawa na chama mbadala kinginecho chochote ambacho nacho pia siku moja kinaweza kuwa chama tawala. Usawa huu unawalinda wote kwa kuhakikisha kuwa hakuna anayepora nguvu na mamlaka zaidi ya yale ya kuwa chama mara anapopewa kuongoza serikali. Aghalabu hili husaulika sana na vile vyama vinavyodhani vitakaa madarakani milele. Lile linaloitwa BARAZA LA MAPINDUZI visiwani Unguja na Pemba kwa sasa ndio tishio kubwa kuliko kitu kingine chochote kwa demokrasia na hususan Visiwani. Baraza hilo ambalo ni taasisi iliyopitwa na wakati linaendelea kuwepo bila kujua wajibu wake siasa za sasa za nchi.
Limeendelea kuishi katika ukale na kuongoza kutokana na historia badala ya kuongoza kulingana na visheni na misheni mpya katika mfumo wa vyama vingi. Zanzibar ambayo ina nafasi kubwa ya kushindana na nchi kama zile za UAE ikiwemo Dubai, Sharijah, Bahrain na kadhalika leo inakwaza kutokana na siasa za dhuluma na uonevu zinazoendeshwa visiwani humo na hasa zile zinazonuia kumnyang'anya mtu haki zake za kikatiba. Ni dhahiri kwamba baraza hilo ni kikwazo kwa mabadiliko ya kweli na ya dhati yanayoweza kuwa chachu muhimu ya kuwaondoa Wazanzibari wote kutokana na udhalili na uhitaji wao karibu katika kila nyanja ya maisha.
Na sio hilo tu vijana wengi wa Kizanzibari ambao leo wanakwepa nchi yao watakuwa na kila sababu ya kurudi au kwa namna moja au nyingine kuchangia vitu vya maana katika maendeleo ya nchi mama yao. Kwa kurubuni, kutapeli na kudhulumu haki za baadhi ya wanajamii uongozi uliopo hauoneshi ujanja bali upofu na uziwi juu ya kule dunia inakoelekea siku hizi. Ikumbukwe kwamba unaweza kubabaisha kundi fulani la watu leo na kesho lakini huwezi kubabaisha makundi yote ya watu wakati wote na unafiki na uzandiki wako usijulikane.
Na aghalabu hata yule unayemtuma kudhulumu anaweza akawa si wako ila kwa kukuogopa anatekeleza amri ya kafiri apate mradi wake. Na kwa siasa hizi ni rahisi kujikuta umezungukwa na wanafiki kuliko wacha Mungu na wapenda utu na haki za binadamu. Matokeo ya hili ni kuwa na wakubwa wanaovunja sheria lakini ukawalinda kutokana na upofu na uziwi ulio nao. Hakuna binadamu mwenye akili zake timamu na uwezo wa kuleta mabadiliko yeye mwenyewe anayeweza kukubali dhuluma na mabavu siku zote. Iko siku atajibu.
Na siku hiyo isije ikawa ya kusaga meno. Hakuna anayekubali siasa za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kama ni motokari sasa watu watakuwekea mawe usishuke zaidi ya hapo ulipoteremka ukirudi nyuma. Unafiki mara nyingi ni dalili za uongozi dhaifu usio na dira ya kule unakoweza kuwafikisha wanaoongozwa. Katika kutapatapa na kuhangaika basi huishia kuvuruga na kuchafua na hivyo kuwatia wananchi umasikini na ukiwa zaidi. Maendeleo ya nchi hayawezi kamwe kuletwa na ubinafsi, choyo, jeuri, kiburi, ujibari na dharau kama hiyo ndio tabia ya viongozi.
Katika dunia hii hii imewahi kutokea utawala wa wezi katika nchi fulani pale wananchi walipodanganyika na walipojisahau na kushindwa kutimiza wajibu wao. Ni dhahiri pia katika miaka hii tunaweza kushuhudia uongozi wa wahuni, waongo, wababaishaji na hata watu wajinga pindi nasi tutakapojisahau na kudhani kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Kikwazo kingine kikubwa kwa demokrasia ni ujinga wa watu juu ya Demokrasia Vijijini.Uchumi na siasa zetu zimekaa kwa namna ambayo wananchi vijijini bado kabisa kujua faida na manufaa ya mfumo wa vyama vingi. Walioko madarakani wametumia fursa hii kuonyesha tu kasoro na hasara za mfumo wa vyama vingi.
Na kutokana na kiwango chao cha elimu na kukosa huduma muhimu za mawasiliano kama vile magazeti wanayomudu kununua, redio na televisheni basi wanakuwa na uwezo duni wa kuchambua na kutathmini wanayoambiwa na viongozi wapita njia au wale wa kwao vijijini. Katika hili ni dhahiri ipo haja ya kuweka mkakati wa elimu na njia za kufikisha elimu kwa wananchi vijijini wakati wote ili wawe wanaendelea kufunguka macho na masikio juu ya manufaa ya demokrasia katika maisha yao ya kila siku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment