MTANZANIA mmoja aliyewahi kwenda Ulaya alinifanya niamini kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya binadamu wa sasa na wale wa zamani.
Yeye aliniambia kwamba, jambo lililomshangaza ni kukuta madaraja makubwa na mazuri, makanisa, majumba ya kifalme na kitajiri na majengo mengine mengi
yaliyojengwa miaka mia tano au zaidi iliyopita. Kilichomshangaza ni kuwa wakati huo hakukuwa na zana na vifaa vya ujenzi kama vilivyopo leo. Akawa anajiuliza
kwanini watu hao enzi hizo za teknolojia duni walitengeneza madaraja na Watanzania waleo wanashindwa?
Maajabu ya binadamu wa kale kujenga vitu vikubwa na vya kushangaza sio tu yapo Ulaya, bali yapo pia Uchina, Japani, Russia, India, Amerika ya Kusini na
Kaskazini na hata Afrika ikiwemo majengo yaliyopo huko Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar.
Ni kitu gani walichokuwa nacho binadamu wa miaka hiyo kiasi cha wao kufanya makubwa, lakini sisi tunashindwa?
Njia na vyombo vimebadilika. Lakini matatizo yalikuwa ni yale yale. Kama ni usafiri wao walitumia majahazi au farasi au punda au ngamia au tembo na magari
yaliyovutwa na wanyama hao.
Leo tunatumia magari, meli na ndege lakini matatizo yetu ya usafiri ni makubwa kuliko ya kwao.
Wagiriki na Warumi walijenga barabara kwa kutumia mawe, udongo na mchanga na zikapitika kwa watu na magari ya farasi. Leo sisi tunashindwa kufanya hivyo
na hasa huko vijijini kuliko na shida kubwa ya barabara.
Watu walijenga madaraja makubwa kwa kutumia miti na mawe. Leo tuna saruji, kreni na mitambo mingine, lakini ni ngoma nzito kujenga daraja la uhakika sehemu
yoyote nchini.
Watu hawakuwa na matrekta lakini walilima mashamba makubwa na wakavuna chakula cha kutosha kwa matajiri na masikini. Hivi leo pamoja na elimu yetu yote
tukiwa na vyuo vya kilimo njaa inaweza kulipuka wakati wowote.
Watu walijenga mabwawa na wakahifadhi maji ya kutumia kwa muda mrefu hata pale palipotokea ukame, leo maji kila kukichwa yanatiririkia baharini au maziwani
na miradi ya umwagiliaji maji haioneshi kufanya kile ambacho Wamisri wa kale wala Wasudan wa leo wanachoweza kukifanya.
Ukitafakari haya yote nadhani utaona kwamba, kuna tatizo mahala fulani ambalo ndilo linalochangia umaskini wa Tanzania na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Wengi wamekwishaandika juu ya kwanini Waafrika ni masikini. Sababu kubwa zilizotolewa ni pamoja na nchi zilizoendelea na hususan Ulaya na Marekani
kuzinyonya nchi masikini; Afrika kuathirika kwa unyonyaji wa ukoloni; Afrika kukosa wasomi na wataalamu; Afrika kukosa teknolojia;kukosa masoko ya bidhaa zake
kwa bei nzuri na ya haki.
Baada ya miaka 50 ya Uhuru huu ni wakati muafaka wa kuziangalia tena sababu hizi na kuona kweli kama ndio chanzo cha Waafrika kuwa maskini kuzidi watu
wote duniani. Au kuna mambo mengine yaliyojificha na ambayo tunastahili kuanza kuyafanyia kazi.
Mimi sina majibu ya maswali nitakayouliza na siamini kama ndio maswali pekee ya kuuliza. Isipokuwa kuuliza na kujibu ndio njia mwafaka ya kupata majibu juu ya
swali kwanini sisi ni masikini. Hebu tujiulize basi na kisha tujaribu kujibu maswali haya:
• • Umaskini wetu unachangiwa kwa kiasi gani kwa maneno katika visheni yetu kutofanana na kile kinachofanyika kila siku nchini kwa kuwa na
ramani ya maendeleoya nchi?
• • Je, kutegemea misaada kumetulemaza na kutufanya tushindwe kujikwamua na umaskini kwa kiasi gani?
• • Je, nchi za Magharibi na nyinginezo zinazokubali kuficha fedha za marais na viongozi wengine wa Afrika walizowaibia wananchi wao
hazisaidii kuongeza umaskini wetu ?
• • Umaskini unaweza kupungua kwa kuwa na mtazamo finyu wa ndani zaidi unaoshindwa kuielewa dunia ya utandawazi na jinsi ilivyo muhimu
kutafuta maendeleo kupitia rasilimali zenu wenyewe na zile za watu wengine au watu wa nje? Jinsi gani tunavyoweza kuwatumia watu wa nchi zingine kuijenga
nchi yetu iwe ni walimu, wahadhiri, wahandisi, madaktari, wataalamu wa kompyuta na kadhalika-ili mradi shule zetu zina wanafunzi toka nje na hospitali zetu zina
wagonjwa toka nje ?
• • Je, tabia ya uvivu na kutosheka na kukata tamaa kwa baadhi ya watu wetu ama kutokana na hulka yao wenyewe au kutokana na yale
yanayofanywa au yasiyofanywa na viongozi wao yanachangia kwa kiasi gani umaskini wetu?
• • Je, bila kuendeleza vipaji na utundu wa ubunifu, ugunduzi na uvumbuzi wa vijana wetu ili hatua kwa hatua waweza kuzalisha vifaa, zana,
mashine na mitambo mbalimbali tunayohitaji sisi wenyewe tutaendelea?
• • Je, watawala na matajiri wanaweza wakawa ndio maamiri jeshi wa kuongoza mapambana na umaskini au wao kwa sababu wanazozijua
wangelipenda zaidi kutawala masikini kwa kuwa ni rahisi kufanya hivyo?
• • Je, umaskini unaweza kuondoka huku nchi ikiwa bado haiwezi kutengeneza barabara zake yenyewe achilia mbali reli, bandari na viwanja vya
ndege? Nchi ikiwa bado inategemea misaada na wataalamu toka nje kujenga viwanja vyake vya michezo?
• • Je, umaskini kweli utakwisha huku kila kifaa, mashine, mtambo na kadhalika vinavyotumika nchini vinaagizwa kutoka nje ?
• • Je, umaskini utakwisha wakati maji kitu kinachoweza kuwatoa wengine toka kwenye umaskini ni tatizo kubwa kwa baadhi ya maeneo nchini
wakati nchi imezungukwa na maziwa makubwa yaliyomo barani Afrika?
• • Je, umasikini utakwisha wakati nchi hii imeshindwa kutengeneza hata baiskeli? Achilia mbali matrekta, motokaa, malori, treni, meli, ndege na
kadhalika? Kila chombo unachokiona nchini kinatengenezwa nchi za nje! Si raia, si jeshi hawapati mafunzo kwa vitendo ya kutosha na ya hali ya juu kabisa wala
rasilimali za kufungua, pangapangua, kunyambua kitu kama vile trekta au lori na kisha kuwa na trekta au lori letu wenyewe kama wenzetu Korea, India, Uchina
walivyofanya?
• • Wakati ni asilimia 5-12 ya wananchi ndiyo wanaopata umeme tena si wa uhakika. Shirika lenyewe likiwa limekaa mkao wa kukamua damu
toka kwenye jiwe, kwa mana ya kuwanyonya kupita kiasi wateja wachache waliopo. Tutafika kwa namna hii kweli?
• • Barabara na masoko kwenda vijijini bado ni tatizo na hapaonekani programu maalum ya kuweka jambo hili katika kaburi la sahau hivi karibuni
Je, kwa namna hii kuna njia ya wakazi wa vijiji kuuaga umaskini wao?
• • Hivi tunaweza kuendelea wakati tunatumia lugha ya kigeni ambayo labda ni asilimia tano tu ya watu wetu wanaielewa? Ni nini mchango wa
matumizi ya lugha ya Kiswahili na hususan katika kumfanya kila Mtanzania kupata elimu muhimu ya maisha ikiwemo uchumi, utawala/uongozi, menejimenti,
nadharia ya masoko, nadharia ya uzalishaji mali, nadharia ya masoko na vitu kama hivyo?
• • Matumizi ya kifahari kama vile ununuzi wa magari makubwa au sherehe ambazo fedha zake zinaweza kuwatoa wanakijiji wote katika kijiji
fulani toka kwenye umaskini milele?
• • Tutaumaliza umaskini wakati viongozi ni wabinafsi na wanatanguliza maslahi yao mbele ya kitu na hawafikirii kuwatoa kwanza wananchi
kwenye umaskini na wanangojea miujiza wananchi waondokane na umaskini wao wenyewe. Watu hawataishi kwa mkate wa siasa peke yake?
• • Je umaskini utakwisha pasipo kujengea kila familia nchini angalau nyumba moja ya vyumba viwili ambayo wataiendeleza wao wenyewe
baadaye ili sasa watu washughulike na uzalishaji mali na sio tena kila Mtanzania kuwa na mradi wa kujenga nyumba mwaka nenda mwaka rudi?
• • Je, umasikini utakwisha bila kugeuza wilaya na mikoa ili ijiendeshe kama makampuni kwa kupanga cha kufanya na jinsi ya kujitathmini kila
baada ya miezi mitatu?
• • Je, bila kuwa na hospitali na hasa zilizopo katika miji mikubwa na ile ya mipakani zinazotibu wagonjwa toka nchi za nje umasikini utakwisha?
• • Je, bila kuwa na shule na vyuo ambavyo vinapokea wanafunzi wengi kutoka nchi za nje badala ya sisi kuwa ndio tunaopeleka watoto wetu
nchi za nje, je, umaskini utakwisha?
• • Je, bila kuwa na majeshi ikiwemo JKT inayoweza kuchangia katika uzalishaji mitambo na mashine muhimu vikiwemo matrekta na malori; JKT
kutoa huduma muhimu za jamii, ulinzi na usalama ikiwemo usalama barabarani, kutunza wazee, watoto/mayatima na kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mali
kikwelikweli zitakazorahisisha maisha yao na ya wananchi kwa ujumla tutaupa umaskini?
Monday, May 23, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment