Monday, May 23, 2011

Iundwe Mamlaka ya Usafirishaji Dar

PENGINE wanaohusika hawaelewi kwa undani tatizo la usafiri jijini. Na baya zaidi inaelekea hawaelewi au hawajapata muda wa kukaa, kutafakari na kuelewa wapi

jiji linakoelekea-na nini lifanyike ili hali hii isiendelee kuwa mbaya na kuwa ni tatizo kubwa zaidi. Kutokana na hili katika makala haya matatizo yanayoikabili sekta ya

usafiri na uchukuzi Dar es salaam kama kielelezo cha Tanzania nzima yanayoorodheshwa na kufafanuliwa.

Kisha tunapendekeza kuwa matatizo ya usafiri jijini kwa kiasi kikubwa yatapungua ikiwa sekta hii itaendeshwa na Mamlaka ya Jiji ya kusimamia usafiri na uchukuzi

jijini. Mamlaka hiyo inaweza kuwa na mabasi yake katika njia muhimu jijini na ikaachia baadhi ya njia kuchukuliwa na manispaa za Kinondoni, Temeke na Ilala

ambao wataanzisha kampuni yao ya usafiri yatakayoendeshwa kama daladala binafsi na kutoruhusu biashara hiyo kuingiza hasara hata siku moja. Watu binafsi

wataachiwa baadhi ya njia lakini kwa kuzingatia wanafuata sheria na maadili ya usafiri jijini.

Kinachozungumzwa hapa sio kigeni. Tumeona hili likifanyika kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama jijini, pale ambapo polisi waliamriwa kuanzisha kanda au mikoa

maalum ndani ya Mkoa wa Dar es salaam. Na hili ukiachilia matatizo ya udhibiti, uratibu na rasimali ndogo limeonesha tofauti fulani.

Tunachokizungumza hapa ni kwamba, japo abira wa Dar es salaam na mikoa jirani wamekuwa waaminifu na wanatimiza wajibu wao katika suala la usafiri jijini

watu binafsi wanaomiliki daladala na mabasi mengine wameshindwa kutimiza upande wao kiuwajibikaji na wanaendelea kudai hata zaidi ya haki wanayostahili

ikiwa ni pamoja na kudai haki ya kuvunja sheria na wasichukuliwe hatua yoyote. Huu sio tu kukosa uwajibikaji bali pia ni kukosa utu, ubinadamu na maadili katika

jamii.

Kwa maneno mengine, japo serikali ilikuwa na nia njema kuwakabidhi watu binafsi sekta ya usafiri jijini, lakini watu hao wamekosa shukrani na wameamua kuuma

mkono unaowalisha. Unapewa riziki na unapoanza kula, kushiba na kusaza; unaanza kukufuru bila kutambua kuwa riziki unayopewa anaimezea mate mtu

mwingine.

Watu wa Dar es Salaam wamechoshwa na tabia ya wenye daladala. Hivi sasa wanajiuliza iweje watu binafsi wanapata faida katika daladala lakini UDA ikashindwa

kupata faida. Ni uendeshaji mbovu, au kukosa udhibiti, au rasilimali zake kuporwa na nguvu zisizojulikana?

Katika miaka hii ya ujasiriamali na hususan UJASIRIAMALI WA JAMII - waliofunguka macho wanaweza na wana haki ya kudai kumilikishwa huduma za mashirika

fulani kwa wao kuwekeza au kukopeshwa na serikali au benki ili waiendeshe miradi kama hiyo ikiwa na sura ya ubinadamu na utu.

Matatizo yanayoikabili sekta ya usafiri jijini Dar es salaam ni pamoja na daladala kuwa juu ya sheria; tamaa za matajiri wenye mabasi; rushwa; uendeshaji mabasi

kiholela na usio na maadii wala utu.

Matatizo mengine ni pamoja na uchafu wa magari, madereva na makonda; mabasi yasifuata taratibu waka kujirudi yenyewe, ushindani barabarani unaohatarisha

maisha ya abiria na watembea kwa miguu.

Mnaweza mkayajadili matatizo mengine wenyewe lakini binafsi ningelipenda kuzungumzia hili la daladala kumilikiwa na viongozi na matrafiki. Tatizo hili peke yake

linatuletea kisheria kitu kinachoitwa 'conflict of interest'. Je, wakati wa mzozo kati ya SUMATRA na wenye daladala kiongozi au trafiki mwenye daladala atasimama

upande gani?

Tafakari! Ila ukweli unabakia kuwa kwa kuifanya sekta ya usafiri jijini iendeshwe na watu binafsi tumekaribisha pia watumishi na viongozi wa umma waingie katika

biashara hiyo na hivyo kuviza na kutia uburu nguvu za udhibiti na usimamizi wa serikali juu ya sekta hiyo.

Serikali na sekta ya Usafiri
Kwa bahati mbaya serikali yetu haina sifa nzuri katika usimamizi na uendeshaji wa sekta za usafiri na uchukuzi. Kinachoshangaza, hata hivyo, ni kuwa hatujawahi

kusikia lolote kuhusu kwanini serikali ilishindwa na inashindwa kuendeleza kwa faida sekta hizi.

Tatizo ni nini? Rasilimali Watu ? Uwekezaji? Uingiliwaji kisiasa? Viongozi na watumishi kusafiri au kubebewa mizigo bure? Udhaifu katika uongozi au udhibiti, au

kitu gani?
Kwanini daladala za watu binafsi zinapata faida lakini za serikali zisipate ? Kwanini Precision Air inaendelea huku ATCL inadidimia? Kwanini kampuni yetu ya meli ni

holelaholela ?

Pamoja na majibu yatakayotolewa, ukweli ni kwamba, serikali kuu na serikali za mitaa zina uwezo; kwa sababu na faida katika kusimamia na kuendesha huduma

za usafiri hapa jijini kama zitasimamiwa na kuendeshwa na watu waadilifu ambao hawataingiliwa na wakubwa kisiasa.

Na kama serikali inashindwa kufanya hivyo basi kama ilivyoweza kuanzisha mashirika ya umma kwa kutumia kodi ya wananchi inatakiwa pia isaidie manispaa na

wakazi wa Wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala wanaotaka kuwa na kampuni zao za usafiri ili wananchi wote wasafiri kistaarabu na kwa usalama zaidi kuliko ilivyo

sasa chini ya mfumo wa usafiri ambao kila daladala inamilikiwa na mtu asiye na utu kwa wateja wake.

Usafiri jijini na Ujasiriamali jamii
Waliopata mwanga na wanaojua juu ya dhana ya ujasiriamali jamii wakati umefika wa kuanza kuwaamsha wakazi wenzao wa jijini Dar juu ya uwezekano wa wao

kumiliki kampuni zao za usafiri hapa jijini kwa pamoja kwa faida yao wote.
Kampuni hizi zitaendeshwa na wataalamu waliofuzu masuala ya usafiri na uchukuzi chini ya baraza la wanahisa ikiwemo wawakilishi wa serikali kuu, serikali za

mitaa, benki kuu, benki iliyotoa mikopo na wawakilishi wa wananchi waliowekeza pia.

Kilal waajiriwa wawili watapewa basi moja na malengo ya kufikisha kwa siku. Udhibiti na ufuatiliaji utakuwa ni wa kila siku kama wenye daladala binafsi

wanavyofanya. Benki iliyotoa mkopo itafanya kazi pamoja na watu kama M-Pesa ambapo kila siku dereva-konda hao watatuma benki mapato ya siku hiyo kupitia

simu zao za mkononi kwa wakala wa M-Pesa aliye karibu au tawi la benki lililo karibu. Kwa namna hii ufujaji mapato wa mabasi hayo utadhibitiwa kwa kiasi

kikubwa. Na vile vile kurahisisha utoaji mikopo siku zijazo kwa ununuzi wa mabasi mapya.

Serikali kuu na Benki Kuu zitakuwa na dhamana ya kugarantii mikopo kutoka benki kwa kampuni mama nchini-Kampuni ya Usafiri Tanzania (UTA) na kampuni za

wilaya tatu za Dar es salaam.

Majibu ya ndani kwa matatizo yetu
Watanzania wengi wamejenga tabia ya kutegemea majibu na ufumbuzi wa matatizo yao yatoke nje. Hili sio jambo sahihi. Kama tunataka tuifikie barabara ya kweli

kuelekea kwenye maendeleo ni muhimu tuanza kutafuta majibu ya ndani kwa matatizo yetu yote.

Ingelikuwa jambo zuri kama serikali hii ingelifanya mpango wa kuwapeleka vijana wetu kwenda huko Kenya ili waone jinsi vijana wa nchi hiyo wanavyojitahidi usiku

na mchana kutafuta majibu ya matatizo yao ya kimaendeleo. Ni mfano wa kuigwa, na tutakuwa tumepata hasara kubwa tusipokwenda kujifunza kutoka kwao.

Ninaamini viongozi wa NMG watakuwa zaidi ya tayari kupeleka vijana wetu Kenya kuona wenzao waliogundua uzalishaji umeme kwa upepo, mitambo ya redio

kwenye sanduku, mifuko ya kuhifadhi kinyesi Kibera, mitambo ya kurejelea taka na kadhalika.

Ingawa matatizo ya usafiri yapo dunia nzima lakini nchi kama Tanzania haina sababu ya kurudia makosa yaliyofanywa na wengine. Kwa pamoja serikali, wananchi,

serikali za mitaa na kampuni binafsi inayowezekana kufanyika ili kuifanya sekta ya usafiri jijini kuwa sio tu jambo la kutujengea heshima bali pia jambo la kuwavutia

watalii na majirani zetu kuja kututembelea mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment