NCHI yoyote ile inayotaka kuendelea kwa utaratibu mzuri au kwa njia za kistaarabu inapashwa kuangalia kwa makini na karibu sana miingiliano kati ya watu na vitu
ili pasitokee migongano isiyo ya lazima katika jamii.
Wakati huo huo, tunapozungumzia utawala bora hatuzungumzii juu ya wakubwa na matajiri kuishi maisha ya anasa zaidi.
La hasha. Utawala bora ni kuhakikisha
mwananchi wa kawaida anayepanda daladala anapanda daladala na kusafiri kwa staha, heshima na salama; mtembea kwa miguu anapita kwenye njia yake bila
kukerwa kwa sababu kuna daladala zilizo juu ya sheria; au jamaa wa usalama barabarani wanaachiwa kuwageuzia watu kibao kwa sababu ya kitu kidogo.
Hili ndilo jukumu mama kwa serikali yoyote linapokuja suala la watu na jamii. Ni jukumu la serikali kuona kuwa miingiliano kati ya mtu na mtu, mtu na watu wengine,
mtu na kampuni, mtu na serikali, mtu na vyama vya kisiasa, mtu na vyombo vya usafiri haisababishi hasara kwa mtu mmoja na faida kwa watu wengine.
Hapo panakuwa hakuna haki wala usawa mbele ya sheria.
Inaeleweka kabisa kuwa nauli ya mpanda daladala anayolipa inampa haki ya kupanda basi zuri na sio mkweche ambao hauna madirisha, waipa na wakati mwingine kuna mbao na mawe badala ya viti. Aidha abiria akishalipa nauli yake kusafiri na treni au meli au ndege anastahili kuondoka na kufika kwa muda uliopangwa na sio vinginevyo.
Lakini katika hili lipo ombwe kwa sababu hapo awali mashirika mengi yalikuwa yakimilikiwa na serikali. Leo mashirika hayo ni mali ya watu binafsi. Ingawa sheria zinamlinda mwenye basi, ndege, treni au meli hazimlindi na wala hazimpi haki yake ya fidia abiria na mwananchi kwa ujumla.
Hili linajulikana na linasemwa. Hata hivyo, hakuna masikio yanayosikiliza wala haielekei kama kuna akili, busara na hekima zinazolitafakari achilia mbali kulifanyia
kazi suala hili. Halina maslahi kwa wabunge au wakubwa wengine kwa hiyo nani wa kulibebea bango? Ni pale yanapowakuta jamaa zao wa karibu ndio mtu
atakurupuka na kuanza kula kiporo.
Migongano na matatizo mingine katika maingiliano hukwamisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha heshima ya nchi kama taifa lililostaarabika huwa
mashakani.
Nimewahi kuzungumzia huko nyuma kwamba, kiwango cha ustaarabu katika jamii kwa kiasi fulani huweza kuonekana katika barabara zetu na jinsi ambavyo ama
wote wanafuata sheria au pale wachache wanapokuwa juu ya sheria. Na hili likakubalika kama ndio utamaduni wa jamii husika.
Bwana mmoja anayeishi sasa huko Marekani nusura agongwe nyuma hivi majuzi kwa kuwa kazoea kuwaheshimu sana waendao kwa miguu. Maana sheria
ndivyo zitakavyo. Bwana huyu pamoja na kuponea chupuchupu kubamizwa, hata hivyo, aliangushiwa matusi mzomzo kisa kikiwa yeye kutaka kuonesha
ustaarabu barabarani kitu ambacho kwa Tanzania hivi sasa kimekufa.
Tatizo kama hili haliwezi kuacha kutokea ikiwa viongozi wa juu hawajui hali halisi katika barabara zao. Na linapotokea ombwe kwamba, haijulikani ni wizara au
idara au mamlaka ipi inawajibika na suala la ustaarabu na uungwana barabarani basi inakuwa kizaazaa kitupu.
Lakini bila shaka kuna wizara husika. Na pengine ipo pia idara husika. Na inawezekana kabisa kwamba, pia kuna mamlaka pengine zaidi ya moja zinazostahili
kushughulikia ustaarabu na uungwana barabarani. Lakini kwa sababu moja au nyingine hakuna anayeonekana kufanya kazi pamoja na malalamiko ya kila siku
ya wananchi.
Panaonekana pana ombwe. Je, ni rais tena anayetakiwa ashuke huko aliko ili barabara na njia zetu zitumike kwa nidhamu na ustaarabu? Pengine mawaziri, wakurugenzi na mameneja wahusika hawajui dhamana kubwa wanayobeba kwa niaba ya taifa hili.
Ni dhahiri kwamba, kama Tanzania itashindwa kusimamia suala la barabara na usafiri kwa namna ya kistaarabu na kitaaluma ili kuondoa kero na maudhi yanayotishia amani majiani basi hata aina ya uongozi na nchi tutakayokuwa nayo itakuwa sawa tu kama vile hali katika barabara zetu na usafiri wetu zilivyo. Hivi serikali ikiamua kweli itashindwa kuhakikisha kuwa ni mabasi yanayostahili kuitwa mabasi kikweli ndiyo yanayobeba abiria.
Hivi sasa kuna 'hatari' chungu nzima zinazoitwa mabasi zikifanya kazi ya kubeba, kama sio kuhatarisha roho na miili ya watu. Nchi hii na jina lake kubwa imeshindwa kabisa kuona kwamba madereva wanaheshimu 'ZEBRA CROSSING!' alama ambayo inaheshimiwa duniani kote.
Na mtu anapokuwa kando yake ni lazima gari lisimame hata mtu huyo akiwa mtoto mchanga. Hivi wizara na idara husika zinaweza kusema nini juu ya hili? Zimeshiba mno
kwa fedha za serikali na hazihitaji faini inayoweza kupatikana kwa kuwatoza madereva wakorofi wasiosimama kwenye zebra crossing?
Katika hali ya sasa ya mchafukoge mabarabarani imekuwa ni jambo la kawaida madereva wa daladala kutumia njia za wenda kwa miguu na hivyo kuhatarisha usalama wao. Je, hii ni haki na huu ni ustaarabu na uungwana barabarani?
Serikali hiyo hiyo inaonesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kudhibiti kiburi cha madereva na makonda wa daladala kutovaa yunifomu. Hivi watu wa nje wanatuonaje kwa kuona tuna madereva na makonda wanaovaa masembere huku serikali kupitia vyombo husika ina kila sababu ya kuhakikisha kuwa watu hawa wanavaa na wanapendeza na sio kuwa chanzo cha kipindupindu na magonjwa mengine kwa abiria?
Inaelekea kama kazi kubwa ya idara ya usalama barabarani hufanyika barabarani. Lakini nina hakika kuwa inawezekana kabisa pasiwe na kusimamisha magari ovyo barabarani na tukawa na magari yanayofaa kuwepo barabarani kwa kufuata utaratibu wa kalenda wa kupeleka magari kuchekiwa na wakala ambaye atawajibika kibima atakaporuhusu gari bovu kubeba abiria.
Aidha adhabu zinazotolewa kwa madereva na watumiaji barabara wengine wakorofi ni ndogo mno kiasi kwamba wengi wao wanazidharau. Huko Ulaya na Marekani (kama tukipata fursa ya kwenda kujifunza) yapo makosa ambayo humpeleka mtu ndani bila faini na akitoka huko hatakaa tena afanye kosa hilo.
Baadhi yetu, inavyoelekea tunaogopa au tunajipendelea kwa namna fulani na sheria zetu kuhusu usalama barabarani kama zilivyo nyingine zinaonesha ni usanii wa hali ya juu
tu. Na hali ya barabarani pamoja na kero na maudhi yake mengi kwa watumiaji wa kawaida wa barabara ambao magari mengine hayawezi kusimamishwa ili wao
wapite inaendelea kuwa ile ile kama ilivyokuwa jana na itakavyokuwa kesho.
Hivi sasa mwananchi jijini Dar es salaam anatumia saa mbili au tatu kwenda kazini na saa hizo hizo kurudi nyumbani. Mtu huyu anakuwa kachoka, taabani akifika kazini. Na hivyo ana hatari ya kuonekana hatimizi wajibu kazini. Akirudi nyumbani ndio kwisha kabisa. Ana hatari ya kutimiza majukumu yake ya unyumba. Ipo hatari kwa hiyo ya kuvunja familia za maelfu kama sio malaki ya wanajiji. Hili sio suala la kulifanyia mzaha na la ngoja ngoja. Litatutokea puani!
Nimalizie kwa kunadi kwa mara nyingine tena kwamba bila usafiri wetu na barabara zetu hapa Tanzania kuwa za kitu cha kistaarabu sio serikali wala nchi wala watu wetu wataonekana wastaarabu mbele ya macho ya dunia. Heshima yetu kama nchi na taifa itatokana kwa kiasi kikubwa jinsi tunavyojenga kuheshimiana,
kuthaminiana na ustaarabu kwenye vyombo vya safari na katika barabara zetu. Mengi yamesemwa kuhusu nchi hii kuwa na utawala wa kisheria. Hali halisi sio sawa na riwaya za wanasiasa majukwaani na kwenye makongamano. Ukitaka
kujua utawala wa kisheria hamna Tanzania tazama barabarani na kwenye vyombo vyetu vya usafiri. Utawala wa kisheria hauji kwa kutaka kuwapendeza watu au kwa kutamani tu. Utawala wa kisheria huja kwa kuzifanya sheria zilizopo juu ya kusimamia masuala fulani zifanye kazi na kila mtu aone zinafanya kazi.
Na pale ambapo sheria mpya inahitajika au mbovu kuondolewa jambo hilo lifanyike fumba na kufumbua. Lazima viongozi waondoe dhana inayojengeka miongoni
mwa watu hivi sasa kwamba viongozi wanaachia sheria nyoronyoro kwa kuhofia na wao pia kunaswa na sheria kama sheria hizo zitakuwa sheria ngangari.
Nisingelipenda kuamini hivyo na ninaamini pia Watanzania wenzangu wasingelipenda kuamini hivyo na kwamba viongozi wetu wanatamani na wao kuwa na taifa
la kiungwana na kistaarabu na wako tayari kufanya lolote lile litakalotuwezesha kuwa na jamii ya kiungwana na kistaarabu isiyotanguliza ukubwa, cheo, utajiri na
ubinafsi mbele.
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment